Mapya kesi ya kutekwa Kabendera, Vodacom yaitwa mahakamani

Mwanahabari, Erick Kabendera wakati alipokuwa chumba cha mahakama. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kabendera alitiwa mbaroni na askari polisi nyumbani kwake eneo la Mbweni, Julai 29, 2019, kisha alipandishwa kizimbani kwa kesi ya uhujumu uchumi, lakini sasa ameifugulia kesi ya madai kampuni ya Vodacom akitaka imlipe fidia ya Sh28 bilioni kwa madai ndio iliyofanikishwa kile anachokiita kutekwa kwake.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeitaka kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mkononi, Vodacom kufika mahakamani na kuwasilisha nyaraka inazotarajia kuzitumia kujitetea katika kesi ya madai iliyofunguliwa na mwanahabari, Erick Kabendera dhidi yake.

Katika kesi hiyo, Kabendera anaoimba mahakama iiamuru kampuni hiyo imlipe fidia ya Dola za Marekani 10 milioni (sawa na Sh28 bilioni), akiituhumu kuwa ndiyo iliyofanikisha kukamatwa kwake na polisi, tukio analoliita kutekwa na kisha kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, mwaka 2019.

Kabla ya kufungua kesi hiyo, Kabendera aliyejikita katika uandishi wa habari za uchunguzi, kupitia kwa Wakili Peter Madeleka aliiandikia barua kampuni hiyo akiitaka imlipe fidia ya Dola za Marekani 1 milioni (zaidi ya Sh2.5 bilioni), huku akiipa siku 14 kufanya hivyo, vinginevyo angeifikisha mahakamani.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC, Zuweina Furaha alilithibitishia Mwananchi wakati huo, kuwa wamepokea barua hiyo na walikuwa wanaifanyia kazi.

Hata hivyo, Madeleka amelieleza Mwananchi kuwa mteja wake amechukua uamuzi wa kufungua shauri mahakamani baada ya muda wa siku 14 aliyoipatia kampuni hiyo kumalizika bila kampuni hiyo kufanyia kazi maelekezo hayo.

Wakili amesema shauri hilo limepangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi na litatajwa saa 2:30 asubuhi, Julai 9, 2024.

Kwa mujibu wa hati ya wito kwa wadaawa kufika mahakamani, kampuni hiyo imetakiwa kufika bila kukosa na kuwasilisha nyaraka inazotarajia kuzitumia katika utetezi wake.

Katika kesi hiyo namba 12799/2024, Kabendera anadai kuwa kutokana na matukio ya kutekwa kwake na kufunguliwa mashtaka, amepata madhara ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi; ya kijamii, maumivu ya kiakili na kimaono, hasara ya kutokufurahia maisha, hasara ya maendeleo binafsi, hadhi yake katika jamii na kutokuaminiwa kitaaluma.

Hivyo, anaitaka mahakama iiamuru kampuni hiyo imlipe Dola za Marekani 10 milioni (Sh28 bilioni) kama fidia ya hasara halisi na riba kwa kiwango cha mahakama (asilimia), kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kumaliza malipo yote.

Pia, anataka alipwe fidia ya hasara ya jumla kadiri mahakama itakavyotathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine kadiri mahakama itakavyoona inafaa.


Simulizi ya kutekwa kwake

Kwa mujibu wa hati ya madai katika kesi hiyo, Kabendera ameeleza matukio yaliyojiri katika simu yake kabla ya tukio la kukamatwa kwake, kuwa ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kupata huduma ya mawasiliano.

Pia, ameelezea juhudi alizofanya kujua chanzo cha hali hiyo kwa kufanya mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo, lakini hakupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake ambayo alikuwa ameizima tangu jana yake usiku na kwamba ndipo alipobaini kuwa haikuwa na mtandao.

Hivyo aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.

Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza kuwa namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796) ilikuwa na changamoto za kiufundi ambazo zilimhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu, kilichopo Tegeta.

Kabendera alimtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa akidai ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.

"Hata hivyo, (Kabendera alisita kwenda huko kituo cha huduma kwa wateja) kwa kuwa kulikuwa na matukio kadhaa ya watu kutekwa au kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016," inasomeka sehemu ya hati hiyo ya hiyo na kuongeza:

Inaendelea kueleza kuwa Jumatatu, Julai 29, 2019 saa 4:00 asubuhi, Kabendera alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akilalamika kuwa alikuwa akihitaji kutoa fedha kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.

Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza kuwa asubiri kidogo, ili amuulize meneja wake na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kuwa kesi yake ilikuwa nyeti na kwamba ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua.

Badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mliman City, asubuhi hiyo.

Hata hivyo saa 9:00 alasiri siku hiyohiyo Julai 29, ghafla simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom ambaye alimtaka (Kabendera) amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumwelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia tena baadaye kidogo.

Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom ambayo aliipokea akabaini ilikuwa ni sauti ya mwanamume, ambaye alimtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa inakwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa.

“Kabla ya simu hiyo kukatwa mteja wetu alimsikia huyo aliyempigia simu hiyo akinong'ona kuwa alikuwa nyumbani kwake na kuongeza kuwa sogea karibu na nyumba yake,” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya madai.

Kwa mujibu wa hati hiyo, maelezo hayo yalimstua Kabendera na akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake.

Kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegeshwa mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake, halafu wakashuka watu wanne ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa Polisi, lakini walikataa kutoa utambulisho. Walimpiga pingu na  kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.

Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa wakati wa mahojiano, maofisa wa Polisi walifika katika chumba cha mahojiano wakiwa na karatasi zilizochapishwa kutoka katika kompyuta (printout) za akaunti ya pesa ya simu na za namba simu alizokuwa amezipiga kwa mwaka mzima.

Hivyo walimhoji lengo la kila muamala alioufanya kwa mwaka mzima nyuma yake na pia walimhoji uhusiano wake na watu aliokuwa amewasiliana nao miaka kadhaa.

Kabendera anadai kuwa polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusu ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashfu Rais John Magufuli. Hatimaye alishtakiwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi. Inaeleza zaidi kuwa wakati akiwa mahabusu mama yake, Verdiana Mujwahuzi alifariki dunia na hakuruhusiwa kuhudhuria mazishi yake na hata yeye mwenyewe alikuwa na tatizo la kiafya.

Pia inaeleza kuwa kutokana na hali, hiyo aliamua kukiri makosa na kulipa fidia ya Sh273 milioni, ili atoke mahabusu na kwamba baada ya kuachiliwa marafiki na familia yake walimweleza kuwa walipigiwa simu na polisi wakiwaonya kutokumtembelea mahabusu, vinginevyo wangepata shida.


Kesi ya uhujumu uchumi

Kabendera baada ya kutiwa mbaroni nyumbani kwake Mbweni, Julai 29, 2019, alishikiliwa kwa wiki nzima. Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Agosti 5, 2019 akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Alisomewa mashtaka matatu ya kupanga na kushirikiana na mtandao wa kiuhalifu.

Mashtaka mengine yaliyokuwa yanamkabili Kabendera ni la ukwepaji kodi zaidi ya Sh173 milioni na utakatishaji wa kiasi hicho cha fedha.

Alidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019, alitenda kosa la kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia masilahi.

Katika shtaka la pili la ukwepaji kodi, alidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 19, 2019, alishindwa kulipa kodi kiasi cha Sh173,247,047.02.

Katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha, alidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019, maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, alitakatisha Sh173,247,047.02.

Alidaiwa kutenda kosa hilo, huku akijua fedha hizo ni mazao ya uhalifu wa kukwepa kodi na kushiriki kupanga uhalifu.

Hata hivyo, Kabendera aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kufanya majadiliano na kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ya kukiri makosa yaliyokuwa yanamkabili.

Katika makubaliano hayo alifutiwa shataka moja la uhalifu wa kupanga na kubakiwa na mashaka mawili ya kukwepa kodi na utakatishaji fedha, ambayo aliposomewa aliyakiri na akahukumiwa kulipa faini ya Sh250,000 au kifungo cha miezi mitatu jela, kulipa fidia ya hasara aliyoisababisha ya Sh173.24 milioni.

Kwa kosa la pili (utakatishaji) alihukumiwa kulipa faini ya Sh100 milioni.