Huduma ya kwanza, ulinzi vyaimarishwa mkutano wa Chadema

Hema la huduma ya kwanza lililopo katika mkutano wa Chadema leo, Temeke
Muktasari:
- Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinafanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Bulyaga, Temeke jijini Dar es Salaam, ukishirikisha viongozi mbalimbali wa kisiasa, wanaharakati, dini na wanasheria.
Dar es Salaam. Gari la kubebea wagonjwa na watoa huduma ya kwanza ni miongoni mwa viliokuwepo katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) unaojadili kuhusu uwekezaji bandari.
Haja ya kuwepo kwa wahudumu hiyoi imetokana na vurugu zilizotokea jana Jumamosi, Julai 22, 2023 wakati wa maandalizi ya mkutano huo na kusababisha baadhi ya watu kujeruhiwa wakiwemo waandishi wa habari.
Katika maandalizi hayo yaliofanyika jana kwenye viwanja vya Bulyaga Temeke jijini Dar es Salaam, hakukuwa na gari la kubebea wagonjwa wala watoa huduma ya kwanza, jambo lililosababisha waliojeruhiwa kukimbizwa hospitali kwa magari binafsi.
Kati ya waliojeruhiwa jana, pia walikuwepo waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sunday George, Fortune Francis na Omary Mhando (dereva).
Hata hivyo, uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti, The Citizen na mitandao yake mbalimbali ya kijamii, wameripoti tukio hilo, Kituo cha Polisi, Chang’ombe.
Kutokana na tukio hilo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amelaani tukio hilo akitaka vyombo vya dola kuwasaka na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kuwashambulia waandishi hao pamoja na dereva.
Jambo lingine lililoimarishwa katika mkutano huo wa leo, Julai 23, 2023 ni suala la ulinzi na usalama, kwani walishuhudiwa maofisa mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama waliozingira eneo hilo.
Katika eneo hilo ilikuwepo gari ya kubebea wagonjwa na watoa huduma ya kwanza walioweka hema tayari kwa shughuli hiyo.
Pamoja na mvua kubwa iliyonyesha muda machache baada ya kutangazwa itifaki ya kuanza shughuli rasmi, haikuwakwaza vijana wa Chadema kuendelea na nyimbo mbalimbali zilizoashiria upinzani wa uwekezaji bandari.
"Tutasimama kupinga uuzwaji bandari yetu kwa mwarabu," ni miongoni mwa maneno yaliyosikika katika nyimbo hizo, huku "Katiba Mpya ndiyo msingi wa haki" yakiwa maneno mengine.
Hadi saa 8 mchana, tayari Balozi wa zamani wa Denmark, Willibrod Slaa, Mwenyekiti wa zamani wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Wakili Mwabukusi walishawasili katika mkutano huo pamoja na viongozi wa dini.
Wengine ni wajumbe wa kamati kuu wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa, Godbless Leman a John Heche wapo kwenye mkutano huo.
Mkutano huo unafanyika kupinga uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini baina ya Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni yake ya Dubai Porty World.
Kadhalika, Bunge la Tanzania Juni 10, mwaka huu limeazimia kupitishwa kwa mkataba huo unaopingwa na baadhi ya wananchi.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia kwa viongozi mbalimbali wamesema mkataba huo hauna tatizo lolote na ushauri na au mapendekezo yanayotolewa yatachukuliwa.
Miongoni mwa viongozi wa Serikali waliozungumzia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amesema, ushauri na mawazo yanayotolewa yafanyiwa kazi wakati wa majadiliano ya mikataba ya utekelezaji baina ya TPA na DP World.