Mahakama yamng’ang’ania aliyeiba Sh23,000, jela miaka 30

Muktasari:
- Said Ally alikata rufaa kupinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa unyang’anyi wa kutumia silaha kosa alilotenda Desemba 27, 2019 katika eneo la Tegeta wilayani Kinondoni karibu na benki ya Azania,ambapo aliiba pochi ya Rajabu Athumani iliyokuwa na Sh23,000 na kabla na baada ya kuiba alimtishia na kumjeruhi kwa panga
Arusha. Juhudi za Said Ally mkazi wa Dar es Salaam, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh23,000 zimegonga mwamba baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa yake.
Hii ni rufaa yake ya pili kushindwa ambapo awali alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni baada ya kukutwa na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu.
Awali ilielezewa kuwa Desemba 27, 2019 katika eneo la Tegeta wilayani Kinondoni karibu na benki ya Azania,mrufani huyo aliiba pochi ya Rajabu Athumani iliyokuwa na Sh23,000 na kabla na baada ya kuiba alimtishia na kumjeruhi kwa panga.
Hukumu ya rufaa hiyo ya jinai namba 844/2023 ilitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini, Juni 20,2025 iliyoketi Dar Es Salaam ambayo nakala yake imewekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Majaji hao ni Barke Sehel, Khamis Ramadhan Shaaban na Dk Ubena Agatho.
Jaji Sehel amesema baada ya kupitia kumbukumbu za rufaa hiyo na kusikiliza hoja za pande zote mbili,Mahakama hiyo imejiridhisha kuwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha lilithibitishwa bila kuacha shaka hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.
Awali
Awali siku ya tukio Rajabu ambaye alikuwa shahidi wa pili katika kesi ya msingi,alieleza kuwa akielekea katika Benki ya Azania akitoka eneo la Tegeta Kibaoni, ghafla alivamiwa na mtu asiyemfahamu ambaye alianza kumshambulia kwa kumkata na panga.
Alieleza kuwa watu walikusanyika wakiwemo mgambo wawili waliokuwa zamu katika Benki ya Azania, Tawi la Tegeta, ambao ni Mohamed Ally (shahidi wa kwanza ) na Hamisi Mohamed (shahidi wa tatu).
Mashahidi hao walieleza kumuona mrufani akimtishia Rajabu ambapo baada ya watu wengine kufika eneo la tukio,mrufani aliondoka na pochi ya Rajabu na kuwa hawakuweza kumkamata kwa kuwa alikuwa na panga na kuwa kwa kuwa ilikuwa mchana walimtambua kwa sura na umbo.
Mashahidi hao walimpeleka Rajabu Kituo cha Polisi cha Wazo ambako alipewa fomu ya polisi namba tatu (PF3) ambayo ilimwezesha kwenda hospitali kwa matibabu.
Januari 7, 2020 Rajabu alimuona mrfuani na kuripoti kwa shahidi wa pili na tatu ambao walifanikiwa kumkatamata na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Madale.
Awali kuanzia Desemba 28, 2019 shahidi wa nne, Koplo Rashid alipewa jukumu la kuchunguza kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo la tukio na kurekodi maelezo ya mashahidi.
Utetezi
Katika utetezi wake mrufani alikana kutenda kosa hilo na kudai alikamatwa Januari 3, 2020 katika eneo la Tegeta Kinyunyu kwa kosa la kubeba mchanga bila kibali.
Alieleza kuwa alipelekwa kituo cha polisi na kufunguliwa mashtaka ya wizi wa kutumia silaha ila alipohojiwa zaidi alikiri kumfahamu Rajabu pamoja na shahidi wa pili na wa tatu kwani alikuwa akiwaona.
Aidha aliomba kukubaliwa kwa maelezo ya Rajabu mahakamani hapo ambayo ilionyesha kuwa Rajabu alidai kuibiwa Sh 230,000 tofauti na Sh23,000 iliyoonyesha.
Baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ilimtia hatiani baada ya kujiridhisha kuwa mrufani alitambuliwa eneo la tukio akiwa ameshika panga.
Rufaa ya kwanza
Baada ya hukumu hiyo ya mahakama ya chini mrufani huyo alikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam,ambapo alikwaa kisiki baada ya mahakama hiyo kukubali kuwa mrufani alitambuliwa eneo la tukio.
Katika rufaa hii ya pili Oktoba 11, 2023 Said aliwasilisha hati ya rufaa ilitokuwa na sababu nne za rufaa na Januari 15, 2025 aliwasilisha hati ya ziada ya rufaa iliyokuwa na sababu tano za ziada za rufaa ikiwemo shtaka la unyang'anyi wa silaha kutothibitishwa.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mrufani alijiwakilisha mwenyewe bila kuwa na uwakilishi wa wakili huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili ambao walipinga rufaa hiyo.
Miongoni mwa sababu za rufaa ni pamoja na kudai kuwa shtaka linatofautiana kwani kituo cha polisi iliripotiwa kuwa ziliibiwa Sh230,000 badala ya Sh23,000 ambayo iko kwenye hati ya mashtaka.
Uamuzi Majaji
Jaji Sehel amesema baada ya kuangalia kumbukumbu za rufaa hiyo na uwasilishwaji wa pande zore mbili suala la uamuzi wao litakuwa ni iwapo shtaka linatofautiana na ushahidi kuhusu kiasi cha fedha kilichoibiwa.
Amesema wakili wa Jamhuri alieleza kuwa kielelezo cha kwanza cha utetezi kilikubaliwa kimakosa katika ushahidi kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa kilipokelewa bila mrufani kusomewa.
Jaji Sehel amesema ni msimamo wa sheria kwamba kila ushahidi wa maandishi uliooelekwa na kukubaliwa katika ushahidi lazima usomwe kwa mshtakiwa,akinukuu kesi ya John Mghandi dhidi ya Jamhuri, katika rufaa ya jinai 352/2018).
Amesema wanafuta kielelezo hicho kutoka kwenye kumbukumbu na kuwa baada ya kuifuta hakuna ushahidi mwingine wowote wa kuunga mkono malalamiko ya mrufani juu ya tofauti ya jumla iliyoibiwa.
“Hata hivyo, kwa kuchukulia kwamba kielelezo halijafutwa, tunakubaliana na wakili wa Jamhuri kwamba kiasi cha pesa kilichoonyeshwa kwenye kielelezo kilikuwa katika takwimu na si maneno,” amesema.
“Kwenye kielelezo ilionyesha ni Sh230,000 huku shahidi wa kwanza hadi wa tatu wakitaja kiasi kilichoibiwa kuwa ni Sh 23,000 kwa hali hiyo, tuna maoni thabiti kuwa kielelezo kilikuwa na hitilafu iliyosababishwa na sehemu ya kalamu ambapo sifuri ya ziada iliingizwa kimakosa,”amesema
Jaji Sehel amesema Rajabu alidai kuibiwa Sh 23,000 ushahidi uliothibitishwa na mashahidi wengine wawili hivyo wameridhika kuwa ushahidi uliotolewa ulikuwa sahihi na kwenye hati ya mashtaka.
Kuhusu hoja ya mrufani kulalamikia PF3 kushindwa kutolewa kuthibitisha majeraha aliyopata Rajabu, wakili wa Jamhuri alieleza kuwa nyaraka hiyo haikuwa muhimu kuthibitisha kosa la wizi wa kutumia silaha kwa mujibu wa kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu.
Jaji Sehel amesema kuwa kwa upande wao walipitia upya kumbukumbu ya rufaa na kuwa kwa maoni yao kutokuwepo kwa PF3 hakuathiri ushahidi unaothibitisha uhalifu wa unyang'anyi wa kutumia silaha na haidhoofishi kesi ya mashtaka.
Amesema kuhusu kuthibitishwa kwa kosa, yameibuka maswali ikiwemo iwapo mrufani alitambuliwa vema eneo la tukio na iwapo ushahidi kwenye kumbukumbu ulitosha kuthibitisha kosa la wizi wa kutumia silaha dhidi ya mrufani.
Mahakama hiyo ya rufani imejiridhisha kuwa kesi ya upande wa mashtaka dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo na kubariki adhabu dhidi yake.