Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM: Tumeupokea ushauri wa Warioba lakini...

Muktasari:

  • Ushauri wa Jaji Warioba kuhusu CCM , Serikali kuketi meza moja na Chadema umepokelewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, leo Jumatatu Mei 5,2025  Amos Makalla aliyesema wanakubaliana naye, lakini si kwa sasa akibainisha kuwa chama hicho hakina mgogoro na chama hicho kikuu cha upinzani na wanashirikiana katika mambo mbalimbali.

Morogoro. Siku mbili baada ya Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba kushauri kuweka meza ya mazungumzo kati ya Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema ili kumalize tofauti zao kabla ya uchaguzi, CCM kimesema kinaupokea ushauri huo lakini hakiwezi kuutumia kwa sasa.

Ushauri wa Jaji Warioba umepokelewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla aliyesema wanakubaliana naye, lakini si kwa sasa akibainisha kuwa chama hicho hakina mgogoro na Chadema na wanashirikiana katika mambo mbalimbali.

Mei 3, 2025 akizungumza katika kongamano la Uchaguzi Mkuu 2025 lililoandaliwa na Chama cha Sheria Tanganyika (TLS), Jaji Warioba na  Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, walitoa ushauri  kuwa Serikali, CCM na Chadema wamalize tofauti zao kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ushauri huo ulitokana na kile alichokisema Jaji Warioba endapo hilo halitafanyika nchi itaingia katika uchaguzi ikiwa katika mgawanyiko kuanzia viongozi na wananchi, huku akisema dawa peke yake ipo katika meza ya mazungumzo na si mapambano ya lugha zinazoligawa Taifa zilizopo sasa.

Jaji Warioba alitoa kauli hiyo wakati ambao kumekuwapo na mvutano kati ya Chadema, Serikali na CCM unaosababisha kurushiana maneno huku Chadema wakija na No reforms, no election wakishinikiza kufanyika kwa mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi jambo lililofanya baadhi ya viongozi wake kujikuta mikononi mwa sheria.


Alichokisema Makalla

Leo Jumatatu Mei 5, 2025 akiwahutubia wananchi wa Kata ya Mikese mkoani Morogoro ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya siku saba mkoani hapa, Makalla ameanza kusema wanamuheshimu Jaji Warioba ambaye ni mbobezi katika sheria lakini ushauri wake si kwa sasa.

"Nimesikia akitueleza, akitushauri CCM wakae na Chadema kumaliza tofauti, tunamuheshimu ametoa ushauri mzuri. Ushauri wake tumeupokea lakini hauwezi kutumika sasa kwa sababu CCM hakina mgogoro na Chadema.”

"CCM hakina mgogoro na Chadema, ushauri wake unaweza kutumika endapo CCM itakuwa na mgogoro na Chadema. Tuna uhusiano mzuri kuliko wakati wowote, tuna taasisi ya TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania) ambapo mwenyekiti wa sasa ni Chadema wiki mbili nilienda kuhudhuria kwa niaba ya katibu mkuu, aliyeongoza kikao hicho ni Golugwa (Aman- Naibu Katibu Mkuu Bara) wa Chadema," amesema.

Makalla amesema masuala ya CCM na Chadema yanaongeleka vizuri kupitia vikao vya TCD vinavyofanyika kwa nyakati tofauti, hali inayoashiria kuna uhusiano mzuri baina ya vyama hivyo.

Amshauri Warioba amalize mgogoro Chadema

Katika maelezo yake, Makalla amesema kwa kuwa Jaji Warioba ametoa ushauri nzuri  ni muda mwafaka ukatumike ndani ya Chadema na yeye awe sehemu ya usuluhishi akisema kazi hiyo anaiweza.

"Chadema bado ina makundi tangu kumalizika kwa uchaguzi wao wa ndani ( Januari 21,2025)sasa ni muda sasa Mzee Warioba akaenda pale akakae na G55 pamoja na kina Tundu Lissu ( mwenyekiti) asuluhishe," amesema.

"CCM tutakuwa tayari kuchangia mchango wa mazungumzo kumaliza mgogoro ndani ya Chadema, kwa busara alizonazo Warioba ana uwezo wa kumaliza mara moja mgogoro uliopo ndani ya Chadema," amesema Makalla huku akishangiliwa.


Apokea wanachama wapya

Katika hatua nyingine, Makalla amepokea makada zaidi 20 wanaotoka Chadema, wakiongozwa na Seleman Chanzi aliyewahi kuwania ubunge wa Morogoro Kusini- Mashariki katika uchaguzi mkuu 2015/20.

Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amedai vyama vya upinzani vimekosa sera badala yake vimebakia kupinga kila kitu, wakati CCM imejikita namna ya kutatua changamoto za Watanzania.

"Hatuwezi kuwa na vyama vinavyopinga kila kitu, Serikali iliyopita ilisema ndege zimekufa tuzifufue, tulipinga, lakini baadaye wakazipanda. Chama cha siasa, hakiwezi kupinga kila kitu, baada ya kuona longolongo nikaondoka na kujiunga na jeshi kubwa (CCM)," amesema Msigwa.



Mbunge wa Morogoro Kusini (CCM), Innocent Kalogeris amesema katika kampeni zake za mwaka 2020 aliahidi kupambania ujenzi wa barabara ya Bigwa - Kisaki, yenye thamani ya Sh300 bilioni akisema mkandarasi ameshapatikana na kinachosubiriwa malipo ya awali ili kuanza kazi.

"Mimi na mdogo wangu Taletale (Hamis Taletale - mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, tulipiga kelele bungeni na hatimaye leo mkandarasi amepatikana, kinachosubiriwa ni kuanza kazi, na tumeshaahidiwa na Serikali kwamba fedha za maendeleo zikipatikana basi kazi inaanza mara moja," amesema Kalogeris.

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM), Taletale amedai kuwa jimbo hilo lina mvuto ndio maana viongozi wa Serikali na CCM wanapishana kwa ajili ya kuangalia kukagua, kuhimiza shughuli za maendeleo.

"Hii kazi naipenda kwelikweli, nataka kurudi mheshimiwa mwenezi na hawa (wananchi) bado wananipenda kweli

kweli...," amesema.

"Mimi sio garasa maana ningekuwa garasa hawa wananchi wakiwemo viongozi wa mitaa na kata wasingenifikiria kunichukulia fomu ili niwanie ubunge, nikawaambia hapana nitachukua mwenyewe," amesema Taletale maarufu 'Babu Tale.'