Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manabii pasua kichwa, wazua mjadala kila kona-4

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa watu wengi wanakimbilia kwenye makanisa hayo wakisaka huduma zitakazotatua shida zao maishani na pia kuchoshwa na michango.

Dar es Salaam. Sakata la waumini kutozwa mamilioni ya fedha kwenye makanisa ya maombezi limekuwa pasua kichwa, limezua mjadala kote nchini, huku mvutano mpya ukiibuka kuhusu waumini kuyahama makanisa makongwe kwenda huko, miongoni mwa sababu ikitajwa ni waumini kupenda miujiza.

Imeelezwa kuwa watu wengi wanakimbilia kwenye makanisa hayo wakisaka huduma zitakazotatua shida zao maishani na pia kuchoshwa na michango.

Mwananchi limefanya uchunguzi katika baadhi ya makanisa ya maombezi jijini Dar es Salaam na kubaini baadhi ya viongozi wa makanisa hayo wakitajirika kwa huduma za maombezi, huku wakiuza bidhaa kama maji, mafuta na leso kwa waumini wao, vitu vinavyodaiwa kuwa na nguvu za Mungu.


Mjadala

Katika mfululizo wa habari zilizochapishwa kutokana na uchunguzi huo, kumeibuka mijadala maeneo mbalimbali, ikiwemo viongozi wa makanisa kunyoosheana kidole, wengine wakitaka Serikali ichukue hatua.

Katikati ya mjadala huo, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja akizungumza na Mwananchi jana, amesema kinachosababisha watu kukimbilia kwenye makanisa ya maombezi, ni ongezeko la michango na sadaka kwenye makanisa makongwe.

Amesema ifike mahali makanisa hayo makongwe yarudi kwenye msingi wake wa kufundisha injili na kupunguza mlolongo wa michango ili kuwatuliza waumini makanisani.

“Kwenye haya makanisa yetu tumeacha kujikita kwenye injili tumeweka nguvu kubwa kwenye michango ili kutengeneza vitegauchumi. Sasa watu wanaona hakuna wanachopata, ni heri waende huko angalau watapewa matumaini kwa kupewa maji na mafuta.

“Tunapoondoka kwenye ajenda ya neno la Mungu na kujikita kwenye vitegauchumi ni upotofu, ndiyo maana hawa wenye makanisa ya kinabii wanafanikiwa kuwavuta watu,” alisema.

Akizungumzia kinachofanyika kwenye makanisa hayo ya kinabii, Hananja alisema viongozi wake wanatumia udhaifu wa watu ili wajinufaishe.

“Ifike mahali watu wawe na akili, wanadanganywa na wenyewe wanakubali kudanganyika. Hivyo vyote wanavyoambiwa vina upako hawashtuki kwa nini wanauziwa.

“Wenzao wanafanya biashara na kutajirika kupitia hivyo vinavyoelezwa kuwa na upako, yaani wamegeuza madhabahu kuwa magenge na vijiwe vya biashara. Kwa mtindo huu naona ipo haja Serikali iende huko kukusanya kodi, maana kinachofanyika ni biashara,” amesema.

Hananja ameitaka Serikali pia kufungua jicho lake kuhusu makanisa hayo, kwa kuwa yanachangia kuharibu nguvukazi ya Taifa, kwa kile alichoeleza watu wanaacha kufanya kazi na kwenda kusubiri miujiza makanisani.

“Tunakoelekea tutakuwa na watu wengi wenye matatizo ya kisaikolojia na afya ya akili. Unakuta vijana wenye nguvu kabisa wanaacha kufanya kazi wanazunguka kwa manabii kusubiri utajiri. Ila sijui watu wana akili gani, unaambiwa utumie maji, mafuta, chumvi sijui ma ‘apple’ ili upate utajiri na unaamini kwamba hilo linawezekana,” amesema.


Walichokisema CCT

Katibu Mkuu Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) yenye madhehebu 12, Canon Dk Moses Matonya amesema wameweka utaratibu mzuri wa utoaji wa sadaka na kama kuna mtu ana kero anaruhusiwa kuieleza.

“Sadaka zinaeleweka, yaani mtu anamtolea Mungu sadaka ya shukrani, sadaka ya matoleo ya kila ibada Jumapili na sadaka mbalimbali kama za kipaimara au kama kuna changizo maalumu la ujenzi. Hayo yote kila kanisa lina utararibu wake,” amesema.

Amesema wanaoondoka kwenye makanisa hayo na kwenda kwenye makanisa ya maombezi wanafanya kwa  uhuru wao binafsi.

“Haya makanisa yetu ya CCT yana sadaka zinazoeleweka na kila sadaka ina sababu yake na waumini wanaelewa,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu madai ya baadhi ya waumini kuhamia kwenye makanisa ya maombezi kutafuta huduma, licha ya gharama wanazotozwa, amesema ni uhuru wao.

“Mtu kukimbia huko na huko kutafuta majani mabichi ni kitu cha kawaida sana, labda mtu anataka aponywe ugonjwa fulani, ni kitu cha kawaida sana. Pengine anaona hiyo huduma hamfanyi, ataondoka tu. Hayo ni matamanio ya binadamu.

“Kwa Tanzania bahati nzuri tumeruhusu uhuru wa kuabudu ilimradi mtu havunji sheria, kila mtu ana uhuru kwenda huko na huko,” amesema.

Makanisa hayo 12 yanayounda CCT, ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana Tanzania (ACT), Kanisa la Moravian Tanzania, Africa Inland Church Tanzania (AICT), Mennonite Church in Tanzania (MCT), Kanisa la Kibatisti Tanzania (BCT) na Jeshi la Wokovu Tanzania.

Mengine ni, Presbyterian of East Africa (PEA), Bible Church Tanzania, Church of God in Tanzania, Evangelistic Church in Tanzania na Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (KIUMA).


Mzee wa Upako na hoja ya makanisa kuendeshwa kwa sadaka

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Wasafi TV juzi, Mchungaji wa Kanisa la Gospel Revival Center, Anthony Lusekelo, maarufu kama Mzee wa Upako, alisema mambo ya imani ni makubaliano.

Alisema maandiko ya Biblia yameelekeza waumini kwenda kanisani na sadaka, hivyo haipaswi kwenda na mikono mitupu kwa sababu Mungu amewawezesha waumini kuwa matajiri.

“Ukienda kwa mtumishi usiende mikono mitupu. Mungu aliandaa watu kuwa matajiri, ukiwa masikini ni uzembe wako,” alisema Mzee wa Upako, akinukuu maandiko, alipokuwa akijibu swali la kwa nini makanisa yanauza bidhaa kama mafuta na maji kwa waumini.

“Nitawapeleka nchi ya maziwa na asali mtakayolima, mtalima shayiri, zabibu na ngano nchi ya shaba inayofuka chuma, mimi nitawabariki. Wewe kesho unakujaje kanisani bila sadaka,” alihoji.

Akiendelea kujenga hoja ya watu kutoa sadaka, Mzee wa Upako alisema Mungu aliwaambia wafalme, kwamba wataongoza nchi kwa kodi.

“Akawaambia watu wa makanisa, na ninyi mtaendesha makanisa kwa sadaka. Taratibu zinatumikaje, Mungu akaandika sadaka hii itakuwa kwa ajili ya wajane, sadaka hii itakuwa kwa ajili ya makuhani, wachungaji na maaskofu ili wasiende kufanya kazi kule,” alisema.

Alipoulizwa kama mafuta ya upako yanaponya, Mzee wa Upako alisema amewahi kuona watu wakiponywa.

“Nimewahi kuona mimi si mara moja si mara tatu, mafuta ya upako yanasaidia watu kupona mpaka kuwa matajiri. Ila sasa mafuta ya upako yanaanzia unapoishia wewe, lakini lazima uwajibike, upambane,” alisema.


Kingi Master: Kila mtu afanye kazi zake

Nabii na Kiongozi wa Madhabahu ya Makuhani, Master King John Paul, mwenye kanisa lake jijini Dar es Salaam, amesema kuna uhuru wa kuabudu, hivyo watu wasibughudhiwe wanapokwenda kuabudu kwenye makanisa ya maombezi.

Mahojiano yake na Mwananchi yalikuwa hivi:-

Swali: Nini hasa kinafanya watu kufurika wenye makanisa ya maombezi?

Jibu: Watu wanatoka kwenye makanisa yao kuja kwenye makanisa yetu ya maombezi kwa sababu wamekosa suluhisho la matatizo yao.

Biblia inasema; “Wakusanyikapo tai ndipo palipo na mzoga.” Hivyo hao watu wanakuja kwenye makanisa yetu kwa sababu wanapata majibu ya matatizo yao.

Wanaolalamikia haya makanisa yetu wameshindwa kutoa majibu kwa waumini wao.

Swali: Kwa nini mnawatoza ada ya kuonana na mtumishi wa Mungu?

Jibu: Hakuna aliyekuja kukuita uje kanisani, hivyo kama unaona gharama ni kubwa, beba begi lako uondoke.

Kama unaona Sh300,000 ya kukuombea ni kubwa, ondoka kanisani. Watu wanaolalamika ni wapinzani wa kazi ya Mungu.

Swali: Kama ni wagonjwa, kwa nini hamwendi hospitalini kuwaombea mnasubiri waje kanisani?

Jibu: Kila mtu afanye kazi zake, hospitali watafanya kazi yao na sisi tunafanya kazi zetu, hakuna kuingiliana.


Mwamposa

Kiongozi wa Kanisa la Arise and Shine, Mtume Boniface Mwamposa amesema hakuna malipo ya kumuona wala kuombewa.

“Nimesikia kwamba ukitaka kuniona lazima ulipe pesa, hakuna kanuni kama hiyo hata Kibiblia. Nikisema watu walipe ni kweli wanaweza kulipa, lakini haina misingi katika maandiko, kwa sababu huyu ambaye hana kitu atanionaje,” amehoji.

Mwamposa, akizungumza jana katika mahojiano na stesheni ya Ayo TV kuhusu masuala mbalimbali,  alisema kuna maelfu ya watu wanaokuja kumuona, hivyo Mungu amempa uwezo wa kuwahudumia na kwamba utaratibu ni kuandikisha majina.

“Kuna watu nimewaweka, kama mtu jambo lake limekuwa nyeti wanaweza kumpa nafasi anakuja ofisini kuniona moja kwa moja, lakini hakuna malipo hata shilingi moja. Uponyaji ni bure, miujiza ni bure,” amesema.

Kuhusu kuuza mafuta na maji ya upako, alisema bei ya maji yao na mengine yanayouzwa dukani ni Sh1,000.

“Mafuta ya upako ni chupa ndogo ambayo kama ningesema niuze Sh50,000 hakuna ambaye angechukua, lakini nimeweka Sh1,000 ili mpaka mtu wa chini apate,” amesema.

Amesema chanzo ni janga lililotokea mkoani Kilimanjaro ambako alifanya maombezi, ambapo watu 20 walifariki dunia na wengine kujeruhiwa wakati wakigombea kukanyaga mafuta ya upako mwaka 2020.

Amesema baada ya tukio hilo aliongea na kiwanda ambacho hakukitaja jina na kukubaliana kutengeneza chupa za aina moja na kuwataka waumini wake wachangie gharama hizo.


Kanisa Katoliki linasemaje?

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amesema licha ya kuwepo kwa michango mingi katika kanisa hilo, lakini hiyo sio sababu ya waumini wao kwenda kwenye makanisa ya maombezi.

Pisa, ambaye ni Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi, alisema michango iliyopo katika kanisa hilo ipo Kibiblia, zikiwamo zaka na sadaka ambazo alisema hata muumini asipotoa hawezi kufukuzwa kanisani.

“Michango yote iko kwenye Biblia, kwa mfano zaka yaani 1/10 ya mapato yako. Wana wa Israel waliambiwa tangu awali wapeleke, iwe ni shamba, mifugo au mapato,” amesema.

Alisema pia kuna sadaka za uzao wa kwanza tangu wa mwanadamu hadi kwa wanyama na mazao ya shambani kuwa ni sadaka.

Alitaja sadaka ya kawaida akisema ni rasmi na inatakiwa itolewe na waumini.

“Hata hivyo, hizi sadaka hazina kikwazo kwamba usipotoa utazuiliwa kuingia kanisani au utakuta majina mlangoni ya waliolipa na ambao hawakulipa.

“Hivyo sikubaliani na madai kwamba waumini wanaondoka kwa sababu michango imeongezeka,” amesema.

Akifafanua zaidi, Askofu Pisa alisema kuna michango inayojadiliwa na waumini wenyewe kwa ajili ya maendeleo ya kanisa, kama ujenzi wa kanisa au nyumba ya parokia, akisema hata kanisa hilo huwa linapeleka sehemu ya mapato yake makao makuu Vatican kwa ajili ya kusaidia makanisa masikini na waliopatwa na majanga.

Kuhusu huduma ambazo waumini wanakimbilia kwenye makanisa ya maombezi, Askofu Pisa alisema kuna Wakristo wanaopenda miujiza na ahadi za uongo.

“Wapo Wakristo wanaopenda Injili za mafanikio, wanapenda miujiza, lakini Yesu alisema hakuna muujiza mkubwa kama wa Yona kumezwa na samaki siku tatu na yeye kufa na kufufuka siku ya tatu.

“Kanisa Katoliki linafundisha neno la Mungu, lakini wapo watu wakisikia ukipeleka hati ya nyumba utajenga nyumba, ukiombewa utanunua gari. Hivi kweli utafanikiwa bila kufanya kazi?” alihoji.


Kauli ya Serikali

Moja ya maoni ya wadau mbalimbali yaliyotokana na mfululizo za habari hizi, ilikuwa ni hatua gani Serikali inachukua licha ya Katiba kuruhusu uhuru wa kuabudu. Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni hazikufanikiwa jana, ikielezwa alikuwa kwenye kikao cha ndani. Naye Naibu wake, Daniel Sillo hakupatikana alipotafutwa kwa simu.

Mwananchi pia lilimtafuta Msajili wa Jumuiya za Kiraia kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Kihampa tangu juzi bila mafanikio na alipotumiwa ujumbe, alijibu yuko kwenye kikao.

Hata hivyo, alipozungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo Aprili mwaka huu, wakati wa maandalizi ya kukusanya habari hii, Kihampa alisema Serikali ikibaini taasisi hizo kukiuka taratibu, huchukua hatua kulingana na mazingira yaliyopo.

 “Zipo hatua tunazochukua kwa taasisi zote zinazojiendesha kinyume na utaratibu,” alisema bila kufafanua.

Kuhusu taasisi hizo kuwauzia waumini wake maji na bidhaa mbalimbali, alisema wao hawasajili taasisi za biashara.

“Mwaka 2021 aliyekuwa Rais wa Tanzania alitoa maelekezo zile taasisi za dini zenye mrengo wa kutengeneza faida zilipe kodi, hivyo sisi hatufuatilii biashara kwa sababu zipo mamlaka zenye wajibu huo,” alisema.


Kilichosemwa na Brela

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),  Andrew Mkapa amesema uuzaji wa vitu vidogovidogo haupo ngazi ya kitaifa ambayo Brella inashughulika nayo,  badala yake wanaosimamia ni serikali za mitaa.

“Kanisa linaposajiliwa huwasilisha katiba na huainisha mambo watakayofanya na hayo huyapeleka kwa Msajili wa Jumuiya na si Brella na hazisajiliwi kama taasisi binafsi. Sasa anayepaswa kuingilia kati ni yule aliyewasajili kuwahoji kwa nini wanafanya kazi kinyume na katiba yao,’’ amesema.


Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.