Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sita kortini wakidaiwa kutumia Nida za wenzao kutakatisha Sh355 milioni

Washtakiwa wanaokabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kutumia laini za simu zilizosajili kwa majina ya watu wengine, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka yao. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Nyamitah na wenzake watano wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Mei mosi, 2025 na Aprili 2026 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na waliongoza genge la uhalifu na kutakatisha Sh355 milioni kwa udanganyifu.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Madale, Gilbert Nyamitah (33), na wenzake watano wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 28, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa jina la mtu mwingine.

Pia wanadaiwa kutumia vitambulisho vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) vya watu mbalimbali kusajilia laini za simu za watu tofauti kinyume cha sheria, pamoja na kutakatisha Sh355 milioni.

Mbali na Nyamitah, washtakiwa wengine ni Fabian Kulwa (40), mkazi wa Mbezi Makabe, Mnyamisi Selumamala (34), mkazi wa Musoma mkoani Mara, Salum Kapene (31), mkazi wa Nyamanoro mkoani Mwanza, Onesmo Aron (34), mkazi wa Runzewe mkoani Geita na Joram Fanuel (23), mkazi wa Tarime mkoani Mara.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Mei 5, 2026, na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 9426 ya mwaka 2026 na Wakili wa Serikali, Michael Shindai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Kati ya mashtaka 28 yanayowakabili, mashtaka 16 ni ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, mashtaka 10 ni ya kutumia kitambulisho cha Nida cha mtu mwingine kusajilia laini za simu, shtaka moja ni la kuongoza genge la uhalifu na kisha kutakatisha Sh355 milioni.

Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Nyaki alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wawili (Gilbert na Kulwa) halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea kubaki rumande.

Baada ya maelekezo hayo, Hakimu Nyaki alielekeza upande wa mashtaka kuwasomea mashtaka washtakiwa hao.

Akiwasomea mashtaka yao, Wakili Shindai alidai shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu, shtaka linalowakabili wote. Wanadaiwa kati ya Mei mosi, 2025 na Aprili 2026, katika eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia taarifa za wateja na laini za simu zenye usajili wa watu wengine, pamoja na kadi za Nida za watu tofauti bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.

Mshtakiwa Gilbert Nyamitah (mwenyekiti mwendo) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mshtakiwa huyo na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kutumia laini za simu zilizosajili kwa majina ya watu wengine. Picha na Hadija Jumanne

Shtaka la pili hadi la 17 ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, mashtaka yanayomkabili Nyamitah peke yake.

Nyamitah anadaiwa kutenda makosa hayo Machi 31, 2026, katika eneo la Madale, Wilaya ya Kinondoni, ambapo alitumia laini 16 za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu tofauti bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wakati akijua ni kinyume cha sheria.

Baadhi ya laini za simu alizotumia zilikuwa zimesajiliwa kwa majina ya Daniel Matiko, Chacha Marwa, Zainabu Burunya, Manga Manga, Boke Mwita na wengine.

Shtaka la 18 hadi la 27 ni kutumia vibaya taarifa za wateja kwa kutumia kitambulisho cha Nida kusajilia laini za simu bila ridhaa yao na kinyume cha sheria, shtaka linalomkabili mshtakiwa Fanuel pekee.

Wakili Shindai alidai Fanuel anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 28, 2025 hadi Agosti 21, 2025 katika maeneo ya Nyanjage-Gachuma (Tarime), Busega na Rorya, ambapo akiwa wakala wa Kampuni ya Honora Tanzania PLC (Yas), aliyesajiliwa kwa jina la Roza Stivin Magoiga, alitumia vibaya vitambulisho 10 vya Nida vya watu wengine kusajilia laini mbalimbali za simu kinyume cha sheria.

Iliendelea kudaiwa kuwa shtaka la 28 ni la kutakatisha fedha, linalowakabili Nyamitah na Kulwa, ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Mei mosi, 2025 na Aprili 2026 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walijipatia Sh355 milioni kilichotokana na usajili wa laini, wakijua kuwa fedha hizo zimetokana na makosa ya awali ya kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika, hivyo ukaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Hakimu Nyaki alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa wanne, ambao ni Joram, Selumamala, Kapene na Aron, ambao hawana shtaka la kutakatisha fedha.

Masharti hayo ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaotambuliwa kisheria, watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo kurudishwa rumande.

Hakimu Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 18, 2026, itakapotajwa.