Mbunge Bonnah mguu kwa mguu fidia Kipawa

Mbunge wa Jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli
Muktasari:
- Mwaka 1995 Serikali ilitangaza kulichukua eneo hilo kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege na miaka miwili baadaye ilifanyika tathmini, ambapo kutokana na gharama za fidia na uhaba wa fedha wakati huo, Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wakazi hao
Dar es Salaam. Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam, imetaka mchakato wa malipo ya fidia kwa waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kufanyika kwa haraka ili walengwa wapate haki yao.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Novemba 14, 2023; Mbunge wa jimbo hilo Bonnah Kamoli amesema ofisi yake inaufuatilia mchakato huo kwa umakini na hasa baada ya muda walioahidiwa kuwa umepita.
“Katika Mtaa wa Kipunguni, Kata ya Kipawa, kuna wananchi 1800 ambao kimsingi waliishafanyiwa tathnmini mwezi wa sita mwaka huu, na baadaye Serikali kupitia Waziri wa Fedha ambaye tuliongozana mpaka eneo husika, tuliwaambia malipo yangefanyika Septemba,” amesema mbunge huyo na kuongeza;
“Mpaka sasa hivi wale wananchi bado hawajalipwa, niiombe sana Serikali ifanikishe zoeli hili mapema, huu ni mwezi Novemba...kumbuka tuliwaahidi wangelipwa mwezi Juni...katika wananchi hawa, kuna ambao tayari wameishabomoa nyumba zao huku wakisubiri malipo.”
Kwa mujibu wa mbunge huyo, hata zile nyumba ambazo zilikuwa zinatumika kibiashara kwa kupangisha, nazo ziko tupu kwani watu wameitikia wito wa kupisha upanuzi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege.
“Kwa hiyo nimuombe Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, pamoja na mambo mengine yote wanayofanya, wananchi hawa wanahitajika kulipwa haki zao maana toka Juni wanasubiri bila mafanikio, kuharakisha malipo hayo, kutawawezesha wananchi hawa kuendelea na shughuli zingine za Ustawi wa maisha yao,” amesema.
Wakati wa kuhitimisha hoja ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2024/25 bungeni jini Dodoma November 10, 2023; Waziri Nchemba aliezea kilichochelewesha malipo hayo.
Kwa mujibu wa Mwigulu, katika uhakiki iliyofanyika kwenye madai ya fidia kwa wakazi hao wa Kipunguni, ilibainika kuwa baadhi ya watu waliishafidiwa maeneo mengine, na kwamba kufanya malipo mengine, ni kulipa fidia mara mbili.
“Sio kwamba fedha hazipo, kilichowachelewesha kulipa Septemba kama tulivyokuwa tumeahidi, ni baada ya kufanya uhakiki na iligundulika kati hao wananchi, kuna ambao walishapewa maeneo mengine lakini majina yao yalikuwepo tena katika orodha ya fidia,” alieleza na kuongeza;
“Kwa hiyo ilibidi kufanyika utaratibu ili masuala ya fidia yaweze kuendelea. Tunaamini baada ya kumaliza mzozo huo ndani ya mwezi mmoja tutaenda kulipa Kipunguni na maeneo mengine ambayo yenye kesi kama hiyo,”amesema.
Julai 7, 2023; Dk Mwigulu akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kipunguni, alitangaza kukamilika kwa taratibu zote za tathmini na kueleza kuwa tayari Serikali imesharidhia kulipa fidia hiyo kinachoendelea sasa ni hatua za ndani kabla ya watu kuanza kulipwa.
Kiasi cha Sh143.9 bilioni kinatarajiwa kutumika kulipa fidia wakazi wa mtaa wa Kipunguni kata ya Kipawa ili wapishe upanuzi wa uwanja wa ndege.
Fedha hizo zitatolewa baada ya kukamilika kwa tathmini mpya iliyoanza kufanyika Julai mwaka jana ambayo imeonyesha kuwa jumla ya watu 1865 wanatakiwa kupata fidia hiyo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kipunguni, Dk Nchemba ameeleza kuwa tayari ofisi yake imepokea barua ya tathmini na kinachoendelea sasa ni kukamilisha taratibu za ndani ili malipo yaanze kufanyika.
Mwaka 1995 Serikali ilitangaza kulichukua eneo hilo kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege na miaka miwili baadaye ilifanyika tathmini ambapo kutokana na gharama za fidia na uhaba wa fedha wakati huo, Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wakazi hao kwa awamu.