Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawakili walifikisha sakata la bandari mahakamani

Muktasari:

  • Mawakili wanne nchini Tanzania wamelifikisha mahakamani sakata la mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai juu ya uendelezaji na uboreshaji wa Bandari za Tanzania.

Dar es Salaam. Hatima ya uhalali wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai sasa kuamuriwa na Mahakama baada ya jopo la mawakili wanne kuiburuza Serikali mahakamani kupinga mkataba huo.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mjadala mkali kuhusu uhalali wa mkataba huo baina ya Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Dubai kupitia Kampuni ya Dubai Port World kuhusu uboreshaji na uendeshaji wa bandari nchini.

Juni 10, 2023, Bunge la Tanzania lilipitia azimio la kuridhia ushirikiano.

Licha ya Bunge kuridhia, mjadala umeendelea kuhusu ushirikiano huo huku Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaeleza Watanzania kutokuwa na wasiwasi kwani Serikali haitadharau maoni, ushauri na mapendezo yatakayokuwa yametolewa.

Hata hivyo, wakati mjadala huo ukiendelea kutoka kwa makundi mbalimbali, jopo la mawakili wanne wamechukua hatuza za kisheria kwa kuufikisha mjadala huo mahakamani.

Mawakili hao, Alphonce Lusako, Emmanuel Kalikenya Changula, Raphael Japhet  Ngonde na Frank John Nyalusi, wameiburuza mahakamani Serikali, kutokana na kupitisha mkataba huo kwa kile wanachodai hauzingatii maslahi ya nchi.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona kuthibitishwa na wakili Lusako leo Jumanne, Juni 27, 2023, mawakili hao wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania.

Madai dhidi ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Katibu Mkuu wake wanadaiwa kusaini mkataba huo wa kimataifa na kuupeleka bungeni kwa ajili ya kupitishwa bila kushirikisha umma na kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutoa maoni yao.

Wanadaiwa kwa kufanya hivyo wamekiuka Sheria ya Rasilimali za Taifa namba.5 ya mwaka 2017, kifungu cha 11 (1) na (2).

Kwa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu wa Bunge madai yanayowakabili katika shauri hilo ni kuwaongoza wabunge vibaya, kupiga kura ya kuitikia kwa ujumla kwa pamoja (yaani kura ya ndio) badala ya kura ya Mbunge mmoja mmoja.

Wadai hao katika shauri hilo wanadai kuwa wadaiwa hao kuwaongoza wabunge kupiga kura ya namna hiyo ni kinyume cha Sheria.

Kwa mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani, ambayo Mwananchi limeiona nakala yake, shauri hilo limepangwa kuanza kutajwa Julai 3, 2023 saa 3:00 asubuhi na Serikali (wadaiwa) wametakiwa kufika mahakamani siku hiyo bila kukosa.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 5 la mwaka 2023, limepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watu lianoloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji Mustafa Ismail na Abd Kagomba.