Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fidia waliopisha upanuzi JNIA yaongezeka kwa Sh22 bilioni

Muktasari:

Tathmini mpya iliyofanywa Mei 2020 baada ya ile ya mwaka 1997 inaonyesha fidia wanayopaswa kulipwa wananchi hao waliokuwa wanaishi maeneo ya Kipawa, Kigilagila na Kipunguni imeongezeka kwa zaidi ya mara nne hivi sasa.

Dar es Salaam. Ucheleweshaji ya fidia kwa kaya 1,125 zilizopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa miaka 23 umeongeza riba kwa Sh22.35 bilioni na kufika Sh29.76 bilioni.

Awali, miaka 23 iliyopita, kaya hizo zilipaswa kulipwa Sh7.41 bilioni lakini kutokana na ucheleweshaji Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema Serikali sasa inatakiwa kutoa Sh29.76 bilioni.

CAG amebainisha hilo kwenye ripoti yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya mwaka 2020/21 iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni. Kaya zinazosubiri malipo hayo ni zilizokuwa zikiishi maeneo ya Kipawa, Kigilagila na Kipunguni.

CAG amesema kutokana na tathmini ya mali iliyofanyika mwaka 1997, malipo ya fidia yalifanyika kwa baadhi ya kaya zilizopisha mradi, lakini 1,125 zilisalia pasipo kulipwa fidia ya Sh7.41 bilioni kutokana na ufinyu wa bajeti iliyotengwa kwa ajili hiyo na mpaka anakamilisha ukaguzi wake zilikuwa zinaendelea kusubiri.

Kuchelewa kulipwa kwa deni hilo kwa muda mrefu, CAG amesema kulisababisha kufanyika tathmini nyingine kadhaa ili kupata thamani halisi kuendana na mabadiliko ya muda na thamani ya fedha.

“Tathmini iliyofanyika Mei 2020 kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 13(3) ya Kanuni za Ardhi (uhakiki wa thamani ya fidia ya ardhi) ya mwaka 2001 ilifanya marekebisho ya riba ya asilimia sita kwa mwaka mpaka Septemba 2019 kutoka kwenye tathmini ya mwaka 1997.

“Marudio haya ya tathmini yalizalisha thamani mpya kutoka deni la awali na kufika Sh29.76 bilioni, likiwa ni ongezeko la Sh22.35 bilioni sawa na asilimia 302 ikilinganishwa na deni la awali. Pia, nilibaini ukokotoaji wa gharama hizi za fidia haukuwa umeidhinishwa na mthamini mkuu wa Serikali,” amesema CAG Kichere.

Imeelezwa kuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi iliingia mkataba na Kampuni ya Ushauri (Land Consult Limited kwa kushirikiana na Tan Valuers and Property Consultants) kutafiti na kutathmini mali zinazomilikiwa na kaya zilizoathiriwa na mradi wa upanuzi wa uwanja huo.

“Nashauri menejimenti ya TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege) kwa kushirikiana na mthamini mkuu wa Serikali ifanye mapitio ya kiasi cha fidia kinachopaswa kulipwa kwa kaya hizi 1,125 na kuhakikisha malipo yanafanyika bila kuchelewa kuepuka ongezeko zaidi la gharama za fidia,” ameshauri CAG.

Kichere amependekeza hivyo kutokana na ukweli kwamba madai hayo yamedumu kwa zaidi ya miaka 23 bila kulipwa hivyo kuongeza gharama za mradi huku ustawi wa maisha ya kaya zilizoathiriwa ukiendelea kuzorota kutokana na kutolipwa fidia zao kwa wakati, huku wakiwa wamepoteza mali walizokuwa nazo awali.