Aliyemnyonga mkewe kwa kamba ya kiatu ahukumiwa kunyongwa

Muktasari:
- Akijitetea mahakamani, Abel Stephano alikana kutenda kosa hilo na kukiri kuwa kulikuwa na ugomvi mdogo baina yake na mkewe, kwani alitaka mke wake abadilishe dini na kuwa Mkristo, alieleza kuwa mkewe alimpa soda yenye sumu, akaumwa tumbo, kutapika hadi akapoteza fahamu na asubuhi alipoamka alikuta mkewe amefariki.
Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Abel Stephano baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mkewe Nuru Karim, kwa kumnyonga na kamba ya viatu.
Licha ya Abel kukana mahakamani kutenda kosa hilo, alikiri kuwa yeye na mkewe (marehemu) walikuwa na ugomvi mdogo katika ndoa yake kwani alitaka mkewe abadilishe dini na kuwa Mkristo lakini mkewe hakukubali.
Upande wa mashitaka ulieleza Mahakama kuwa tukio hilo lilitokea Julai 24, 2023 wakiwa nyumbani kwao eneo la Kitunda Mzinga ambapo wakiwa chumbani ugomvi baina yao ulitokea (Nuru) akitaka kwenda kwao.
Ilielezwa kuwa Abel alikutwa chumbani kwao huku mkewe marehemu akiwa amefariki dunia akiwa amelala kitandani na chini ya kitanda hicho kulikuwa na kamba ya kiatu iliyoelezwa kutumika kumnyongea hadi kufa.
Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, mshtakiwa alifanya hivyo ikiwa ni njia ya kumzuia marehemu asitoke nje ya nyumba hiyo na baada ya kutekeleza kitendo hicho alipiga kelele kuomba msaada, kwani hakuwa na funguo za mlango.
Majirani waliitikia kengele na kuvunja mlango na kumkuta mshtakiwa akiwa amesimama ndani, tukio liliripotiwa kwa mwenyekiti wa mtaa huo ambaye pia alitoa taarifa polisi na Abel kupelekwa Kituo cha Polisi cha Stakishari.
Jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alitoa hukumu hiyo Aprili 30, 2025 na kueleza kuwa baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Ilivyokuwa
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa wakati wa mahojiano Abel alikiri kumuua mkewe.
Alipofikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo, alikana kutenda kosa hilo ambapo katika kuthibitisha kosa upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watano, vielelezo viwili huku utetezi Abel akiwa shahidi pekee na vielelezo vitatu.
Shahidi wa kwanza, Karim Mohamed (baba wa marehemu), alisema marehemu na Abel walikuwa na mabishano kuhusiana na imani ya kidini ambapo Julai 23,2023 aliitwa na Abel kujadili suala hilo.
Alieleza kuwa kikao hicho kilipangwa kufanyika Julai 24, 2023 ila kabla hajaenda alipigiwa simu saa tisa alasiri na mama mwenye nyumba wa Abel akimjulisha kuwa binti yake amefariki.
Shahidi huyo alieleza kuwa Julai 25, 2023 alikwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuutambua mwili wa marehemu ambao alikuta ana uvimbe shingoni.
Shahidi wa pili, Ofisa wa Polisi ASP Abrugast Mathew alieleza siku ya tukio, alipewa taarifa na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Daniel Nyakobe kuwa Abel amemnyonga mkewe hadi kufa.
Alieleza kuwa akiwa na wapelelezi wenzake walipofika eneo la tukio, walikuta mwili wa marehemu ukiwa nusu utupu kitandani na waliona alama ya kamba shingoni kwa marehemu.
Aliieleza Mahakama kuwa alimuhoji Abel aliyemweleza kuwa usiku walikuwa na ugomvi uliosababisha mapigano baina yao na kuwa marehemu alikuwa akipiga kelele kwa sababu amekunywa pombe, hali iliyomfanya akasirike na kumdhibiti kwa kumfunga na kamba ya kiatu shingoni hadi aliponyamaza kimya.
Shahidi huyo alieleza kama sehemu ya uchunguzi wake, pia alichukua chupa tupu ya pombe hiyo, glasi ambayo walitumia kunywea pombe hiyo na Julai 27, 2023 vitu hivyo vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kuwa ripoti ilionyesha kinywaji hakikuwa na sumu.
Shahidi wa tatu alikuwa askari Polisi mwenye Fumba, alieleza kuwa alipokea vielelezo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwemo sehemu ya ini, tumbo, damu, na figo na kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, ripoti ya matibabu ilionyesha kuwa chanzo cha kifo kilitokana na kamba iliyokazwa shingoni, ambayo ilisababisha ukosefu wa oksijeni kwa marehemu.
Shahidi wa nne, Eda Vuhahula, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa mstaafu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye alitoa ushahidi kuwa, Julai 25, 2023 alimfanyia uchunguzi marehemu na kuwa Nuru alifariki kutokana na kukosa oksijeni.
Shahidi wa tano, Salome Moses, alithibitisha kuwa mshtakiwa alikodisha chumba nyumbani kwake na siku ya tukio alishuhudia marehemu akiwa amelala kitandani na kuripoti tukio hilo kwa mwenyekiti wa mtaa ambaye aliripoti Polisi.
Utetezi
Katika utetezi wake, Abel alikana shitaka hilo, ingawa alikiri kwamba marehemu alikuwa mke wake, na kwamba walikuwa na ugomvi mdogo katika ndoa yao, kwani alitaka mkewe abadili dini na kuwa Mkristo.
Kwa mujibu wa utetezi wake, alieleza kuwa mkewe alimpa soda yenye sumu akaanza kuumwa tumbo, akatapika na kupoteza fahamu ambapo asubuhi alipoamka alikuta mlango umefungwa, mkewe amelala kitandani akiwa amefariki.
Kutokana na hali hiyo alieleza kuwa alilazimika kuomba msaada kwa majirani zake ambao walivunja mlango na kuwa muda wote aliokuwa mahabusu, amekuwa akipatiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na Kifua Kikuu (TB) na kutoa vyeti vya hospitali.
Abel alijitenga na mashitaka yanayomkabili, na kuomba Mahakama imuone hana hatia na imuachie huru.
Uamuzi wa jaji
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji amesema kabla ya kuangalia masuala mengine upande wa mashitaka una wajibu wa kuthibitisha kosa pasipo kuacha shaka.
Jaji Mwanga amesema Nuru alikufa kifo kisicho cha kawaida kwa kunyongwa kama ilivyoshuhudiwa na shahidi wa nne na kuonyeshwa kwenye ripoti ya uchunguzi wa mwili.
Ushahidi huo ulithibitishwa na shahidi wa kwanza na wa pili ambao walishuhudia kumwona marehemu akiwa na alama shingoni na kuwa suala pekee linalobishaniwa ni iwapo Abel ndiye aliyesababisha kifo hicho.
Amesema kutokana na ushahidi wa mashtaka haina ubishi kuwa mshtakiwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na Nuru alipokuwa hai hadi alipokutwa amekufa chumbani kwao.
Jaji huyo amesema utetezi wa mshtakiwa kwamba marehemu alijiua kwa kunywa sumu na kumpa yeye sumu pia ni simulizi ya uongo, ambayo haiungwi mkono na ushahidi wowote.
“Shahidi wa nne alifafanua kuwa marehemu alinyongwa koo na sampuli iliyopelekwa kwa Mkemia wa Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa hakukuwa na sumu katika vinywaji hivyo,"
“Ni ukweli usiofichika kuwa mshtakiwa alikuwa akiishi na marehemu kama mke wake, na anakiri kuwa alimkuta mkewe akiwa amefariki chumbani kwao. Hata hivyo, ushahidi wa upande wa mashitaka ulithibitisha kuwa marehemu alinyongwa ,”
Jaji Mwanga amesema kutokana na ushahidi uliotolewa, Mahakama imeona kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo la mauaji dhidi ya mshtakiwa huyo bila kuacha shaka yoyote, hivyo kumkuta Abel na hatia na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.