Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge wang’aka ukosefu wa madawati shule za msingi

Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa akijibu hoja za wabunge kwenye Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi iliyowasilishwa April 22, 2025 jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Wametoa kilio hicho wakati wakichangia kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa mwaka 2025/26, wakishauri mkakati maalumu wa kuondoa upungufu huo.

Dodoma. Upungufu wa madawati katika shule za msingi umezua mjadala bungeni baada ya wabunge kuibua vilio wakisema ni aibu Taifa kuendelea kuzungumza jambo hilo.

Katika michango ya wabunge leo, Jumanne Aprili 22, 2025, baadhi yao wameitaka Serikali ifikirie upya mkakati wa kumaliza upungufu huo.

Kilio cha upungufu wa madawati kilianza Aprili 17, 2025, siku ya kwanza ya mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa. Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje alisema Taifa linapata aibu kwa wanafunzi kuendelea kukaa chini.

“Pamoja na mambo mazuri yanayofanywa na Serikali hii, lakini ni aibu kubwa zaidi ya miaka 64 ya Uhuru bado tunazungumzia upungufu wa matundu ya vyoo na uhaba wa madawati, hili linatia doa,” alisema Hanje.

Mbunge huyo alifananisha maeneo ya wanafunzi kujifunzia na jengo la Bunge ambalo alisema limezungukwa na vyoo kila kona baada ya kuona umuhimu mkubwa wa huduma hiyo.

Leo, Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu (CCM), ameibua tena hoja hiyo akitaka kujua kwa nini Tamisemi imeshindwa kumaliza uhaba wa madawati kwa shule zake.

Tabasamu amesema baadhi ya maeneo nchini misitu imejaa, lakini bado idadi kubwa ya wanafunzi wanaendelea kusoma kwa kukaa chini.

“Halmashauri zitengewe fedha za kutosha kwenye madawati jamani, hii ni aibu kubwa tena ya nchi, kwani baada ya miaka zaidi ya 60 ya Uhuru eti tunashindwa kuwanunulia madawati wanafunzi?” ahoji Tabasamu.

Mbunge huyo ameitaka Tamisemi kutoa maagizo kwa halmashauri zote ili zinapotenga bajeti zake kwa mwaka, iwalazimishe kutenga fedha kwa ajili ya madawati, na ametolea mfano wa jimbo lake kwamba kila dawati moja linatengenezwa kwa Sh60,000.

Kwa upande wake, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya (CCM), amezungumzia upungufu wa madawati kwamba bila kuwa na mkakati wa kutosha, upungufu changamoto hiyo itaendelea kuwa kilio cha kudumu.

Dk Chaya, ambaye amesema aliwahi kuwa mshauri wa masuala ya Tamisemi, haoni mkakati wa makusudi katika kumaliza kilio cha madawati, hasa wakati huu ambao majengo mazuri ya shule yanaendelea kujengwa.

Kwa maelezo ya Dk Chaya, ili kumaliza tatizo hilo ni muhimu Tamisemi wakaja na mkakati maalumu wa kumaliza tatizo na iwashirikishe wadau.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko, ameitaka Serikali kuangalia utaratibu wake inapopeleka fedha za kujenga majengo mazuri, ipeleke na bajeti ya madawati.


Majibu ya naibu mawaziri

Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainabu Katimba, amezungumzia suala la ajira kwa walimu, akisema katika kipindi cha miaka minne Serikali imetoa ajira kwa walimu 45,742 wa shule za awali hadi sekondari.

Amesema pia Serikali inaendelea kusimamia utaratibu wa kutoa ajira za mkataba na kuwatumia walimu walioko katika mafunzo ya vitendo ili kupunguza uhaba wa watumishi.

Kwa mujibu wa Katimba, Serikali imejenga majengo mengi ya shule za msingi na sekondari na itaendelea kufanya hivyo, licha ya ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi kutokana na mfumo wa elimu bila malipo.

Katika majibu yake, Naibu Waziri Festo Dugange amesema katika kipindi cha miaka minne kazi kubwa imefanyika, hasa katika ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, ikiwemo ongezeko la idadi ya watumishi katika sekta hiyo.


Majibu ya Waziri Mchengerwa

Akijibu hoja za wabunge, Waziri Mchengerwa ameitaja hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, kuwa ni cheche za kisiasa, huku akisema hakuna hata senti moja ya wananchi iliyopotea.

Mchengerwa amesema atatoa taarifa sahihi kwa muda atakaokuwa amepangiwa na Spika kuhusu tuhuma za Gambo, lakini akaonya wabunge wasipende kutumia majukwaa kufanya kiki za kisiasa na kuacha kuhukumu kwa jazba, kwa sababu Tamisemi haitakuwa tayari kuvumilia mambo hayo.

Katika mchango wake, Mrisho Gambo aliibua tuhuma kuwa katika ujenzi wa jengo la utawala na soko jijini Arusha, fedha nyingi zilitumika vibaya, akaomba uchunguzi wa kina ufanyike kwenye maeneo hayo.

“Mheshimiwa Spika, niseme tu maneno ya mwisho katika taarifa hiyo, hakuna senti ya Watanzania iliyopotea kwenye ujenzi huo, tuache cheche za kisiasa, tuhoji kwa hoja na tusihukumu kwa jazba,” amesema Mchengerwa.

Katika hoja ya matundu ya vyoo, amesema bado kuna tatizo la upungufu mkubwa kwa shule za msingi na sekondari na hadi sasa upungufu ni matundu 51,262.

Waziri ametaja kuwa upungufu huo unasababisha wanafunzi wa kiume kwa shule za sekondari kutumia tundu moja wanafunzi 35 badala ya 25, na wasichana wanatumia tundu moja wanafunzi 35 badala ya 20 kama sera inavyotaka.

Kwa upande wa shule za msingi, amesema wanatumia tundu moja wanafunzi 43 wakati mwongozo unataka tundu moja litumiwe na wanafunzi 25, hivyo Serikali imeamua kutenga Sh26.57 milioni kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 25,880 kwa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha 2025/26.

Amesema vifaa vya maabara kwa shule zote 426 za sayansi vimeshanunuliwa, na kazi iliyopo ni usambazaji kwa shule hizo, ikiwemo shule 26 za sayansi za wasichana zilizojengwa hivi karibuni.

Kuhusu malipo ya madeni na malimbikizo, amesema Serikali imekuwa ikilipa madeni kutokana na uhakiki, ambapo mwaka 2023/24 zililipwa jumla ya Sh116.08 bilioni na mwaka 2024/25 Serikali ililipa Sh78.75 bilioni.

Waziri ameziagiza halmashauri 36 zenye uwezo kuendelea kulipa malimbikizo ya madeni, wakati Serikali ikiendelea kuhakiki madeni ya halmashauri zisizo na uwezo ili yalipwe, huku akitoa onyo kwa wahusika wanaoendelea kuzalisha madeni kuacha mara moja.