Vijana hatarini kuathiriwa na rushwa ya uchaguzi

Muktasari:
Akitoa matokeo ya utafiti huo jana, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Alex Awiti alisema suala la rushwa siyo la Serikali wala marais waliotangulia, bali lipo katika jamii na kwamba ili kukabiliana na hali hiyo lazima ishirikiane na taasisi za dini kuitokomeza.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikifanya kila jitihada kuhakikisha inaziba mianya ya rushwa, utafiti uliofanywa na taasisi ya Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan umeonyesha kuwa asilimia 74 ya vijana wapo katika hatari ya kudhurika kutokana na kuwapo kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi.
Akitoa matokeo ya utafiti huo jana, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Alex Awiti alisema suala la rushwa siyo la Serikali wala marais waliotangulia, bali lipo katika jamii na kwamba ili kukabiliana na hali hiyo lazima ishirikiane na taasisi za dini kuitokomeza.
Dk Awiti alisema mbali na suala la rushwa, asilimia 58 ya vijana wa Kitanzania wanajitambua na wanathamini mambo ya dini na asilimia 50 wana moyo wa kuanzisha biashara zao binafsi licha ya kukosa fursa.
Alisema utafiti huo ulifanyika mwaka 2014 hadi 2015 kwa kuhoji vijana 1,940 wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 35 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda na uliangazia maadili , mitazamo, wasiwasi kwa vijana na matarajio yao.
Dk Awiti alisema habari njema ni kwamba, asilimia 70 ya vijana waliamini kuwa viwango vya ufisadi vitapungua katika siku za hivi karibuni.
“Katika kundi hili la vijana, Rais Magufuli ana washirika wenye nguvu, ingawa vijana walikuwa wanaumizwa na kuwa na wasiwasi kwa sababu ya ukosefu wa ajira, lakini walikuwa tayari kusaidia kuleta ufumbuzi kwa kubuni ajira kupitia kwa wawekezaji,” alisema Dk Awiti.
Alisema asilimia 60 ya vijana hao waliamini kuwa walikuwa na uwezo wa kuleta mageuzi katika uchaguzi huku asilimia 68 wakiamini kuwa kupiga kura ni muhimu.
Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu – Watu wenye Ulemavu), Dk Abdallah Possi alisema: “Rushwa ipo katika taasisi na jamii, hivyo ni lazima tusimame kwa pamoja katika kukemea suala la rushwa ili vijana wetu wasitekwe na wanasiasa kipindi cha uchaguzi,” alisema Dk Possi.
Awali, mkurugenzi wa taasisi ya kuendeleza elimu kwa nchi za Afrika Mashariki kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan (IED-EA ), Profesa Joe Lugalla alisema jamii haina budi kubadili mfumo wa mawazo ya vijana ya kuomba rushwa.
“Utafiti huu hautoi suluhisho au mapendekezo ya sera, bali unachochea majadiliano, mijadala na maswali mapya ili kusaidia kuboresha sera za umma na marekebisho,” alisema Profesa Lugalla.
Hata hivyo, Profesa Lugalla alisema utafiti huo umeonyesha kuwa vijana wa Kitanzania wana matumaini na wanaamini kuwa siku za usoni zitakuwa na ufanisi katika upatikanaji wa ajira, matibabu na elimu bora.
Matokeo ya utafiti
Akizungumzia utafiti huo, Dk Awiti alisema asilimia 58 ya vijana waliamini kwamba haijalishi ni vipi mtu atapata fedha ilimradi tu asishikwe na kufungwa gerezani.Asilimia 45 waliamini kuwa ufisadi una manufaa.
“Katika kipengele cha uadilifu, asilimia 44 ya vijana walikuwa tayari kupokea au kutoa hongo wakati asilimia 34 pekee ndiyo walioamini kuwa ni muhimu kulipa ushuru,” alisema Dk Awiti.
Kuhusu kushiriki katika siasa, utafiti huo ulionyesha kuwa vijana walikuwa na maoni chanya kuhusu siasa na demokrasia. Asilimia 68 ya vijana wa Kitanzania waliamini kuwa ilikuwa muhimu kupiga kura wakati asilimia 60 waliamini kuwa walikuwa na uwezo wa kuleta mageuzi.
Pia, asilimia 74 ya vijana hao walikuwa katika hatari ya kudhurika na hongo za uchaguzi wakati asilimia 39 walisema wangempigia kura mgombea ambaye angewahonga.
Dk Awiti alisema asilimia 75 ya vijana hao walithamini dini kwanza huku asilimia 61 wakithamini kazi kwanza, wakati asilimia 46 walithamini familia kwanza. Asilimia 41 walithamini utajiri kwanza na asilimia 22 walithamini uhuru kwanza.
Kuhusu elimu, alisema asilimia 56 ya vijana hao walikuwa na elimu ya sekondari wakati asilimia 44 walikuwa na elimu ya msingi huku asilimia 12 pekee ndiyo waliokuwa na elimu ya chuo.
Akizungumzia kuhusu elimu nchini, Dk Awiti alisema idadi ya wanaume katika vyuo vikuu ni mara mbili zaidi ya ile ya wanawake licha ya Tanzania kufanya vizuri katika utoaji wa elimu kwa usawa wa kijinsia.