NHIF yarejesha huduma hospitali za Aga Khan

Muktasari:
- Agosti 12, 2024 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ulitoa taarifa kwa umma kusitisha huduma zake katika Hospitali za Aga Khan, ili kupisha mazungumzo ya kimkataba yaliyokuwa yakiendelea.
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeeleza kurejeshwa kwa huduma kwa wanachama wake katika Hospitali za Aga Khan nchini mpaka pale itakapotangazwa vinginevyo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Agosti 13, 2024 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Grace Temba imeeleza hatua hiyo inatokana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kuendelea na mazungumzo na hospitali hiyo juu ya utoaji wa huduma za afya kwa wanachama wa NHIF.
“Kutokana na hayo, wanachama wa NHIF wanaweza kuendelea kupata huduma katika vituo vya Aga Khan kwa utaratibu uliokuwepo awali au kutumia vituo vingine vilivyosajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchi nzima,” amesema Temba na kuongeza;
“Hivyo, endapo mwanachama atapata changamoto yoyote awasiliane na mfuko kupitia ofisi zake zilizoko nchi nzima, pamoja na kituo cha huduma kwa wateja kinachofanya kazi saa 24 kila siku kupitia namba 199 bila malipo.”
Agosti 11, 2024 NHIF ilitoa taarifa ya kusitisha utoaji huduma za matibabu kwa wanachama wa mfuko huo katika Hospitali za Aga Khan ifikapo Agosti 13, 2024.
NHIF ilikiri kupokea maombi ya Hospitali ya Aga Khan ya kusitisha utoaji wa huduma kwa wanachama wa mfuko, kutokana na sababu za kiundeshaji za hospitali hiyo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Meneja Uhusiano wa NHIF, Grace Michael ilieleza kwa mujibu wa mkataba baina ya mfuko na mtoa huduma, upande wowote una haki ya kuomba kusitisha au kuendelea na utoaji wa huduma, hivyo Agha Khan kama ilivyo kwa vituo vingine anao uhuru wa kutumia haki ya kimkataba.
“Wakati majadiliano na mtoa huduma yakiendelea kuhusu maombi yake ya kusitisha huduma, mfuko unatoa taarifa kwa wadau wake wote kuwa ifikapo Agosti 13 wanachama wanashauriwa kutumia vituo mbadala vilivyosajiliwa na mfuko kupata huduma za matibabu,” ilieleza taarifa hiyo.
Mfuko wa NHIF umesajili vituo zaidi ya 9,000 nchini ambavyo vinamilikiwa na Serikali, taasisi binafsi na mashirika ya dini.
Vituo hivyo ni vya ngazi mbalimbali kuanzia zahanati hadi ngazi ya Hospitali ya Taifa ya Rufaa. Lengo la kusajili vituo hivyo ni kumpa uhuru mwanachama kuchagua kituo cha kupata huduma za matibabu popote alipo ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfuko huo ulikuwa umefanya maandalizi ya kuwezesha mwendelezo wa huduma kwa wanachama waliokuwa wanapata huduma katika Hospitali ya Aga Khan, ikiwemo kusajili vituo mbadala vyenye hadhi sawa au zaidi ya hospitali hiyo.