Prime
Taswira ya Polisi yazidi kuathirika licha ya tathmini ya Afrobarometer

Muktasari:
- Ni kutokana na mfululizo wa matukio kutokuwa na majibu ya uchunguzi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa neno.
Dar/Mikoani. Uhusiano baina ya askari polisi na raia umezidi kutia hofu kutokana na kile kinachoendelea katika mitandao ya kijamii, ikiwa ni matokeo ya namna jeshi hilo linavyoshughulikia matukio mbalimbali ya uhalifu, yanayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Hali inaonekana si nzuri hasa pale polisi wanapokutwa na madhila, ikiwemo ajali au madhara katika makabiliano na wahalifu, ambapo baadhi ya watu hueleza furaha yao mitandaoni—kitu kinachokinzana na mila, utu na utamaduni wa Mtanzania.
Hata hivyo, kinyume na mtazamo huo, Jeshi la Polisi Tanzania lilitajwa kuwa miongoni mwa majeshi bora 10 barani Afrika, kwa kuwa na weledi na kuheshimu haki za wananchi, kwa mujibu wa utafiti wa Afrobarometer uliotangazwa mapema mwaka jana.
Mijadala katika mitandao ya kijamii kama Club House, Twitter, Instagram, Facebook na makundi ya WhatsApp imejaa maneno ya kuchochea chuki yanayotokana namna jeshi hilo linashughulia matukio mbalimbali yakiwemo ya utekaji.
Tukio la usiku wa kuamkia Mei 2, 2025 la watu wasiojulikana wakiwa na silaha kuvamia nyumbani kwa mwanaharakati na kada wa Chadema jijini Mbeya, Mdude Nyagali na kumtesa kisha kutoweka naye, limeongeza petroli kwenye moto.
Baadhi ya wachangiaji wamedai licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kukana askari wake kuhusika, kwamba wanao ushahidi unaowahusisha.
“Tumewapa polisi majina ya askari watatu ambao tuna taarifa za uhakika wameshiriki kumteka na kumtesa Mdude lakini RPC kasema hawawatambui…” aliandika mmoja wa wachangiaji.
Kupitia mitandao hiyo, wachangiaji wameweka picha na namba ya simu ya askari wanayemtuhumu kuongoza genge hilo wakihamasishana "wamtembelee".
Hata hivyo, Jeshi la Polisi makuu limetoa taarifa kuwa limetuma timu ya upelelezi kufuatilia madai dhidi ya askari hao.
Matukio mengine ya karibuni yanayotajwa kuibua msuguano kati ya raia—hasa wanachama wa Chadema—na polisi ni pamoja na kupoteza kwa makada Deusdedit Soka na wenzake na kuuawa kwa mzee Ali Kibao.
Mbali na hayo, tukio la viongozi na wanachama wa Chadema kukamatwa na polisi Aprili 24, 2025 nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walipokwenda kuhudhuria kesi ya uhaini ya Tundu Lissu, kisha kutupwa porini wakiwa na wamejeruhiwa nalo limechochea uhasama.
Licha ya uwepo wa video zikionyesha viongozi na wafuasi hao wakikamatwa na polisi, wengine wakipigwa na kutupwa porini, Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilikana kufanya tukio hilo.
Hali hii imeakisi kilichoelezwa katika Tume ya Haki jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu mwaka 2023, iliyobaini kuwa taswira ya Jeshi la Polisi kwa wananchi si nzuri kutokana na malalamiko yanayohusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na ucheleweshwaji wa kufika kwenye maeneo ya matukio.
Tume ilieleza kuwa hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.
Tume ilipendekeza Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha maboresho makubwa, na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo, likibadilishwa kisheria, kimuundo na kifikra.
Hata hivyo, utekelezaji wa mapendekezo hayo unaendelea kwa mwendo wa kinyonga huku wananchi wakizidi kulinyooshea kidole jeshi hilo, chuki kati yake na raia zikiendelea kuonekana, na wengine kushangilia kila linapopata madhila.
Nafasi ya 10 Afrika
Licha ya hali hiyo, Jeshi la Polisi la Tanzania lilitajwa kuwa miongoni mwa majeshi bora 10 barani Afrika kwa kuwa na weledi na kuheshimu haki za wananchi.
Katika kigezo hicho, Burkina Faso iliongoza ikifuatiwa na Morocco, Niger, Benin, Mali, Senegal, Tanzania, Madagascar, Mauritania na Mauritius.
Mbali na kigezo hicho, pia Tanzania ilitajwa kuongoza kwa wananchi kuwa na imani na polisi, ikishika nafasi ya pili kwa wananchi kutohofia usalama wao.
Kwa matokeo hayo, Jeshi la Polisi Tanzania limeyapita majeshi ya nchi za Afrika Mashariki zikiwamo Kenya na Uganda ambazo kwa ujumla zimefanya vibaya katika vigezo mbalimbali vilivyotumiwa katika utafiti huo.
Kwa nyakati tofauti, Mwananchi limemtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Cammilius Wambura pasipo mafanikio kwani licha ya kupigiwa simu na kutumiwa ujumbe mfupi haukupata majibu.
Mitizamo ya wadau
Akizungumzia hilo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema hali ya uhasama inachochewa na Jeshi la Polisi kutumia nguvu zaidi dhidi ya raia na hivyo kuwafanya wananchi kupoteza imani kuwa jeshi hilo.
Ole Ngurumwa ameeleza kuwa njia pekee ya kukomesha hali hiyo ni kuvunjwa kwa dhana, misingi na sheria ya Jeshi la Polisi kwa kuwa asili yake ilianzia enzi za ukoloni kwa lengo la kukandamiza wananchi.
“Ibadilike kutoka kuwa jeshi la kukandamiza raia na kuwa jeshi la huduma ya usalama kwa raia kwa sababu wananchi wanawachukia askari kutokana na mabavu wanayotumia,” amesema.
“Athari nyingine ni kuwa siku moja inaweza kusababisha watu wapate hasira kali na kufanya uamuzi mgumu utakaochafua amani ya nchi.”
Kwa upande wake, Wakili Edson Kilatu amesema katika kanuni za utoaji haki, mtu hawezi kuwa jaji wa kesi yake mwenyewe.
“Kesi yako anapaswa kuhukumu mtu mwingine ambaye hana masilahi nayo. Uzoefu unaonyesha kuna baadhi ya matukio yaliyowahusu polisi yalichunguzwa na vyombo vingine na ukweli ukajulikana,” amesema.
Ameshauri ili kupata majibu kuhusu tukio la Mdude, ni lazima Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ichunguze jambo hilo.
“Polisi wanapoenda kuchunguza tayari wameshaanza kujitetea mapema. Watu wameleta majina, tunawatuhumu fulani na Fulani, badala ya kusema ‘tumepokea, ngoja tujiridhishe.’ Unasema hatuwajui, si sahihi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma amesema kinachopaswa kufanyika ni Jeshi la Polisi kufanya shughuli zake kwa weledi, kwa kufuata taratibu na miongozo yao.
“Tunaamini wakizingatia hayo wanaweza kufanya majukumu yao vizuri.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla), Tike Mwambipile, amesema utekelezaji bora wa wajibu wa Jeshi la Polisi ndiyo njia pekee ya kumaliza changamoto hizo.
Amesema iwapo jeshi hilo litafanya kazi kwa uadilifu na uaminifu bila kuwatesa wananchi, hakuna atakayefurahia maumivu yao.
Hilo pia limezungumziwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe, kuwa ili jamii irudishe imani kwa Jeshi la Polisi ni lazima yatumiwe mapendekezo yaliyowasilishwa na wadau kwa Tume ya Haki Jinai.
“Tulipendekeza kuwepo mamlaka huru ya kiraia ya kupokea mashauri dhidi ya Polisi pale wanapolalamikiwa. Tunapaswa kujifunza kutoka nchi kama Kenya wakati wa utawala wa Rais Daniel arap Moi walipokutana na
Mwenyekiti Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema vipo vyombo vingi vya kisheria na tume hiyo imepewa jukumu la kushughulikia haki za binadamu kunapotokea ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Amesema wakati mwingine matukio yanakuwa mengi na taasisi hiyo haina rasilimali watu wala bajeti ya kutosha hivyo kushindwa kufika kila mahali.
“Ni sehemu ya kazi yetu. Tunapokea malalamiko na tunashughulikia mengi, lakini yanapokuwa mengi kupita kiasi hatuwezi kufanya yote,” amesema.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Dk Juma Homera, amelielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada za kuwatafuta waliomshambulia Mdude, huku akiahidi Sh milioni 5 kwa atakayesaidia kumpata akiwa hai au amekufa.
Amesema kwa kuwa limetokea mkoani kwake, ameamua kulifanyia kazi ili kuhakikisha haki inapatikana.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka, amesema wana matumaini ya kumpata kada wao, na wanaamini waliomfanyia unyama huo walimtupa katika pori moja mkoani Iringa, kisha kumhamishia eneo jingine mkoani Mbeya.