Makinda: Ruksa kutumia takwimu Sensa ya 2022

Muktasari:
Kamisaa wa Sensa nchini na Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Anne Makinda amesema, ruksa kwa mdau yeyote anayetaka kutumia taarifa ya matokeo ya Sensa ya mwaka 2022.
Arusha. Kamisaa wa Sensa nchini na Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda amesema, kwa sasa ni ruksa kwa mdau yeyote anayetaka kutumia taarifa ya matokeo ya Sensa ya mwaka 2022.
Makinda ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2023 jijini Arusha, mbele ya waandishi wa habari wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwepo Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwenye mafunzo ya uwasilishaji usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2023.
"Tanzania imekuwa bora zaidi katika takwimu za Sensa na haijapata kutokea kwingine katika Bara la Afrika...Sasa wadau mnaweza kuzitumia kwa ustawi wa Taifa letu na maendeleo ya wananchi kwa ujumla," amesema Makinda.
Amesema upatikanaji wa taarifa sahihi na zikatumika kikamilifu inasaidia Serikali na wadau wengine kuwatumikia wananchi.
"Kwa hiyo mjue kwamba sensa hii ni makini na haijawahi kutokea katika Bara la Afrika isipokuwa hapa Tanzania.. na waandishi wa habari mmecheza mchezo mzuri sana katika zoezi hili kwa sababu bila ninyi tusingeweza kufanikisha," amesema Makinda.
Anasema matokeo hayo ya Sensa ya mwaka 2022 baada ya kutangazwa ulitoka mwongozo wa kukutanisha makundi mbalimbali na kuyapa taarifa hizi wakiwemo waandishi wa habari.
"Kwa hiyo katika kutoa matokeo mwaka jana ulitoka mwongozo wa kutakiwa kushirikisha waandishi wa habari na kuwafundisha yaliyotokea kutokana na zoezi la Sensa ili wanapotoa taarifa zao watoe taarifa sahihi," amesema Makinda.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Amina Msengwa amesema zoezi hilo la Sensa ya watu na makazi la mwaka 2022 halikuwa rahisi kuwafikia Watanzania milioni 61 kwa wakati bali mafanikio yalitokana na ushirikiano mzuri na ukaribu na waandishi wa habari kuhabarisha umma.
"Haikuwa rahisi kuwafikia watu mil 61 lakini kwa nguvu ya wana habari tuliweza kuwafikia hivyo wana habari ni kiungo muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kuwafikia mwananchi," amesema mwenyekiti wa bodi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo hayo, amesema jamii imepata elimu ya umuhimu wa Sensa na katika dunia ya sasa na teknolojia taarifa ya Sensa ni muhimu.
"Tumepata elimu ya kutosha kujua Sensa maana yake ni nini... katika dunia ya sasa ya teknolojia na Sayansi bila kuwa na takwimu sahihi hakuna maamuzi sahihi...sensa ni nyenzo kuu ya uwaji ya taarifa"
Waandishi hao wa habari kanda ya kaskazini wameeleza kuwa baada ya mafunzo hayo ya siku mbili watakuwa na uwezo wa kuwasilisha kusambaza na kuhamasisha matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.