Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka kituo cha majeruhi wa vita hadi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro

Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro

Muktasari:

  • Kilianzishwa mwaka 1945 kama kituo cha kuwahudumia majeruhi wa Vita ya Pili ya Dunia, kituo hiki sasa kimeboreshwa na kuwa hospitali ya kisasa, kikiwa na majengo mapya ya huduma za dharura na wagonjwa mahututi.

Morogoro. Wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ikiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945, Serikali imeeleza hatua mbalimbali za maboresho ya miundombinu na huduma za afya zinazotekelezwa katika hospitali hiyo, hususan katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Maboresho hayo yamechangia kupunguza gharama na usumbufu kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kupata huduma bora na za kibingwa.

Awali, hospitali hiyo ambayo kwa sasa ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ilianzishwa katika kipindi cha ukoloni kama kituo cha kutoa huduma za afya kwa majeruhi wa Vita ya Pili ya Dunia (1939–1945).

Hata hivyo, kwa sasa imekua na kubadilika na kuwa miongoni mwa hospitali bora za rufaa za mikoa hapa nchini.

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 80 ya hospitali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima akizungumza na waandishi wa habari jana amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha hospitali hiyo.

Ameeleza kuwa kwa sasa ujenzi wa majengo ya kisasa ya huduma za dharura, jengo la wagonjwa mahututi (ICU), pamoja na usimikaji wa vifaa vya kisasa vya utoaji huduma umefanyika.

Malima amesema vifaa hivyo ni pamoja na mashine ya CT Scan, Digital X-Ray, mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni, kifaa cha uchunguzi wa sikio, pua na koo (ENT), mashine 10 za kusafisha damu (dialysis), pamoja na uboreshaji wa huduma za daraja la kwanza.

Katika hatua nyingine, Malima amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya afya, hususan kwenye hospitali hiyo. Amefafanua kuwa hospitali hiyo imepokea zaidi ya Sh7.8 bilioni kwa ajili ya kuboresha huduma za afya na miundombinu ya utoaji wa huduma za dharura.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo Malima amesema kuwa tangu Mei 5,2025 hadi sasa, jumla ya wananchi 3,772 wamepatiwa huduma za uchunguzi wa afya, na kati yao, 170 wamefanyiwa upasuaji wa kibingwa bila malipo. Lengo ni kuwafanyia upasuaji jumla ya wagonjwa 242 waliobainika kuhitaji huduma hiyo.

“Tunaona umuhimu wa kuadhimisha mafanikio ya hospitali hii kwa kuwafikia wananchi kupitia uchunguzi wa afya, upasuaji wa kibingwa kwa wanaohitaji, pamoja na matembezi ya hisani na harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha baadhi ya miundombinu ya hospitali hiyo,” amesema Malima.

Ameongeza kuwa: “Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro kushiriki katika maadhimisho haya pamoja na matembezi ya hisani.  Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Miaka 80 ya Ujenzi wa Jamii Yenye Afya.’”

Mmoja wa wananchi waliopata huduma ya matibabu bila malipo, Osward Nyamoga amesema alifika hospitalini kumpeleka mke wake ambaye kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni.

Amesema baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari kupitia huduma za 'Afya Check', mke wake alipatiwa kipimo cha ultrasound bila malipo na hatimaye kugundulika tatizo lililokuwa likimsumbua.

“Kutokana na hali ngumu ya kifedha na gharama kubwa za vipimo, nilikuwa nashindwa kumpeleka mke wangu hospitali. Lakini kupitia kambi hii ya madaktari, tatizo lake limegunduliwa na amepewa dawa anazotumia akiwa nyumbani,” amesema Nyamoga.

Kwa upande wake, Rahma Salumu ambaye pia alipata matibabu kwenye kambi hiyo, ameomba Serikali kuendelea kupeleka madaktari mara kwa mara kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya kwa wananchi, hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kifedha.

“Leo tumepata matibabu kupitia maadhimisho haya ya miaka 80, lakini hatujui maadhimisho mengine kama haya yatafanyika lini  labda baada ya miaka 100.

“Hii si sawa. Naiomba Serikali iwe inafanya maadhimisho ya aina hii kila mwaka ili sisi wanyonge na maskini tusio na uwezo wa kugharamia matibabu tupate huduma za uchunguzi wa afya bure,” amesema Rahma.