Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makandarasi waomba utatuzi changamoto mbili, Waziri Ulega asema…

Muktasari:

  • Asema kutokamilika miradi kwa wakati hakuiongezei hasara Serikali pekee, bali pia wananchi kwa kukosa kunufaika nayo kama ilivyokusudiwa.

Dar es Salaam. Makandarasi nchini Tanzania wametaja changamoto mbili zinazowakabili kwa muda mrefu na kuiomba Serikali ione namna ya kuwasaidia kuzitokomeza.

Changamoto hizo ni ucheleweshwaji wa malipo katika miradi mingi inayosimamiwa na taasisi nyingi za umma.

Nyingine ni utekelezaji wa vifungu mbalimbali vya sheria ya manunuzi ya umma pamoja na kanuni zake hususan katika dhamana za zabuni.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 15, 2025 kwenye mkutano wa mashauriano wa wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam.

 Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Farida Mawenya amesema changamoto hizo ni za muda mrefu akiiomba Serikali kuona namna ya kuzitatua.

Akizungumzia hilo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali itaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha makandarasi wanalipwa kwa wakati, akibainisha ucheleweshaji huo hauwaathiri pekee yao, bali hata Serikali na wananchi. “Miradi kutokamilika kwa wakati kunachelewesha wananchi kuitumi.

"Tulipokutana Dodoma Aprili 30 mwaka huu nilisema Serikali inafahamu changamoto hiyo na athari zake, ina nia thabiti ya kuona mnalipwa kwa wakati," amesema Waziri Ulega akifungua mkutano huo, wenye kaulimbiu isemayo: “Ukuaji wa Makandarasi wa Ndani; Fursa na Changamoto”.

Waziri Ulega pia amesisitiza makandarasi kuwa mabalozi na kufanya kazi kwa weledi huku akiitaka CRB, kuwachukulia hatua makandarasi wazembe wanaosababisha hasara kwa Serikali na wananchi.

Ulega amewapongeza baadhi ya makandarasi wa ndani kwa kufanya kazi kwa uzalendo na kumaliza kwa wakati.

Awali, Mawenya alitoa wito kwa makandarasi nchini kuepukana vitendo vya rushwa na kuwataka kushindana kwa haki ili kukuza sekta ya ukandarasi na uchumi wa nchi.

Amesema mkakati wa Serikali ni kuendelea kutoa kipaumbele kwa makandarasi wazawa, kupitia vifungu wezeshi katika Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kanuni zake za Mwaka 2024 kunaongeza ukuaji kwa makandarasi katika kutekeleza sehemu ya miradi mikubwa ya ujenzi na kuwezesha kushindana katika masoko ya nje ya Tanzania.

Akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Bodi, Msajili wa Bodi ya CRB, Rhoben Nkori amesema katika kipindi cha mwaka 2024 ilisajili jumla ya makandarasi 1,812 na hivyo kufanya idadi ya makandarasi hai waliosajiliwa kufikia 13,596.

"Katika kipindi hicho Bodi imesajili miradi 4,691 yenye thamani ya Sh10.472 trilioni na kukagua miradi 3,581," amesema.

Amesema miradi 2,092 sawa na asilimia 58.4 haikukutwa na kasoro yoyote na miradi 1,489 sawa na asilimia 41.6 ilikutwa na kasoro mbalimbali hivyo kutolewa maelekezo stahiki kwa mujibu wa sheria.