Makamba, Mudavadi watia mguu sakata la Kenya Airways na ATCL

Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi (Kulia).
Muktasari:
- Mawaziri hao kupitia kurasa zao za mtandao wa kijamii wa X, wameeleza kuwa baada ya sakata hilo wamekuwa na mazungumzo ambayo yamezaa azimio la kumaliza tofauti hizo ndani ya siku tatu na kurejesha safari za anga.
Dar es Salaam. Mawaziri wa mambo ya nje wa Tanzania na Kenya, wameingilia kati suala la mamlaka za usafiri wa anga katika nchi hizo, kuyanyima vibali vya kutoa huduma mashirika ya ndege ya ATCL na KQ.
Mapema leo Mamlaka ya usafiri wa anga nchini (TCAA) kupitia taarifa ya Mkurugenzi Mkuu, ilitangaza kusitisha kibali cha shirika la ndege la Kenya (KQ) kufanya safari kati ya Jiji la Dar es Salaam na Nairobi kuanzia Januari 22, 2024.
TCAA imesema hatua hiyo inajibu hatua iliyochukuliwa na mamlaka za usimamizi wa anga la Kenya, kukataa maombi ya safari zote za ndege za mizigo zilizoombwa na Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) lililotaka kufanya safari kati ya Nairobi na mataifa mengine.
Baada ya sakata hiyo hali ya wasiwasi iliibuka miongoni mwa wasafiri wa miji hiyo mikubwa Afrika Mashariki, hali iliyolazima Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba na mwenzake Musalia Mudavadi kuingilia kati.
Wawili hao kupitia kurasa zao za mtandao wa kijamii wa X, wameeleza kuwa baada ya sakata hilo wamekuwa na mazungumzo ambayo yamezaa azimio la kumaliza tofauti hizo ndani ya siku tatu.
Wawili hao wamesema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi, kwani wameelekeza mamlaka za usafiri wa anga katika mataifa yao kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha wanamaliza jambo hilo.
Taarifa ya KQ iliyotolewa muda mchache baada ya taarifa ya TCAA, inaeleza kuwa wanatambua kuhusu zuio hilo lakini wanafanya kazi kuhakikisha safari zao baina ya majiji hayo makubwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haziathiriki.
"KQ inawasiliana na mamlaka za usafiri wa anga, taasisi za Serikali za Kenya na Tanzania zinazohusika ili kupata suluhisho linalotoa uhakika wa kutokatishwa kwa safari kati ya Nairobi na Dar es Salaam," imeeleza taarifa kwa umma ya KQ iliyotolewa na kitengo chake cha mawasiliano.