Makumbusho ya Taifa Posta kunufaika na maboresho yatakayofanywa na Serikali ya Oman

Dar es Salaam. Makumbusho ya Taifa ya Posta, inatarajiwa kuwa na muonekano mpya, baada ya Serikali ya Oman kuahidi kufadhili maboresho yatakayokwenda sambamba na ujenzi wa jengo la ghorofa mbili katika eneo hilo.
Ufadhili huo pia, utahusisha maboresho ya picha na michoro iliyopo ndani ya makumbusho hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam ili kuongeza mvuto kwa watu mbalimbali watakaoitembelea.
Hayo yameelezwa juzi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki alipohutubia katika hafla ya majadiliano ya utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kati ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania na ile ya Oman.
Shughuli hiyo, ilihudhuriwa na Balozi wa Omani nchini, Saud bin Hilal Saud Al Shaidhani na Jamal Bin Hassan Al-Moosawi ambaye ni Katibu Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Sultani wa Oman.
Waziri Kairuki, alisema miongoni mwa maboresho yanayotarajiwa ni katika ghorofa ya pili ya jengo lililopo sasa, ili kuweka mikusanyo ya kihistoria.
“Wataiboresha na kuweka taa mpya, usimamizi wa mazingira na wataweka mambo yote, kwa ufupi itakuwa ya kisasa. Mimi nawaambia kama ghorofa moja itakuwa nzuri sana, vipi kuhusu nyingine na nakuombea wakati unamalizia nyaraka naomba uhusishe na ghorofa nyingine,” alisema.
Mbali na maboresho hayo, Waziri Kairuki alisema jengo jipya la ghorofa mbili pia litajengwa katika ushirikiano ili kulinda utamaduni na urithi wa Tanzania.
“Pia litakuwa kwa ajili ya kuhifadhi nyalaka za Kiswahili na kuonyesha historia ya pamoja ya ukoloni ambayo Tanzania na Oman tunayo,” amesema Kairuki.
Pamoja na hayo, Waziri huyo alisema katika majadiliano yao ameomba pia Serikali ya Omani chini ya Sultan kusaidia Makumbusho ya Taifa ya Posta katika mpango kazi wa ujenzi wa makumbusho hiyo.
Kairuki ameiishukuru Serikali ya Oman kwa kazi ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa Juni 13 baina ya mataifa hayo mawili kuhusu uboreshaji wa makumbusho ya Taifa.
“Juni mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea Oman na kushuhudia makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo ya utamaduni ikiwemo ushirikiano kati ya makumbusho hizi mbili za Tanzania na Oman.
“Matarajio yangu makubaliano haya yatayanufaisha mataifa haya mawili ikiwemo Tanzania kupata vifaa vya kisasa katika maonesho na maboresho sehemu ya makumbusho. Pamoja na kuwajengea uwezo watendaji kupitia mafunzo,” amesema Kairuki.
Kwa upande wake, balozi Al Shaidhani ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika, “ni jambo la faraja kuona makubaliano ya ushirikiano yameanza kufanyiwa kazi kwa hatua ya kwanza,” amesema.
“Namshukuru Rais Samia kwa kuhakikisha makubaliano haya ya ushirikiano yamesainiwa, najisikia faraja kusimama hapa leo (jana), kuna kuna hatua imeanza kupigwa katika makubaliano haya, najisikia raha kwa hili,” amesema.
Balozi Al Shaidhani alimuahakikishia Waziri Kairuki kuwa watampa kila aina ya ushirikiano ili kupata matokeo bora kati ya Oman na Tanzania, akisema wana historia, uhusiano mzuri baina mataifa hayo mawili.