Malasusa: Viongozi tusikilize na kunyenyekea tunaowaongoza

Askofu Alex Malasusa
Muktasari:
- Malasusa amesema hayo leo Mei 13, 2025 wakati akihubiri katika ibada ya maziko ya kiongozi huyo ambayo inafanyika katika kanisa la KKKT Usharika wa Usangi Kivindu, Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro.
Mwanga. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa, amesema kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa Msuya, alikuwa kiongozi mwenye kipawa cha kusikiliza na unyenyekevu katika uongozi wake, hivyo amewataka viongozi kuiga mfano wake.
Malasusa amesema hayo leo Mei 13, 2025 wakati akihubiri katika ibada ya maziko ya kiongozi huyo ambayo inafanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Usangi Kivindu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Msuya ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro alifariki dunia Mei 7,2025 kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam na atazikwa leo Mei 13, 2025, katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwake.
Akihubiri katika ibada hiyo, Dk Malasusa amesema viongozi wanaowajibu mkubwa wa kuwasikiliza watu na kuwanyenyekea wanaowasimamia katika jamii.
"Ushuhuda wa Mzee Msuya nimesikia wengi wa ngazi yake wakisifu na ngazi za chini wakisifu, huyu mzee alipewa kipawa cha kusikiliza na kunyenyekea, kwani kusema ni shaba na kusikiliza ni dhahabu, tumuombe Mungu atupe tabia ya unyenyekevu ndani ya kanisa, jamii na familia,"amesema Dk Malasusa
"Tukijua kuwa siku zetu ni chache katika dunia hii tutaishi kwa kupenda amani na kujali wengine. Baba huyu aliyelala alitafuta sana amani na watu wote, Watu walimuheshimu na ni mmoja ya viongozi waliokuwa makini, pia alikuwa mtu wa busara na hekima," amesema Dk Malasusa
Amesema marehemu Msuya watu walimheshimu sio kwamba alikuwa na nguvu sana ni kutokana na hekima yake na busara zake na kwamba alitanguliza amani kwa watu wote.
"Tukijua kuwa siku zetu ni chache katika dunia hii tutaishi kwa kupenda amani na kujali wengine. Baba huyu aliyelala alitafuta sana amani na watu wote, Watu walimuheshimu na ni mmoja ya viongozi waliokuwa makini, pia alikuwa mtu wa busara na hekima,"
Aidha amewataka pia viongozi kutambua kuwa Mungu amewapa nafasi walizo nazo ili kuwathamini watu wa chini na kuwa baraka kwa wengine.
"Viongozi tuwakumbuke wale ambao Mungu anawaweka chini yetu ili siku za kuishi ziwe baraka, Mzee Msuya alikuwa kielekezo kizuri kwetu Watanzania,"amesema Dk Malasusa
Katika hatua nyingine Dk Malasusa ameitaka jamii kuishi maisha yenye kuacha alama ambayo itakuwa ushuhuda kwa wengine.
"Maisha haya tunaweza tukaondoka haijalishi umeishi siku ngapi ila umeondokaje na umeacha nini.Tukijua siku zetu tutaushi tukipendana, kutakiana baraka na kutafuta amani na watu wote".
"Tutengeneze ushuhuda wetu tungali na uhai na leo kila mmoja aende kuzungumza na Mungu wake kwenye maombi amjulishe siku zake ili aondoe kiburi na kuishi maisha ya ushuhuda na watu waone baraka"amesema Dk Malasusa