Majaliwa asisitiza amani, agusia 4R za Rais Samia

Mwanza. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kulinda na kudumisha amani nchini ili kuhamasisha maendeleo na kuziba mianya ya kuibuka kwa migogoro miongoni mwa wanajamii.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 29, 2025 wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufunga kongamano la Amani Afrika Mashariki lililoandaliwa na The Islamic Foundation, katika viwanja vya Shule ya Msingi Mirongo jijini Mwanza
“Nataka niwaambie bila amani hatuwezi kupata mafanikio yoyote, kupitia kongamano hili mmepata nafasi ya kujadili kuhusu tunu hii ya amani, ambayo wakati wote tumeshuhudia viongozi wa dini mkiwa kwenye majukwaa yenu mkihimiza amani miongoni mwa wanajamii, tuishike tunu hii,” amesema.
Pia Majaliwa amesema falsafa ya 4R ya Resilience (Ustahimilivu), Reconciliation (Maridhiano), Reforms (Mageuzi), Rebulding (Kujenga upya) iliyoasisiwa na Rais Samia imejikita katika misingi imara ya kulinda amani. “Falsafa hii imeifanya Tanzania kuwa tulivu na salama.”

Naye Mwenyekiti wa Islamic Foundation, Aref Nahdi amesema taasisi zao zitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuijenga Tanzania yenye haki, amani, usawa, maendeleo na heshima kwa wote.
Aidha, amesema kuwa taasisi hizo zitaendelea kukemea vikali kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa amani, upendo na kuvunja heshima za viongozi wa kitaifa. “Kwa kufanya hivyo inakuwa ni sehemu ya mafundisho ya dini,”amesema.