Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa ataja mbinu kukuza Kiswahili duniani

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha inakuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani, ikiwamo kuagiza balozi zote za Tanzania kuweka vituo vya lugha hiyo.

Mbeya. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha inakuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani, ikiwamo kuagiza balozi zote za Tanzania kuweka vituo vya lugha hiyo.

Amesema hayo leo Machi 18, 2024 jijini hapa akifungua kongamano la nne la Idhaa za Kiswahili Duniani.

Majaliwa amesema Serikali inaandaa mkakati wa kitaifa katika kuifanya lugha hiyo kuwa fursa kiuchumi.

Amesema hadi sasa Watanzania waishio nje ya nchi,  tayari wamepata elimu ikiwa ni kuongeza wigo wa ajira.

Amewataka wananchi kujipanga vizuri ili kutopoteza fursa hiyo kwa wenye uhitaji.

"Zipo balozi ambazo  zimefungua vituo vya lugha ya Kiswahili kama vile Korea, Colombia, Italia, Zimbabwe na Ufaransa. Nilifurahi nilipofika shule moja ya Korea kuongea na Wakorea ambao waliongea Kiswahili na wengine wamejipa majina yakiwamo Zuhura, Tausi, Joseph na Adam," amesema na kuongeza:

"Kwa maana hiyo, lazima tujipange vizuri vinginevyo ajira zitatutoka na kwenda kwa wenye mapenzi ya lugha hii. Serikali inaandaa mkakati wa kitaifa kufanya lugha hii kuwa fursa kiuchumi," amesema Majaliwa.

Amesema kwa sasa lugha hiyo imepiga hatua kubwa, awali ilikuwa ikiunganisha mataifa ya Afrika Mashariki, lakini sasa imeanza kufika hadi ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambako kuna watu wanaozungumza Kiswahili.

Amesema katika kuenzi kazi ya viongozi wa awamu ya kwanza walioshawishi lugha hiyo, lazima Kiswahili kitumike bila kuchanganywa katika matukio yoyote ikiwamo bungeni.

"Katika kukuza lugha hii eneo la wanahabari linahitaji kuboreshwa na ni muhimu sasa kutoa mwongozo ili kuondoa zile lugha binafsi. Wizara itafute mkakati wa kutoa mafunzo kwa vijana kuondokana na upotoshaji wa  lugha kwa kuzingatia matumizi ya sarufi," ameagiza.

Ametoa maelekezo kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, na ile ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar kutafsiri lugha inayokuwapo kwenye vifaa vya dawa.


Pia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  kuandaa na kuimarisha mafunzo kwa kuandaa wataalamu wa kutafsiri lugha ili kutoa wigo kwa Watanzania kupata ajira.

"Bakita na Bakiza tekelezeni mpango wa mafunzo kwa wahariri, wandishi wa vitabu, nyaraka zote za Serikali ziwe katika lugha ya Kiswahili sawa na matukio yote, na kama kutakuwapo mtu kutoka nje haelewi Kiswahili asaidiwe kwa vifaa maalumu au mkalimani," amesema.

Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid amesema wizara yake kwa kushirikiana na Dk Damas Ndumbaro (Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo) watahakikisha wanaitangaza lugha hiyo na kuziletea kipato nchi, pia kidumishe tamaduni.

"Dk Ndumbaro tutashirikiana kutekeleza maelekezo ya viongozi kuhakikisha tunaitangaza lugha hii kwa manufaa, ikiwamo pato la nchi zetu," amesema Tabia.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Consolata Mushi amesema lengo la kongamano hilo ni kuangalia matumizi ya lugha, maudhui katika uandishi na utangazaji.

"Katika hitimisho la kongamano hili tutapokea mawazo, ushauri na mapendekezo ya washiriki na kisha Baraza litayafanyia kazi, ikiwamo makosa yanayofanywa na vyombo vya habari," amesema.