Prime
Maji, mafuta yanavyotajirisha manabii, mitume - 3

Muktasari:
- Waumini hutakiwa kununua maji, mafuta au chumvi kabla ya kuingia kwenye ibada au kuonana na viongozi wa makanisa
Dar es Salaam. Madhehebu ya dini mbalimbali yana imani na desturi tofauti kuhusu matumizi ya maji, chumvi, mafuta na vitambaa ambayo hutofautiana kulingana na mafundisho ya kila moja.
Kutokana na imani na tamaduni za madhehebu hayo, vitu hivyo huchukuliwa kwa uzito mkubwa na waumini, kila madhehebu yakiwa na njia yake na ya kipekee ya kuelezea na kutumia vitu hivyo kwa mujibu wa mafundisho yao.
Kwa mfano, maji baada ya kubarikiwa au kuombewa yaaminika kuwa na umuhimu mkubwa katika madhehebu mengi, hasa katika Kikristo.
Wapo wanaoyatumia katika ubatizo na matukio ya kubariki watu au vitu zikiwamo nyumba na mali na kwenye ibada nyingine za utakaso, ikiaminiwa kwamba huondoa uchafu wa kiroho.
Chumvi kwa baadhi ya madhehebu hutumika katika kubariki maji na wengine ni kitu cha utakaso na ulinzi dhidi ya nguvu za giza.
Kwa upande wa mafuta, yapo madhehebu yanayoyatumia kwa upako na tiba za kiroho ikiwamo kuondoa pepo, huku mengine wakiyatumia katika ubatizo.
Vitambaa, mara nyingi vyeupe hutumika ikiwa ni ishara ya imani na baraka, wengine wakivutumia kwa ajili ya uponyaji na ulinzi.
Ni kutokana na imani ya waumini kwa wanayoyapata kupitia maji, chumvi, mafuta na vitambaa hivyo, yapo madhehebu yenye kuwataka kuvipeleka ili vibarikiwe, huku mengine yakibariki vya kwao, mfano maji na kuyatoa pasipo malipo kulingana na mahitaji na matumizi ya muhusika.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa madhehebu wamekuwa wakiwapatia waumini vitu hivyo kwa kuwalipisha fedha, huku wakitoa maelekezo ya namna ya kwenda kuvitumia.
Katika uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, kanisa lililopo jijini Dar es Salaam, waumini kabla ya kuingia kwenye ibada huuziwa maji ya upako, ujazo wa nusu lita kwa Sh1, 000. Katika chupa ya maji hayo, kuna chapa ya jina la kanisa.
“Awali tulikuwa tunauziwa maji ya kawaida baada ya mtume na nabii (anamtaja) kuyaombea, lakini sasa kanisa linazalisha maji tukifika hapa tunanunua,” amesema mmoja wa waumini kwa sharti la kutokutajwa jina.
Muumini mwingine wa kanisa hilo mkazi wa Kijichi, anasema kila anapokwenda kwenye ibada hununua maji ya kumtosha kwa wiki nzima.
“Maji yananisaidia kwenye biashara zangu na hata kama kuna mgonjwa nampa anakunywa anapona. Hata ndugu zangu huwa nawapelekea na kwa kweli yametusaidia,” amesema.
Katika kanisa lililopo Kimara, muumini kabla ya kuonana na kiongozi mkuu anapaswa kwanza kununua mafuta ya kiroho na kuyatumia.
“Lazima kwanza uanze kutumia mafuta, pia nitakuandikia vifaa vya kiroho. Huenda kuna maagano unayo ya mizimu, ambayo yako ndani ya familia, ndiyo sababu una ugomvi na mumeo,” anaeleza mmoja wa watenda kazi katika kanisa hilo, alipozungumza na mwandishi aliyemweleza ana matatizo ya ndoa, anahitaji kuonana na kiongozi wa kanisa, akihoji ni utaratibu gani aufuate.
Orodha ya vifaa hivyo kwa mujibu wa mtendakazi ni mafuta ya maagano, maji ya mfuniko wa zambarau na maji ya mfuniko mweupe, vyote vinauzwa kanisani hapo.
Kuhusu bei, anasema mafuta kulingana na ujazo huanzia Sh15,000 hadi Sh100,000, huku maji yenye ujazo wa lita moja ni Sh2,500.
Kutokana na tatizo la mwandishi aliloelezwa, mtendakazi alimwelekeza anapaswa kumpaka mume wake mafuta hayo na iwapo atashindwa, basi awe anamwekea kwenye mboga kwa siku nane.
“Unapomwekea kwenye mboga yake, uwe unaomba ukisema kila agano la mume wako unaomba liondoke, unaweza kushangaa anabadilika, wanaume wengi wamefunguliwa kwa njia hiyo,” aliagiza mtendakazi huyo.
Pia alimtaka anapokuwa katika hedhi asishike vitu hivyo. Mbali na hilo, baada ya kukutana kimwili na mume wake, asivishike mpaka atakapooga.
“Haya mafuta ya maagano utakuwa unalamba kidogo, kisha unapaka mwili mzima. Mume wako kama nilivyokwambia, utamwekea kwenye mboga yake tu, wakati huo ukimwambia Yesu, naomba mfungue mume wangu,” ameeleza.
“Maji ya kwenye chupa ya zambarau utakuwa unachanganya vifuniko vitano kwenye maji yako ya kuoga ya uvuguvugu,” aliagiza mtendakazi huyo.
Kwa maji yenye mfuniko mweupe, alielekeza yamwagwe kwenye kona zote za nyumba.
Kuhusu vitu hivyo kutumika kwenye biashara, mtendakazi huyo amesema, “Kuna maji ya sumaku, haya ndiyo ya biashara, ambayo unatakiwa kuyapaka unapotoka kwenda kwenye biashara, yanauzwa pia dukani hapo nje, nenda tu kayanunue kama unayahitaji,” anasema.
Kwa mujibu wa mtendakazi huyo, baada ya siku nane za kutumia mafuta na maji, ndipo mwandishi huyo aliyehitaji huduma, arudi kanisani ili kuangalia utaratibu wa kuonana na kiongozi wa kanisa hilo, ambaye mara nyingi hukutana na waumini Ijumaa, Jumanne au Alhamisi kwa jinsi Yesu atakavyomuongoza.
Katika kanisa lililoko Temeke, waumini waingiapo kanisani nao hutakiwa kuwa na maji, mafuta na leso ambavyo huvinunua kutoka kwa wahudumu wa kanisa hilo.
Maji ya ujazo wa nusu lita huuzwa Sh1,000, ya lita moja Sh2,000, leso huuzwa kati ya Sh2,000 na Sh3,000, huku mafuta yakiuzwa Sh10,000, na chumvi gramu 500 kwa Sh5,000.
Kwa wasio na fedha za kununua mafuta, msaidizi wa kiongozi wa kanisa huweka mafuta kiganjani na kuwataka waumini kwenda kuchovya wakilipa kuanzia Sh1, 000.
“Haturuhusiwi kuja na maji kutoka nyumbani, ni lazima tununue hapa,” anasema Dianna Charles, aliyefika kanisani hapo alipozungumza na Mwananchi.
Mbali ya hayo, kanisani hapo huuzwa fulana yenye picha ya kiongozi wa kanisa hilo kwa bei kati ya Sh10, 000 na Sh20,000.
Uchunguzi wa Mwananchi katika kanisa lingine lililopo Kigogo, jijini Dar es Salaam umebaini kuwapo utaratibu maalumu wa kuonana na kiongozi wa kanisa kwa kuwa na vitu kadhaa.
"Ukienda kuonana naye, kuna zana za kiroho ambazo unatakiwa uwe na mojawapo au zote kama ambavyo utabarikiwa," anaeleza msaidizi wa kiongozi huyo.
Anasema zana hizo zinatofautiana bei ya chini ni kuanzia Sh10, 000 na ya juu ni kuanzia Sh40,000.
"Zana hizo ni mafuta, stika, vitabu na nyinginezo, hivyo unapokuja unapaswa kuja na sadaka ya kupata zana mojawapo ya kiroho, hata ukitaka kuchukua zote ni wewe na namna ulivyowasiliana na roho wa Mungu, utaelekezwa namna ya kuitumia na baada ya huduma utaondoka nayo," anasema.
Katika kanisa hilo, mmoja wa waumini ameeleza huduma ya mafuta hutolewa kwa kuwekwa viganjani kulingana na utoaji sadaka wa muumini husika.
“Ikifika wakati wa kutoa sadaka, wale wa kuanzia Sh5 milioni hadi Sh10 milioni huwa wachache kama watano hivi. Wanakuja wa Sh1 milioni hadi Sh500, 000 tunapeleka sadaka madhabahuni, inashuka hadi wa Sh5,000,” anasema.
Wakati wa utoaji sadaka anasema kiongozi wa kanisa hilo huwa na mafuta kwenye vyombo tofauti kulingana na kiasi kilichotolewa, cha juu wakipatiwa huduma kwa chombo mfano wa birika chenye rangi ya dhahabu, ikifuatiwa na isiyong’aa sana na wengine kwenye chombo kinachofanana na kikombe.
Itaendelea kesho ikiangazia maoni ya wadau mbalimbali wakipendekeza nini kifanyike.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.