Mbowe kuzindua Operesheni +255 mjini Kagera

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Muktasari:
Mkutano huo wa uzinduzi utaongozwa na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi kadhaa wa kitaifa.
Bukoba. Chama Cha Democrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajiwa kuzindua operesheni yake ya +255 Katiba Mpya Okoa Bandari Zetu kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika uwanja wa Uhuru maarufu kama Uwanja wa Mayunga mjini Bukoba.
Mkutano huo wa uzinduzi utaongozwa na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi kadhaa wa kitaifa.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Bukoba, Victor Sherejei ameieleza Mwananchi leo Julai 28, 2023 kuwa pamoja na mkutano wa hadhara, hafla hiyo ya uzinduzi itaambatana na matukio kadhaa ya hamasa na ujenzi wa chama katika mitaa ya Manispaa ya Bukoba kuanzia Saa 6:00 mchana.
"Pamoja na oparasheni Class +255, hafla ya uzinduzi pia utaambatana na ukusanyaji ada kwa wanachama wa zamani na usajili wa wanachama wapya kwa kadi kidijitali,’’ amesema Sherejei
Amesema baada ya hafla ya uzinduzi, viongozi wa Chadema wa ngazi mbalimbali watatawanyika katika mitaa, kata na wilaya zote za Mkoa wa Kagera kutoa elimu na kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa Katiba Mpya.
‘’Viongozi wetu wa Kitaifa pia watapata fursa ya kuzungumza na umma kuhusu mkataba wa uwekezaji bandarini ambayo ni miongoni mwa ajenda zinazotawala mijadala nchini,’’ amesema kiongozi huyo
Sherejei amewaomba wakazi wa Mkoa wa Kagera kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa uzinduzi na mikutano mengine itakayofanyika maeneo na wilaya tofauti mkoani humo kuanzia kesho Julai 29, 2023.