Mahakama yawaita kwa dharura wadaawa kesi ya waumini Kanisa la Gwajima

Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Dar es Salaam wakiwa wamekaa nje ya kanisa hilo baada ya kanisa lao kufutwa Juni 3, 2025.
Muktasari:
- Baadhi ya Waumini wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima wamefungua shauri la maombi ya Kikatiba dhidi ya Serikali na wakipinga kuzuiwa kufanya ibada.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imewatia wadaawa katika shauri la maombi ya Kikatiba, lililofunguliwa na baadhi ya waumini wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, kufika mahakamani kesho Ijumaa, Julai 11, 2025.
Shauri hilo la maombi mchanganyiko limefunguliwa na Dinali Mbaga na wenzake 51 dhidi ya Mwanasheria Mkuu w Serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).
Katika shauri hilo, waombaji hao ambao Kanisa lao lililoko Ubungo Dar es Salaam, wanapinga kitendo cha akari wa Jeshi la Polisi kuwazuia kukusanyika kwa ajili ya kufanya ibada na kuwatia mbaroni.
Hivyo, wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa: Mosi, wana haki ya uhuru wa kuabudu kama ilivyowekwa wazi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyowekwa wazi katika Ibara ya 19(1) na (3).
Mbili, wana haki ya uhuru wa binafsi kama ilivyowekwa chini ya Ibara ya 15(1) na (2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Tatu, kitendo cha Polisi walichokifanya chini ya maelekezo na amri za mjibu wa pili (IGP) kuwakamata eneo la Ubungo Maji, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam Jumapili ya Juni 29, 2025 walipokuwa wamekusanyika kwa amani na utulivu kwa ajili ya ibada, hakukuwa na sababu ya kisheria na kinakiuka uhuru wa kuabudu.
Nne, kwamba, askari polisi kwa maelekezo ya IGP kuzuia shughuli zao za ibada, kuwakama na kuwaweka rumande katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam ni ukiukaji wa haki zao za uhuru wa kuabudu na hivyo ni kinyume cha Katiba.
Tano, kwamba, Polisi wakifanya chini ya maelekezo na amri za mjibu wa pili hawana mamlaka ya Kikatiba chini ya Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba kuzuia kwa nguvu shughuli za kidini za waombaji waliokusanyika kihalali kwa sala za kidini Juni 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya kuitwa kwa shauri hilo iliyotolewa kwa wadaawa, shauri hilo limepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Cyprian Mkeha, Ephery Kisanya na Zahra Maruma, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
"Fahamu kuwa shauri tajwa hapo juu limepangwa ajili ya kutolewa amri Julai 11, 2025, saa 14:30 (saa 8:30 mchana)," inasomeka taarifa hiyo ya Mahakama kwa waombaji hao, ambayo Mwananchi limeziona.
Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura wakiomba usikilizwaji wale ufanyike kwa haraka.
Katika hati hiyo ya dharura, wakili wao, Peter Kibatala ameeleza kuwa usikilizwaji wa shauri hilo ni wa dharura kwa kuwa kwanza linagusa haki nyeti ya uhuru wa kuabudu.
Pia, Wakili Kibatala anaeleza kuwa haki ya uhuru wa kuabudu ambayo waombaji wadai kuwa imekiukwa Kwa matendo ya mjibu maombi wa pili (IGP) itaendelea kuwa hatarini mpaka shauri hilo litakapoamuliwa.
Msingi wa madai
Waombaji hao wanadai kuwa Ibara ya 19(1) na (2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatoa Haki za Uhuru wa Kuabudu kwa Wananchi.
Hata hivyo, wanadai kuwa askari Polisi ambao wamekuwa wakitekeleza maelekezo na amri za IGP, bila amri yoyote ya Mahakama, sababu za kisheria au sababu za kweli zinazoweza kuelezeka, wamekuwa wakiingilia kwa nguvu shughuli zao za kidini.
Wanadai kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikijirudia kila Jumapili kwa mwezi mzima wa Juni.