Majaliwa azungumzia changamoto ya barabara Ruangwa

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiangalia kina mama (wa Kabila la Wamwera) wakiwa wamelala chini kama ishara ya heshima ya mapokezi kwake.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa (CCM), amesema changamoto kubwa katika jimbo lake ni barabara zenye viwango vinavyokubalika, hata hivyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa barabara zimeanza kujengwa.
Majaliwa amebainisha hayo leo Septemba 18, 2023 wakati wa ziara ya Rais Samia katika Jimbo la Ruangwa ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya siku nne katika mkoa wa Lindi akitokea mkoa wa Mtwara.
Amesema barabara hizo zina umuhimu kwa wananchi wa Raungwa hasa katika kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni. Amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo.
“Moja ya tatizo kubwa tulilonalo ni viwango vya njia zetu kwa viwango vinavyokubalika kuweza kusafirisha mazao yetu kutoka Ruangwa na njaa kubwa ilikuwa ni kutoka Ruangwa kwenda kuunganisha na Nganga, kutoka Ruangwa kuunganisha na wilaya jirani ya Nachingwea.
“Leo hii tunapozungumza Mheshimiwa Rais, barabara inajengwa, mkandarasi yuko kazini na wameanza awamu ya kwanza ambayo imefikia asilimia 70, na Waziri Bashungwa ameniambia mkandarasi huyo huyo ndiye atakayejenga kutoka Ruangwa kwenda Nachingwea,” amesema.
Majaliwa amemshukuru kwa kutoa fedha Sh51 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizo nyingine. Amesema kuhusu barabara za ndani pia Rais Samia ametoa Sh11 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo.
Kuhusu kero ya maji, Majaliwa amesema walikuwa na shida kubwa ya maji Ruangwa lakini Waziri wa Maji, Juma Aweso alituma timu yake iliyokwenda kubaini vyanzo vya maji na kuangalia mahitaji, sasa wanapata maji katika vijiji mbalimbali
Upande wa kilimo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema bei ya mazao kama korosho, ufuta na mbaazi zimepanda na hasa mbaazi ambazo walikuwa wanazila zikiwa mbichi na kuozea shambani, sasa zao hilo limegeuka kuwa la biashara
“Kwa mara ya kwanza tumeuza kilo Sh2,200. Msisitizao wako wa kutafuta masoko umekuwa mkubwa. Mwakani sisi wakulima tutalima mbaazi nyingi, tuombe soko liendelee kubaki hapo hapo,” amesema Majaliwa huku akishangiliwa na wananchi.
Kwenye sekta ya madini, Majaliwa amesema baada ya vipimo wamegundua kwamba Ruangwa kuna madini mengi na sasa wachimbaji wameanza kuchimba madini ya graphite (kinywe).
“Sasa tumepata kampuni nne za uwekezaji kwenye sekta ya madini hapa Ruangwa…Kazi itakapoanza wilaya hii itapaa kwa viwango vya juu,” amesisitiza Majaliwa.