Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yamgomea DPP muda wa kukata rufaa

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya  Dar es Salaam, imekataa ombi la  Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) la kuongezewa muda wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Temeke, ikieleza kuwa alionyesha uzembe na kushindwa kutoa sababu za msingi.

Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imekataa ombi la Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) la kuongezewa muda wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Temeke, iliyomwachia huru mshtakiwa, Donatila Boniphas.

Uamuzi huo umetolewa Aprili 30, 2026 na Jaji Awamu Mbagwa aliyesikiliza maombi ya jinai namba 3816/2026.

Ombi hilo liliwasilishwa chini ya kifungu cha 379(1)(b) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), mwombaji aliomba kuongezewa muda ili aweze kukata rufaa kupinga hukumu iliyomwachia huru mshtakiwa huyo.

Akitoa uamuzi, Jaji Mbagwa alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imebaini kuwa mwombaji hakutoa sababu za kutosha kuhalalisha kuchelewa kuwasilisha rufaa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi, Mahakama ya Wilaya ya Temeke ilitoa hukumu Agosti 8, 2025 na kumwachia huru mshtakiwa. Baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo, upande wa mashtaka ulidai uliwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa Septemba 1, 2025.

Hata hivyo, ili kuendelea na rufaa hiyo, DPP alipaswa kuomba Mahakama Kuu iongeze muda kwa kuwa muda wa kisheria ulikuwa tayari umepita.

Katika maombi yao, upande wa mwombaji ulieleza kuwa kuchelewa huko kulisababishwa na taratibu za ndani za kupata kibali kutoka ofisini kwa DPP kabla ya kuendelea na mchakato wa rufaa.

Pia, waliomba Mahakama izingatie kuwa hukumu waliyokusudia kuipinga ilikuwa na upungufu wa kisheria.

Upande wa mjibu maombi ulipinga hoja hizo, ukisisitiza kuwa sababu zilizotolewa hazikuwa na uzito wa kisheria. Ulieleza kuwa taratibu za ndani za Serikali haziwezi kuwa kisingizio cha kuchelewesha haki, na kwamba upande wa mashtaka ulipaswa kuchukua hatua kwa wakati.

Katika uamuzi wake, Jaji Mbagwa alieleza kuwa ili Mahakama iridhie kuongeza muda wa kukata rufaa, mwombaji anatakiwa kuonesha sababu za kutosha zilizo wazi na zenye mashiko.

Alifafanua kuwa Mahakama huzingatia mazingira ya kila kesi, ikiwamo muda wa kuchelewa, sababu zilizotolewa na uwepo wa dalili za uzembe.

Mahakama ilibaini upungufu kadhaa katika maombi hayo, ikiwemo kushindwa kuambatanisha nakala ya hukumu iliyokusudiwa kupingwa, jambo lililoifanya ishindwe kujiridhisha iwapo kulikuwa na makosa ya kisheria.

Aidha, licha ya mwombaji kudai kuwa aliwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa kwa wakati, hakuwasilisha hati hiyo kuthibitisha madai yake.

Jaji alieleza kuwa kasoro hizo zinaashiria uzembe na ukosefu wa umakini katika uwasilishaji wa maombi.

“Mahakama haiwezi kuthibitisha madai ya ukiukwaji wa sheria bila kuiona hukumu yenyewe,” alisema Jaji Mbagwa.

Aliongeza kuwa kushindwa kuwasilisha nyaraka muhimu ni dosari kubwa inayodhoofisha hoja za mwombaji, na akatupilia mbali hoja ya kuchelewa kutokana na taratibu za ndani za ofisi ya DPP kwa kuwa haina uzito wa kisheria.

Kwa kuzingatia hoja zote, Mahakama ilihitimisha kuwa mwombaji hakutoa sababu za msingi za kuongezewa muda, hivyo ombi hilo likatupiliwa mbali.