Mapalala: Magonjwa ya akili ni chanzo cha ongezeko la ukatili kwa watoto

Mkurugenzi wa REPPSI Tanzania, Edwick Mapalala akizungumza na baadhi ya vijana kuhusu ukatili wa kijinsia.
Muktasari:
- Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la Masuala ya kisaikolojia kwa watoto na vijana la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI), Edwick Mapalala amesema vitendo vingi vya ukatili kwa watoto ikiwamo ubakaji na ulawiti vinatokana na tatizo la afya ya akili.
Iringa. Wakati watanzania wakiungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, jamii imeaswa kutibu tatizo la akili kwa madai kuwa ni chanzo cha ongezeko la vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwamo kipigo, ubakaji, ulawiti na maneno makali yanayoathiri saikolojia yao.
Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la Masuala ya kisaikolojia hasa kwa watoto la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI), Edwick Mapalala amesema bila kutibu tatizo la akili haitakuwa rahisi kupambana na matukio hayo.
Akizungumza na Mwananchi, Mapalala amesema wakati zamani maeneo ya ibada, shuleni na nyumbani ndiyo yalikuwa salama kwa ulinzi wa mtoto lakini siku hizi hali imekuwa mbaya.
Alisema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwafanyia ukatili watoto wao kutokana na msongo wa mawazo unaosababishwa na ugumu wa maisha.
“Ifike hatua kila mmoja aishi maisha yake, ajikubali yeye na kipato chake kwenye familia yake, asiishi kwa kuangalia maisha ya mwingine, bila kuridhika, tunapata msongo wa mawazo na mwisho hasira zinahamia kwa watoto,” amesema na kuongeza;
“Hizi adhabu za kuwakomoa watoto haziwasaidii zinawaumiza sana, tena ukatili wa kisaikolojia ni mbaya zaidi.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga amesema wakati mwingine ubakaji na ulawiti kwa watoto umekuwa ukisababishwa na imani za kishirikina kwa baadhi ya wanajamii kudanganywa na waganga wanaowashauri kufanya hivyo wapate utajiri.
“Sasa kama mganga anakudanganya na wewe unaenda kubaka mtoto ukiamini utakuwa tajiri, huo ni ugonjwa wa akili,” amesema Sanga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendegu amesema kila anaposikia tukio la ukatili dhidi ya watoto anaumia.
“Jambo muhimu hapa ni kila mzazi na mlezi kutekeleza wajibu wake wa kumuhakikishia mtoto ulinzi na usalama, Iringa tutaendelea kuchukua hatua kwa watakaobainika kufanya hivyo lakini nguvu kubwa tunaiweka kwenye kudhibiti,” amesema Dendegu.