Makalla ziarani Morogoro, asisitiza amani na utulivu

Muktasari:
- Katika ziara hiyo, inayoanza leo hadi Mei 11, atatembelea wilaya za Morogoro Mjini, Malinyi, Gairo, Mvomero, Kilombero, Ulanga na Kilosa ambapo atazungumza na wanachama, viongozi wa CCM pamoja na wananchi kupitia mikutano ya hadhara iliyoandaliwa.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameanza ziara ya siku saba mkoani Morogoro yenye lengo la kuimarisha chama hicho tawala kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Katika ziara hiyo, Makalla ambaye ni mbunge wa zamani wa Mvomero mkoani humo, atatembelea wilaya za Morogoro Mjini, Malinyi, Gairo, Mvomero, Kilombero, Ulanga na Kilosa ambapo atazungumza na wanachama, viongozi wa CCM pamoja na wananchi kupitia mikutano ya hadhara iliyoandaliwa.
Makalla ameanza ziara hiyo leo Jumatatu Mei 5, 2025 ambapo kwa nyakati tofauti akizungumza na wananchi wa stesheni ya reli ya kisasa ya Morogoro, mwenezi huyo amewasisitiza umuhimu wa kuilinda na kutunza amani ya nchi, akiwahakikishia kuwa CCM ipo tayari kwa uchaguzi.

"Nimerudi nyumbani ndugu zangu, nipo katika ziara ya siku saba mkoani hapa, nimeshapita mikoa karibu 24 sasa leo nimeingia Moro huku nilikopita kazi si mmeiona lakini? Akajibiwa na WanaCCM imeonekana.
Miongoni mwa mikoa aliyopita Makalla ni Mbeya, Mwanza, Iringa, Arusha, Manyara, Lindi na Mtwara na Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine alitumia nafasi kujibu hoja za upinzani waliofanya ziara maeneo hayo, sambamba na kuwapokea wanachama wapya.

Makalla amesema ameanza ziara mkoani wa Morogoro kwa lengo la kuimarisha CCM huku akidai kuwa mkoa huo, maarufu mji kasoro bahari ni ngome ya chama hicho tawala.
"Tuendelee kulinda amani yetu kuelekea katika uchaguzi mkuu, wananchi wetu wanahitaji kuona maendeleo na amani pasipo vurugu wala mgawanyiko," amesema Makalla akizungumza na wananchi stesheni na ofisi ya CCM mkoa waliojitokeza kumlaki.
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Morogoro, Joseph Masunga amemkaribisha mwenezi huyo katika mkoa huo, akiahidi kumpa ushirikiano katika siku zote atakazokuwa akifanya ziara katika majimbo mbalimbali.