Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makinda: Wanawake wahamasishe vijana kushiriki uchaguzi

Muktasari:

  • Makinda amesema asilimia 60 ya Watanzania ni vijana, hivyo ni mtaji katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Dodoma. Spika mstaafu  na kamisaa wa Sensa nchini, Anne Makinda amewataka wanawake wawahamasishe vijana, ambao kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ni asilimia 60 ya Watazania, ili wajiandikishe na wakakapige kura.

Ameyasema hayo jana Machi 23, 2024 katika kongamano la Wanawake na Mama Samia jijini Dodoma, akisema sensa ilifanikiwa kutokana na jitihada za wanawake, hivyo wajitahidi kuwa waaminifu na wafanye kazi hii kwa bidii.

“Sensa ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa tuna idadi kubwa ya vijana ambayo ni sawa na asilimia 60 walikuwa na miaka 15 wakati wa sensa na watakuwa na miaka 18 ifikapo mwaka 2025, hivyo nawaomba muwahamsishe wakajiandikishe kwenye daftari la wapiga kura na wakapige kura, kwani hawa ni mtaji tosha.

“Tutumie takwimu za sensa kutafuta kura na ikiwezekana tuwatafute kwenye maeneo yao mmoja mmoja na kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kupiga kura,” amesema.

Pia amewataka wananchi kuzitumia takwimu za sense kiuchumi kwa kubuni miradi ikiwamo kuuza maji na biashara nyinginezo, badala ya kulalamika maisha magumu.

Kauli hiyo pia imeungwa mkono na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa akisema kuna kila sababu wanawake kujua fursa zipo wapi na namna ya kuzitumia, hivyo watumie takwimu za sensa kuzichangamkia fursa hizo.

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amewataka wanawake kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa kwa vitendo na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema Rais Samia anakamilisha miradi mikubwa tangu alipoingia madarakani kama ule wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) na reli ya kisasa (SGR) ambayo amesema iko mbioni kuanza kufanya kazi.

Amefafanua kuwa (Rais) amefuta kodi kwenye sukari ili iingizwe kutoka nje wananchi waipate kwa bei nafuu.

“Niwatie moyo mpo sehemu sahihi, hivyo mkafanye kazi na kuwainua wanawake wezetu kiuchumi na tuendelee kuungana na kushirikiana tusikubali kutengana," amesema.

NMwenyekiti wa Wanawake na Mama Samia Mkoa wa Ruvuma, Judith Mwenda amesema wanawake wamefundishwa fursa nyingi za kiuchumi.

“Hivyo tuache kuzungumza vibaya tushikamane na kuzichangamkia fursa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Wanawake  na Mama Samia Tanzania umetoa tuzo ya heshima kwa Rais Samia ya “mama shujaa, mlezi na mlinzi wa wanawake.” Na kwa mwasisi wa kundi hilo Rosemary Senyamule.

Akikabidhi tuzo hizo katika kongamano hilo, Marry Mwanjelwa amesema wanampongeza  na kuunga mkono jitihada  zinazofanywa na Rais  za kuleta maendeleo.

Naye Mwenyekiti  wa Wanawake na Mama Samia Mkoa wa Dar es salaam, Sophia Kinega akimkabidhi tuzo Senyamule, amesema lengo ni kumtia moyo kwa kuanzisha umoja huo kwani yeye ndiye mbeba maono.