Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahukumiwa kifo uvamizi CRDB, DCB na mauaji ya walinzi Suma JKT

Muktasari:

  • Walipora Sh45 milioni kwa ajili ya kununulia silaha, muuaji mmoja alipewa mgawo wa Sh2.5 milioni.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam imewahukumu adhabu ya kifo, watu wawili waliovamia benki za CRDB na DCB jijini Dar es Salaam na kuua watu watatu kwa mtutu wa bunduki.

Tukio hilo la mauaji lilitokea saa 8:40 mchana wa Desemba 8, 2015 katika eneo la Chanika wilayani Ilala, Dar es Salaam benki hizo zilipovamiwa. Miongoni mwa waliouawa ni walinzi wawili wa Suma-JKT.

Waliouawa wametajwa kuwa ni Ramadhan Halili na Shani Mohamed waliokuwa walinzi wa Suma JKT katika Benki ya CRDB. Mwingne ni Gabriel Ngwangai.

Ingawa hukumu inawataja waliohukumiwa ni washtakiwa Mohamed Hassan na Rajabu Ally, Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amewatambulisha watu hao kuwa masheikh.

Hukumu imetolewa Aprili 28, 2025 na Jaji Butamo Phillip na nakala yake imewekwa katika tovuti ya Mahakama Aprili 30, 2025.

Jaji Phillip amemwachia huru mshitakiwa wa tatu, Kulwa Athuman kwa kukosekana ushahidi dhidi yake.

Usikilizwaji wa kesi hiyo uliendeshwa pasipo kutaja majina ya washtakiwa wala anuani za makazi, mashahidi wa upande wa Jamhuri walitambulishwa mahakamani kwa namba P25, P43, P22, P7, P27, P20, P23 na P24.

Mbali na kutotajwa majina na anuani za makazi yao, lakini mashahidi walitoa ushahidi wakiwa wamefichwa kwenye kizimba maalumu kilichowekwa mahakamani ili kutotoa utambulisho wao halisi wa sura.


Ushahidi ulivyokuwa

Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, aliieleza Mahakama mwaka 2016 alikuwa miongoni mwa maofisa waliokuwa katika kikosi kazi kilichoundwa kufanya upelelezi wa matukio ya ugaidi, ambayo yalihusisha uvamizi wa benki hizo mbili.

Shahidi alidai marehemu katika shauri hilo waliuawa wakati wa uvamizi wa benki hizo ambazo zinatizamana, ushahidi ambao uliungwa mkono na shahidi wa pili wa Jamhuri aliyekuwa ofisa mfawidhi wa CRDB.

Shahidi huyo alieleza benki hiyo ilikuwa na walinzi wawili wa Suma JKT, mmoja mwanamke na mwingine mwanamume. Mlinzi mwanamke alipangwa ndani ya benki na mwanamume nje akiwa na bunduki.

Alieleza Desemba 8, 2015 saa 7:40 mchana benki ilivamiwa na watu wenye silaha, wakati huo alikuwa amekwenda kula jirani na ofisi yake. Alipokuwa akisubiri aletewe chakula alisikia milio ya risasi.

Milio hiyo alisema ilitokea uelekeo wa benki, hivyo alikimbilia Kituo cha Polisi Chanika kutoa taarifa, huko alimkuta ofisa wa polisi ambaye alimfahamisha naye amesikia milio hiyo na ametoa taarifa kituo cha Stakishari.

Baada ya kutoa taarifa, waliongozana na ofisa huyo wa polisi hadi benki. Walipofika alikuta wafanyakazi wenzake wakiwa nje wanalia, wakieleza walinzi wote wawili wameuawa. Alidai alimuona Ramadhan akiwa amelala sakafuni.

Alieleza alikuwa amekufa, pia kulikuwa na matone ya damu chini ya kifua. Alimuona mlinzi mwingine, Shani akiwa na majeraha kichwani amelala sakafuni naye alikuwa tayari ameshapoteza maisha.

Shahidi wa nne, mfanyabiashara na mkazi wa Chanika, alieleza Desemba 8, 2015 alisikia mlio usio wa kawaida alipokuwa akitembea umbali wa takribani mita 100 kutoka zilipo benki za CRDB na DCB zinazotazamana.

Alisimama kutazama ni nini kilichotokea, katika kipindi kifupi alisikia milio ya risasi na akaona watu wakiwa wanakimbia.

Kando mwa barabara alimuona mtu akiwa ameshika bunduki anazuia magari yasipite.

Mtu huyo alionekana akifyatua risasi uelekeo wa magari yaliyolazimisha kupita ili kuwatisha madereva.

Alidai wakati huo yeye alikuwa umbali wa mita 12 tu kutoka mahali alipokuwa amesimama akishuhudia purukushani hizo.

Ni wakati huo alisikia majibizano ya risasi kati ya walinzi wa benki hizo na watu waliokuwa na silaha. Aliona gari likija kutokea benki, mtu mwenye silaha alipanda wakatokomea kusikojulikana.

Shahidi wa sita alieleza mmoja wa walinzi aliyeuawa, Ramadhan Halili alikuwa mpwa wake. Usiku wa siku la tukio alipigiwa simu na uongozi wa Suma JKT. Alikwenda siku iliyofuata akajulishwa kifo cha mpwa wake.

Kwa upande wake, shahidi wa nane, ambaye ni ofisa wa Polisi aliyekuwa akifanya kazi kituo cha Stakishari katika Idara ya Upelelezi, alieleza alishiriki wakati wa uchunguzi wa miili ya walinzi hao uliofanywa na daktari ili kubaini chanzo cha kifo.

Baadaye alikwenda kumuona Gabriel Ngwangai aliyekuwa amelazwa hospitali akiwa na majeraha ya risasi ambaye alifariki dunia baadaye.


Utetezi wa washtakiwa

Katika utetezi wao, washtakiwa hawakuwa na ubishi kuwa marehemu wote watatu hawakufa kifo cha kawaida lakini walidai kamwe hawakushiriki kwa namna yoyote ile na hawana wanachofahamu kuhusu tukio la uvamizi CRDB na DCB.


Hukumu ya Jaji

Akichambua ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Phillip amesema ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwa marehemu waliotajwa waliuawa kwa kupigwa risasi katika uvamizi wa benki za CRDB na DCB.

“Nimeuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi. Hata hivyo, haujaleta shaka yoyote kuwa marehemu waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa uvamizi wa benki hizi mbili, hivyo hawakufa kifo cha kawaida,” amesema.

Katika kuthibitisha kuwa ni washtakiwa ndio waliohusika, Jaji amerejea ushahidi wa shahidi wa kwanza aliyetoa ushahidi kuwa Juni 13, 2015 akiwa Kituo cha Polisi Tazara, alipata taarifa fiche kuwa mmoja wa walioshiriki ni Mohamed Hassan.

Kwamba alikuwa anaishi Mbagala Misheni jirani na kiwanda cha KTM. Mtoa taarifa alimpa mwonekano wake na baada ya kupata taarifa hizo walikwenda eneo hilo akiwa na askari wengine wanane na kumkamata.

Kulingana na shahidi huyo, katika mahojiano mshtakiwa alikiri kushiriki tukio la uvamizi wa benki hizo. Alikubali kutoa ushirikiano na kuwapeleka mahali walipo washirika wake ambao dhamira yao ni kuanzisha Dola la Kiislamu nchini.

Jaji amesema pamoja na ushahidi wa mashahidi wengine, lakini shahidi wa tano ndiye aliandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo wa kwanza na kueleza namna alivyoshiriki mwanzo hadi mwisho katika tukio hilo.

Shahidi wa saba alieleza namna alivyoandika maelezo ya mshtakiwa wa pili, Rajabu Ally aliyeeleza kila kitu kwamba, baada ya kuvamia benki hizo na kuwaua walinzi hao wawili, waliiba pia fedha. Baadaye alipewa mgawo wa Sh2.5 milioni.

Shahidi wa nane alieleza alivyoandika maelezo ya mshtakiwa wa tatu ambaye ameachiwa huru na mahakama. Alidai alimweleza kuna watu wanataka kuanzisha Dola ya Kiislamu.

Katika maswali ya dodoso kutoka kwa wakili wa mshtakiwa huyo, shahidi alidai  kamera za usalama (CCTV) hazikuweza kunasa tukio hilo lakini wahalifu hao waliiba Sh25 milioni katika Benki ya CRDB na Sh20 milioni za DCB.

Jaji amesema vielelezo namba P2 na P3, vinaonyesha mshtakiwa wa kwanza na wa pili walieleza ushiriki wao katika uvamizi wa benki hizo mbili, maelezo yanayoshabihiana na taarifa fiche alizokuwa amepewa shahidi wa kwanza.

Katika vielelezo hivyo ambavyo ni maelezo ya washtakiwa hao, walieleza kwa kirefu juu ya uvamizi huo na kwamba lengo lao lilikuwa kutafuta fedha katika benki hizo ili kuzitumia kununua silaha ili kuanzisha dola la Kiislamu nchini.

Kwa kuchambua ushahidi huo na vielelezo hivyo, Jaji amesema ameridhika kuwa upande wa mashitaka uliweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa wa kwanza, Mohamed na wa pili, Rajabu lakini ulishindwa kwa wa tatu.

Jaji amesema washtakiwa hao walikuwa na nia ovu kutokana na silaha walizotumia, kwani marehemu walikuwa na majeraha maeneo mbalimbali ya miili yao hivyo nao wanahukumiwa kifo, lakini mshtakiwa wa tatu anaachiwa huru.