Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ATCL yaja na mikakati mipya ya safari za nje

Muktasari:

Wakati sekta ya anga ikianza kuimarika baada ya janga la Uviko-19, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linapanga kuongeza safari za nje.


Dar es Salaam. Wakati sekta ya anga ikianza kuimarika baada ya janga la Uviko-19, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linapanga kuongeza safari za nje.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa muhimu katika kuifanya ATCL kujiweka katika nafasi ya kujiendesha kwa faida.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema wako mbioni kuzindua safari za moja kwa moja kwenda jijini London nchini Uingereza kuanzia mwakani, ukiacha safari mbili za nje ya Afrika ambazo ni India na China, ndege zake za Boeing 787-8 Dreamliners zinakotua mara tatu kwa wiki.

Matindi alisema kwa safari za India pekee, ndege hupakia abiria 190 huku kwenda China wakipata abiria 120.

Kuanzia mwishoni mwa mwaka huu, alisema shirika linatarajia kuongeza safari moja kwenda India kutokana na matumaini yanayoonekana katika njia hiyo.

Lakini mambo ni tofauti kwa safari za China, ambapo Matindi alisema ruhusa iliyopatikana ni kufanya safari kwa asilimia 75 ya uwezo wa shirika hilo.

Safari hiyo ya London inakuja ikiwa ni miaka miwili tangu ilipositishwa kwa vigezo vya kisheria, Uviko-19 na kuchelewa kwa vifaa muhimu vinavyokusudiwa katika safari ya masafa marefu.

Mwaka 2019, ATCL ilipata fursa ya kuanzisha safari za kwenda London na ilitarajiwa zifanyike mara tatu kwa wiki kutokea Dar es Salaam kupitia Kilimanjaro.

“Kutokana na changamoto zilizojitokeza Gatwick (London) mwaka 2020, tumeanza upya mchakato wa kufanya mazungumzo ili tuafikiane na mamlaka za Uingereza, mazungumzo yanaendelea vyema,” alisema Matindi.

Kwa sasa, abiria wanaokwenda London wanalazimika kupitia Kenya, Rwanda, Ethiopia, Dubai, Doha, Istanbul au Amsterdam kuunganisha ndege.

Mtaalamu wa usafiri wa anga, Juma Fimbo aliishauri ATCL kushirikiana na mashirika mengine kama British Airways, India na China ambako tayari inafanya safari.

Ushirikiano huo alisema utawafanya watalii kutoka mataifa husika kuwa na imani na Tanzania hatimaye kuvutiwa kuwekeza au kufanya biashara.

“Nina matumaini ushirikiano utavutia watalii uwekezaji kwa kiasi kikubwa kutoka Ulaya kuja Tanzania,” alisema.

Mtaalamu mwingine, Gaudence Temu alisema ili safari hizo ziwe na tija ni muhimu shirika hilo litoe huduma bora.

“Kuzingatia ratiba ni muhimu sana kwa usafiri wa anga. ATCL pia inapaswa kufanya kazi vizuri na wadau wa sekta nyingine zinazofungamana na usafiri wa anga, wakiwamo waongoza watalii na mawakala wa mizigo ili kuitangaza Tanzania,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura alisema ATCL inapaswa kuwa na eneo kubwa la mizigo katika safari zao.

“Nafasi za mizigo ni muhimu ili kulikamata vema soko, hivi sasa wafanyabiashara wengi wanafuata mzigo Uingereza,” alisema.

ATCL pia linapanga kuanza safari kwenda Ghana, Nigeria na DRC ili kukuza uchumi.