Mahakama yakataa madai ya Sh2.4 milioni ya wakili kwa mteja
Picha na Mtandao.
Muktasari:
- Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mwanza, imetupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Wakili Reagan Charles dhidi ya mteja wake, Kamugisha Byabato, kufuatia kushindwa kuelewana kuhusu kiwango cha ada ya huduma za kisheria.
Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mwanza, imekataa ombi la Wakili Reagan Charles lililolenga kutekeleza makubaliano ya malipo ya mdomo dhidi ya mteja wake, Kamugisha Byabato, kufuatia mvutano baina yao kuhusu kiwango cha ada za huduma za kisheria zilizotolewa.
Katika maombi hayo ya marejeo namba 66878/2025, wakili huyo na mteja wake walitofautiana kuhusu makubaliano yaliyofikiwa wakati wa utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa mwombaji, amedai walikubaliana kuwa mteja atamlipa Sh2.4 milioni, huku mjibu maombi akidai kuwa kiwango walichokubaliana ni Sh1.5 milioni.
Kutokuelewana huko kulimfanya wakili huyo kufungua shauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, akiomba utekelezaji wa makubaliano ya mdomo. Mbali na maombi mengine, aliitaka mahakama iamuru mteja wake kulipa kiasi alichodai kuwa walikubaliana.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza pande zote, Mahakama ya Hakimu Mkazi iliona kuwa ombi hilo halikuwa na msingi, ikishikilia kuwa mwombaji alishindwa kuthibitisha kuwepo kwa makubaliano mahususi ya kiwango cha malipo kama alivyodai.
Hukumu ya kutupilia mbali maombi hayo ilitolewa Mei 4, 2026 na Jaji Stanley Kamana wa Mahakama Kuu, aliyesikiliza marejeo hayo baada ya wakili huyo kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama ya chini.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Kamana amesema kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi, hakuna ubishi kwamba Wakili Reagan alitoa huduma za kisheria kwa Kamugisha kufuatia makubaliano ya mdomo kati yao. Hata hivyo, alisema chanzo cha mgogoro kilikuwa ni tofauti ya uelewa kuhusu kiasi cha malipo kilichokubaliwa.
Katika usikilizwaji wa marejeo hayo, Mahakama iliwataka wahusika kujikita katika hoja ya msingi, ambayo ni iwapo makubaliano ya mdomo kuhusu ada za wakili yanaweza kutekelezwa kisheria chini ya sheria za Tanzania.
Katika uchambuzi wake, Jaji Kamana alinukuu masharti ya Amri ya Malipo ya Mawakili ya mwaka 2015 pamoja na kifungu cha 63 cha Sheria ya Mawakili, Sura ya 341 (marejeo ya mwaka 2023), ambacho kinaeleza kuwa makubaliano ya ada kati ya wakili na mteja yanapaswa kuwa ya maandishi.
Ameeleza kuwa madhumuni ya sheria hiyo ni kuhakikisha uwazi, uhakika na ulinzi kwa pande zote mbili, ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza pale ambapo hakuna kumbukumbu rasmi ya makubaliano yaliyofikiwa.
Aidha, Mahakama ilirejea uamuzi wa awali katika kesi ya mwaka 1964 ya “Re Taxation of Costs, Re An Advocate,” ambapo ilishikiliwa kuwa makubaliano ya ada yaliyofanywa kwa mdomo hayana nguvu ya kisheria na hayawezi kutekelezwa.
Kwa kuzingatia misingi hiyo, Mahakama Kuu ilikubaliana na hitimisho la Mahakama ya Hakimu Mkazi, lakini ikaenda hatua zaidi kwa kubainisha kuwa hata kama makubaliano ya mdomo yangethibitishwa, bado yasingeweza kutekelezwa kisheria kwa kuwa hayakuwa ya maandishi.
“Makubaliano ya malipo ya mdomo hayatekelezeki chini ya masharti ya kisheria yaliyopo,” amesisitiza Jaji Kamana katika uamuzi wake.
Kutokana na hoja hiyo, Mahakama Kuu ilitupilia mbali marejeo yaliyowasilishwa na wakili huyo bila kuamuru upande wowote kulipa gharama za kesi.
Ombi hilo liliwasilishwa chini ya masharti ya Amri ya Malipo ya Mawakili ya mwaka 2015, hususan chini ya Agizo la 5(1), (2) na 3(a), yanayotoa mwongozo kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya ada kati ya wakili na mteja.