Mambo yanayomsubiri bosi mpya NHIF

Daktari wa Uchumi, Irene Isaka
Muktasari:
- Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepata bosi mpya ambaye ni Dk Irene Isaka. Wadau wa sekta ya afya wamebainisha maeneo ambayo msomi huyo wa uchumi anapaswa kwenda kuyafanyia kazi.
Dar es Salaam. Daktari wa Uchumi, Irene Isaka mwenye uzoefu wa kuongoza mashirika ya Serikali na binafsi ndani na nje ya nchi, amepewa jukumu la kuongoza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Dk Isaka anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Bernard Konga aliyemaliza muda wake baada ya kuongoza mfumo huo tangu mwaka 2016.
Usiku wa jana Jumatano, Agosti 14, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wakiwemo wa sekta ya afya. Dk Irene akiteuliwa kuwa bosi wa mfumo huo huku Jenista Mhagaka akiteuliwa kuwa Waziri wa Afya.
Mhagama ambaye ameapishwa leo Alhamisi, Agosti 15, 2024 pamoja na viongozi wengine. Amechukua nafasi ya Ummy Mwalimu ambaye amewekwa kando baada ya kuhudumu kwenye wizara hiyo kwa kipindi kirefu cha ingia, toka.
Dk Irene na Waziri Mhagama wanaingia kwenye sekta ya afya kukiwa na matumaini mapya kutoka kwa wadau ambao wanaonyesha maeneo ambayo bosi huyo wa NHIF anapaswa kwenda kuanza nayo.
Mabadiliko haya yanabeba matumaini mapya kwa wananchi kwamba huenda yale ambayo walikuwa wakilalamikia masuala mbalimbali likiwamo la kuondolewa kwa kifurushi cha Toto Afya ambacho kilikuwa mkombozi wa wengi kutokana na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, litakwenda kupatiwa ufumbuzi.
Matumaini haya hayapo kwa wananchi pekee bali hata wadau wa afya wakiwemo madaktari na wamiliki wa vituo vya afya binafsi, ambao waliainisha maeneo ambayo wanatamani kiongozi huyo aanze kuyafanyia kazi.
Wadau wa afya wamesema jambo la kwanza linalomsubiri mtaalamu huyo wa uchumi ni kuondoa changamoto zote zilizolalamikiwa ikiwemo kwenye kitita kipya, kuongeza wigo wa wanufaika wa NHIF, utekelezaji wa bima ya afya kwa wote kutobeba kero zilizotatiza utendaji wa mfuko huo na kutafuta njia ya kuuendesha ili kutoyumba.
Malalamiko makubwa ya watoa huduma ilikuwa ni kupungua kwa ada ya usajili na ushauri wa daktari katika kitita kipya na gharama za huduma zilizowekwa kutoendana na soko.
Katika mabadiliko ya ada ya usajili na ushauri wa daktari, viwango ambavyo vilipunguzwa ni kwa mgonjwa kumuona daktari Hospitali ya Taifa kufikia Sh25,000 kutoka Sh35,000 kwa daktari bingwa mbobezi na Sh20,000 kutoka Sh25,000 kwa daktari bingwa.
Mabadiliko mengine ni kwenye Hospitali ya Rufaa ya kanda na kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh35,000 na kumuona daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh25,000.
MAT: Aanze na kitita kipya
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deusdedit Ndilanha amesema kazi kubwa anayopaswa kuanza nayo ni kitita kipya ambayo tangu kutambulishwa kwake kumekuwa na mvutano baina ya wadau na mfuko huo.
"Baada ya wadau kulalamikia kitita kipya, aliyekuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliunda kamati kushughulikia changamoto hizo, pamoja na kazi ya kamati hiyo wamiliki wa hospitali bado wakiendelea kulia na bei zilizowekwa hazikuendana na watoa huduma na nyingi zinalalamikiwa kutokuwa na uhalisia," amesema.
Dk Ndilanha ametaja jambo lingine linalomsubiri Dk Irene ni kuongeza idadi ya wanufaika wa mfuko kwani kwa miaka 30iliyopita hadi sasa wanufaika wa bima ya afya ni asilimia nane pekee.
Idadi hiyo ameitafsiri ni ndogo hivyo kuondoa mantiki ya bima ya afya, akisema jukumu alilonalo kiongozi huyo sasa ni kuongeza wanufaika wa mfuko huo ambao sasa inaonekana idadi kubwa ya waliojiunga ni wagonjwa.
“Tunachotaka sasa watu wote waingie wale wenye changamoto na wasio nazo, aje na mkakati wa kuongeza wanufaika, tukifikia asilimia 40 hadi 50 hapo tutakuwa tumepunguza hizi kelele.
"Jukumu lingine ni utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, tunakwenda kuanza utekelezaji lazima tuwe makini kwa sababu hatukufanya vizuri sana kwenye NHIF, changamoto tulizokuwa nazo kwenye mfumo huu tusizibebe kwenda nazo kwenye Bima ya Afya kwa Wote tutafeli," ameshauri.
Hoja hizo zinaungwa mkono na Mkurugenzi wa Umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Afya Binafsi Tanzania (Aphfta), Dk Samwel Ogillo ambaye amesema wana imani na Dk Irene kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kuhudumu kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
"Nategemea changamoto zilizokuwa kwa muda mrefu ikiwemo mfuko kushindwa kujiendesha itabidi aangalie chanzo ni nini, ikiwemo changamoto ilivyoonyeshwa kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) vitu vilivyoelezwa kule akazifanyie kazi," amesema.
Taarifa ya CAG anayoitaja Dk Ogillo ni ya mashirika ya umma ya Machi 2022, iliyoonyesha NHIF kupata hasara ya Sh109.71 bilioni.
Kitu kingine, Dk Ogillo amesema kiongozi huyo Mkuu wa NHIF anapaswa kuangalia kwa umakini namna sekta binafsi inavyoendeshwa tofauti na Serikali, kwani haiwezekani bei za utoaji huduma wapangiwe sawa na hospitali za Serikali ambazo zinapokea ruzuku.
Amesema sekta binafsi inajitegemea kwa kila kitu kuanzia ununuzi wa vifaa hadi ulipaji wa mishahara ya watumishi, hivyo hawawezi kuwa sawa na hospitali za umma ambazo zinapata ruzuku na mishahara inalipwa na Serikali.
Kutokana na mgongano uliopo baina yao na NHIF, Dk Ogillo amesema walikuwa wanajipanga kujiondoa NHIF kwani tangu kitita kipya kitangazwe wamekuwa wakipata hasara ya zaidi ya asilimia 50, huku taasisi nyingine zikiingia kwenye madeni makubwa.
"Itabidi aangalie suala hilo na kuleta uwiano mzuri na kitita kuangalia uhalisia wa gharama za afya nchini na sekta ya afya ikue isididimie.”
“Sekta ya afya imeshapiga hatua tusirudi nyuma na tuwatie moyo wananchi wajiunge na bima ya afya kwa kupata huduma bora, na tuna imani naye kutokana na uzoefu alionao atafanya vizuri," amesema.
Naye Rais wa Taasisi ya Kongamano la Afya, (Tanzania Health Summit), Dk Omar Chilo amesema kitu anachopaswa kuona kinafanywa na mkurugenzi mpya wa NHIF ni namna watu wanavyoishindwa kupata huduma kutokana na vitita vilivyopo kwenye mfuko huo.
"Hospitali za Serikali zina ruzuku sekta binafsi hadi kodi wanalipa wakipata ugumu kwenye gharama watashindwa kutoa huduma, sekta hiyo ina viwango vyao vya mishahara na huduma. Rai yangu kiongozi wa sasa aendelee na mazungumzo na sekta binafsi," amesema.
Dk Chillo amesema kwenye bima ya afya NHIF ambayo mtumishi wa Serikali anakatwa michango moja kwa moja hakuna mwanya wa kuongeza fedha kwenye mfuko huo, mtu kama anataka huduma kwenye hospitali binafsi yenye gharama ya juu itampasa akate bima nyingine ya sekta binafsi.
Hekaheka Kitita kipya cha mafao 2023
Februari 2024, Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini Tanzania zilisitisha huduma kwa wanachama wa NHIF baada ya kuanza kwa utekelezaji wa Kitita cha Mafao 2023.
Kutokana na hali hiyo Serikali iliingia kwenye mazungumzo na watoa huduma hao ikiahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazolalamikiwa.
Changamoto zilizolalamikiwa mbali na gharama za kumuona daktari na gharama za dawa kuwa chini NHIF iliziondoa dawa 176 kutokana na kile kilichoelezwa jumla ya dawa 138 hazipo kwenye NEMLIT.
Dawa aina 29 muundo wake haujajumuishwa katika NEMLIT kwa mantiki kuwa zimewekwa dawa mbadala.
Kufuatia hatua hiyo, wadau walipinga kuondolewa kwa dawa hizo na baadaye Serikali kurejesha dawa 178.
Tishio la NHIF kufa
Mwaka 2022 aliyekuwa Mkurugenzi wa NHIF, Konga akizungumza na waandishi wa habari alisema walitumia Sh99.09 bilioni mwaka 2021/22 kulipia magonjwa yasiyoambukiza aliyoyataja ni mzigo kwa mfuko huo.
“Dawa za saratani zinaila zaidi NHIF. Haya ni magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha, kuna huduma ya kusafishwa damu kwa wagonjwa wa figo, tunatumia Sh35.4 bilioni kwa mwaka,” alisema.
Kwa mujibu wa NHIF hadi mwaka 2022 mfuko huo una wanachama 4,831,233 sawa na asilimia nane ya Watanzania wote, huku asilimia sita wakihudumiwa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) huduma nyingine za bima zikihudumia asilimia moja.
Huyu ndiye Dk Irene Isaka
Irene ni daktari wa Uchumi aliyosoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (USDM) kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.
Mwaka 2010 hadi 2018 alihudumu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na mwaka 2021 hadi 2022 akihudumu kama Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).
Mwaka 2019 alihudumu pia kama mkufunzi wa taasisi ya usimamizi wa fedha, mwaka 2020 alikuwa Katibu Mkuu wa Sekta ya Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya mwaka 2022 kushika nafasi kuwa Mkurugenzi wa sekretarieti hiyo.