Majadiliano kumaliza kesi kati ya Serikali na bosi wa Jatu yaendelea

Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya anayekabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, amemwandikia barua DPP ya kuomba kukiri mashtaka.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili likiwamo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, bado anaendelea na vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi baina yake na Serikali.
Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo ‘atazipanda’ kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua ni uongo.
Wakili wa Serikali, Eva Kassa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Juni 3, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kujatwa na kuendelea na vikao vya majadiliano.
Kassa amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini kuwa bado Serikali inaendelea na vikao vya majadiliano dhidi ya mshtakiwa huyo, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua waliyofikia katika majadiliano hayo.
"Tunaendelea na vikao vya Plea Bargaining (majadiliano ya kuimaliza kesi baina ya mshtakiwa na DPP) na bado hatujafikia hitimisho, hivyo tunaomba kesi hii ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na pia kwa ajili ya kuendelea na vikao vya majadiliano," alidai wakili Kassa.
Hakimu Mhini amekubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 18, 2024 kwa ajili ya kutajwa na kuangalina hatua waliyofikia katika majadiliano hayo.
Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video huku mshtakiwa akiwa rumande.
Machi 12, 2024, Gusaya, alimuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ya kukiri na kuomba apunguziwe adhabu dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
Kutokana na barua hiyo, Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa Gusaya kuanza majadiliano na DPP kwa lengo la kuimaliza kesi yake.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.
Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari mosi 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo alilojua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo katika Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.