Maria Sarungi amzungumzia Mange Kimambi utafiti wa Twaweza

Muktasari:
Amesema hivyo baada ya ripoti ya utafiti kuonyesha asilimia 65 ya Watanzania hawako tayari kuandamana kwa lengo la kuishinikiza Serikali kufanya wanachotaka.
Mwananchi.
Sarungi, ambaye ni muasisi wa kampeni ya #ChangeTanzania inayoendeshwa katika mtandao wa Twitter amesema aliwahi kuandika kuhusu Mtanzania huyo anayeishi Marekani ambaye alihamasisha maandamano mwezi Aprili kuipinga Serikali.
Katika ripoti ya utafiti ya Twaweza, suala la wananchi kuandamana linaonekana kuwa bado halijakubalika na wengi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 65 ya wananchi watanzania wanasema hawako tayari kutumia maandamano kuishinikiza Serikali katika mambo yasiyowaridhisha, lakini kuna uwezekano mwananchi mmoja kati ya wanne (asilimia 27) akashiriki maandamano.
Kiwango hicho ni kidogo kiasi kulingananisha na utafiti wa mwaka 2016 ambao ulionyesha waliokuwa tayari kushiriki walikuwa asilimia 29.
Lakini Mange aliangalia zaidi ushiriki wa wanawake baada ya hamasa hiyo.
“Niliandika kuhusu Mange Kimambi, nashukuru pia Twaweza wamelifanyia kazi," amesema Maria Sarungi ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge la Katiba.
"Kitu kinachoonekana ni kwamba ukilinganisha hata mawasilisho haya. Utaona wanawake wamehamasika na walikuwa na utayari wa kuandamana. Mimi nadhani Mange Kimambi kwa kifupi ameweza kuwafikia wanawake wengi kupitia mitandao anayotumia.”
Mange amejipatia umaarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na ujasiri wa kuandika anachokiamini, na hasa kuhusu Serikali.
Harakati zake za kuhamasisha watu kuandamana Aprili 26 hazikufanikiwa hapa nchini, lakini katika nchi kama za Marekani, Uingereza na Sweden kuna vikundi vya Watanzania walioandamana.
Ukiacha suala la Mange, pia Maria alizungumzia suala la uchaguzi hasa kuongezeka kwa kundi la watu ambao hawajaamua watampigia kura nani uchaguzi utakapoitishwa.
“Katika nchi zilizoendelea, wanajua kwamba hicho ndicho kiini cha ushindi. Mara nyingi idadi ya watu ambao hawajaamua kumpigia mtu kura, ilikuwa ndogo kama asilimia 10," ameandika Sarungi.
"Lakini sasa imefikia 30, yaani theluthi moja. Hiyo inamaanisha kwamba hao ndio watakuja kufanya maamuzi mwaka 2020.”