Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yabatilisha mwenendo, hukumu ya aliyehukumiwa kunyongwa kwa kumuua mumewe

Muktasari:

  • Awali, wakati wa usikilizwaji kupitia maelezo ya onyo, Tatu Saidi alikiri kumuua mumewe (Mahona Nchimika) akimtuhumu kumpiga pindi akiwa amelewa na kuwa alimkodi Mwanza Buzuka kumuua mumewe, na Mwanza alikiri kuahidiwa Sh 200,000 kwa kazi hiyo.

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya kunyongwa hadi kufa waliyokuwa wamehukumiwa watu wawili akiwemo Tatu Saidi, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mumewe, Mahona Nchimika.

Pia, mahakama hiyo imeamuru kumbukumbu za kesi hiyo zipelekwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa upya kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, mrufani huyo na mwenzake, Mwanza Buzuka, watabaki kizuizini wakisubiri kesi yao kusikilizwa upya.

Hukumu hiyo imetolewa jana, Juni 24, 2025 na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo iliyoketi Tabora, ambao ni Rehema Mkuye, Dk Paul Kihwelo na Dk Ubena Agatho, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kubaini dosari za kisheria zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, ambapo warufani wote wawili waliwakilishwa na wakili mmoja wakati walikuwa na mgongano wa maslahi katika kesi hiyo.

Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, iliyosikiliza kesi hiyo baada ya hakimu kupewa mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.

Katika mahakama hiyo iliyowatia hatiani warufani wote wawili, kupitia maelezo ya onyo, Tatu alidaiwa kukiri kumuua mumewe baada ya kumkodisha mrufani mwenzake (Mwanza), kwa madai kuwa mumewe (marehemu) alikuwa akimnyanyasa pindi akinywa pombe.

Mauaji hayo yalitokea Aprili 22, 2017 katika Kijiji cha Lufwisi, Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, na katika maelezo ya onyo ya Mwanza, alikiri kumuua Mahona baada ya Tatu kumuomba afanye hivyo kwa madai kuwa atamlipa Sh 200,000, na walipomaliza walimzika karibu na bwawa.


Ilivyokuwa

Awali, katika mahakama hiyo ya chini, warufani walipandishwa kizimbani kwa kosa la mauaji kinyume na Kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, ambapo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita na vielelezo vitano.

Ilielezwa mahakamani kuwa Mahona (marehemu kwa sasa) na Tatu walikuwa mke na mume, ingawa hawakuwa sawa, na shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Rashid Ally, alieleza kupata taarifa kwa Tatu na baba mkwe wake kuwa Mahona amepotea.

Alieleza kuwa jitihada za kumtafuta zilianza, na baadaye mwili wa Mahona ulikutwa ukiwa umefukiwa karibu na bwawa, na Tatu alimtaja Mwanza kuhusika na mauaji hayo.

Shahidi wa pili, WP 7544 Koplo Fatuma, aliaandika maelezo ya mashahidi wote, ambaye katika kesi hiyo, alitoa maelezo ya Jilala Mahona (mtoto wa marehemu), aliyedai kushuhudia Mwanza akimpiga baba yake kichwani mara mbili na kusababisha kifo chake, kisha akaufukia mwili wake kwenye shimo karibu na bwawa.

Ilielezwa mahakamani kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na shahidi wa tano, Mganga Msaidizi Paschal John, aliyeeleza kuona michirizi miwili kwenye kichwa cha marehemu.

Warufani wote walipelekwa kwa Hakimu wa Amani, Armando Kassian (shahidi wa sita), ambapo katika maelezo yao ya onyo, Tatu alikiri kumkodi Mwanza ili amuue mumewe kwani alikuwa akimnyanyasa.

Mwanza alikiri kumpiga marehemu mara tatu kwa fimbo aliyopewa na Katambi Mahona, maelezo yaliyopokelewa kama kielelezo cha kwanza na pili.


Utetezi

Katika utetezi wao, Mwanza alieleza kukamatwa Julai 4, 2017 na mgambo na polisi ambao walimlazimisha kusaini karatasi bila kujua yaliyomo ndani.

Tatu alidai kulikuwa na mgogoro wa ardhi baina ya mumewe (marehemu) pamoja na baba yake, na kusababisha mumewe kuwa na msongo wa mawazo huku akikana kuhusika na mauaji ya mumewe.

Baada ya kusikilizwa pande zote mbili, Mahakama iliona upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo pasipo shaka na hivyo kuwatia hatiani warufani wote wawili kwa kosa la mauaji, kinyume na Kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu na kuwahukumu kila mmoja kunyongwa chini ya Kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu.


Rufaa

Baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo, warufani wote wawili walikata rufaa wakiwa na sababu nne, ambao kwa pamoja waliwakilishwa na Wakili Kelvin Kayaga, huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wawili.

Majaji hao, kabla ya kuanza kusikiliza rufaa hiyo, waliwataka waanze kushughulikia sababu hizo, ikiwemo maelezo yao ya onyo pamoja na kuwakilishwa na wakili mmoja wakati wa usikilizwaji, hivyo kusababisha mgongano wa maslahi.

Wakili Kelvin alikiri kuwa warufani wote wawili waliwakilishwa na wakili mmoja, ambapo aliipeleka mahakama kwenye ukurasa wa 136 na 137 wa kumbukumbu ya rufaa, ambapo Tatu katika maelezo yake ya onyo alimtaja Mwanza kuwa mhusika wa mauaji ya mumewe.

Katika ukurasa wa 140 hadi 143 wa rekodi ya rufaa, Mwanza alimtaja Tatu katika maelezo yake ya onyo kuwa alihusika na mauaji hayo, na wakili huyo kusema walikuwa na mgongano wa maslahi.

Wakili huyo alisema kuwa, wakati wa usikilizwaji, Mwanza aliyakataa maelezo yake na kudai aliteswa na kulazimishwa kusaini karatasi ambayo hakujua ndani yake imeandikwa nini.

Wakili huyo alisema alitilia shaka iwapo wakili aliyewawakilisha warufani wote wawili angeweza kumwakilisha mrufani mmoja kwa kumhoji mwenzake.

Wakili Kelvin alisema suala hilo limesababisha ubatili wa shauri hilo kuanzia yalipoanza kutolewa maelezo ya awali hadi uamuzi unaopingwa.

Wakili huyo aliiomba Mahakama kutumia Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani (The AJA), kubatilisha mwenendo na hukumu hiyo na kutoa amri ya shauri kusikilizwa upya mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mwingine atakayeongezewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili wa Jamhuri aliungana na hoja hiyo na kueleza kuwa haki ya uwakilishi wa kisheria ni ya msingi, na hivyo kila mrufani anapaswa kuwa na wakili wake, na kuiomba Mahakama iamuru kusikilizwa tena kwa kesi hiyo.


Uamuzi wa majaji

Jaji Mkuye alisema wamekagua kumbukumbu ya rufaa na kuzingatia mawasilisho ya mawakili, ambao kimsingi wanakubali kwamba mmoja wa warufani au wote wawili walinyimwa haki kwa kuwakilishwa na wakili mmoja.

Amesema uamuzi wao utaangalia iwapo warufani walipewa haki hiyo, na kuwa katika maelezo ya onyo ya warufani wote wawili, kila mrufani alimfungulia mwenzake hatia ya mauaji.

Jaji Mkuye alisema ili kuhakikisha kama warufani wawili walikuwa na mgongano wa kimaslahi, walipata fursa ya kupitia maelezo hayo ya onyo.

Mahakama ilinukuu sehemu ya maelezo ya Mwanza aliyosema:"Aprili 2017, saa moja hivi, dada yangu Tatu Saidi alikuja nyumbani kwangu na kuniambia kuwa mume wake amekuwa akimnyanyasa kwa kumpiga kila anaporudi nyumbani akiwa amelewa, walidhani amsaidie kumuua... na akaniagiza nimuue mumewe, akiahidi kunilipa Sh200,000".

Sehemu ya maelezo ya Tatu alinukuliwa:"Baada ya siku saba tangu achukue huyo ng’ombe, Mwanza aliniita tena na tukakutana porini na alinieleza kwamba siku hiyo usiku atatekeleza kazi yangu na ilikuwa saa 12 jioni... nilikaa huko mpaka majira ya saa 10 alfajiri nilipoamua kurudi, kwani tayari Mwanza alinijulisha kuwa amemaliza kazi ya kumuua na kumfukia kwenye shimo mume wangu Mahona Chinika…”

Jaji alisema kutokana na nukuu hizo, ni wazi kuwa warufani wote wawili walielekea kulaumiana na kuwa kuna mgongano wa kimaslahi kati yao katika kutenda kosa, na bado waliwakilishwa na wakili mmoja.

Jaji Mkuye alisema baada ya Mwanza kukana maelezo hayo, hali hiyo ilisababisha kesi kuendeshwa ndani ya kesi ili kubaini madai hayo, na kuwa katika hali kama hiyo wanashangaa jinsi wakili angeweza kumhoji mrufani mwenzake.

"Kwa kuzingatia hali kama hiyo, haingewezekana kwa wote wawili kuwakilishwa na wakili mmoja. Kama kanuni ya haki ya asili, kila mwombaji alikuwa na haki ya kupewa nafasi ya kumhoji mwenzake," alisema Jaji.

"Tunakubaliana na mawakili wote wawili kwamba warufani wote, kwa kuwa walikuwa katika mgongano wa kimaslahi, uwakilishi unaofaa wa mrufani yeyote au wote wawili haungewezekana na wakili mmoja, na kusababisha chochote kilichofanyika hadi uamuzi unaopingwa kuwa batili,"

Jaji Mkuye alihitimisha kuwa, kutokana na ukiukwaji huo uliosababisha kukosekana kwa haki, wanatumia mamlaka ya marekebisho waliyopewa chini ya Kifungu cha 4(2) cha AJA, kubatilisha mwenendo kuanzia usikilizwaji wa awali hadi hukumu, na kuagiza shauri lisikilizwe upya na kila mmoja awe na wakili wake.