Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ya Rufani yaamuru sheria ya haki za kiraia irekebishwe

Muktasari:

  • Jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani limeamuru iwapo marekebisho hayatafanyika ndani ya muda, basi yaliyofanywa awali hayatakuwa na nguvu yoyote ya kisheria.

Arusha/Dar. Mahakama ya Rufani imeelekeza ndani ya miezi 12 (mwaka mmoja) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lirekebishe kwa kufuta vifungu vya 6 na 7 vya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya mwaka 2020, ambavyo vilifanyia marekebisho kifungu cha nne cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (Bradea).

Mahakama hiyo iliyoketi jijini Dar es Salaam, imesema endapo hilo halitafanyika ndani ya muda huo (ulioanza jana Juni 13, 2025 hukumu ilipotolewa), basi marekebisho hayo yaliyofanywa kupitia sheria hiyo hayatakuwa na nguvu ya kisheria.

Jopo la majaji Mary Levira, Sam Rumanyika na Paul Ngwembe limetoa amri hiyo baada ya kuikubali rufaa iliyokatwa na mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hukumu hiyo ilisomwa jana Juni 13, 2025 kwa njia ya video, mbele ya mrufani (Ole Ngurumwa), ambaye pia aliwakilishwa na mawakili wake, Profesa Issa Shivji, John Seka, Dk Rugemeleza Nshala na Paul Kisabo.

Mjibu rufaa aliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Narindwa Sekimanga aliyeshirikiana na Wakili wa Serikali, Lucy Kimaryo.

Katika rufaa namba 134 ya mwaka 2022 mrufani alikuwa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania ya Februari 15, 2022 iliyotamka vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5) vya sheria hiyo havipingani na Katiba wala mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.

Mahakama Kuu ilitupilia mbali maombi ya Ole Ngurumwa kwa hoja sita ambazo ni vifungu vinavyokamilisha na kuunganisha Ibara ya 26(2) na 30(3) ya Katiba, hitaji la kuonesha masilahi binafsi lipo kwenye Ibara ya 26(2) na marekebisho hayo yanaendanana na misingi ya mgawanyo wa madaraka, utawala wa sheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Zingine ni kufungua kesi dhidi ya AG badala au kwa niaba ya viongozi wa juu ni sahihi kikatiba, hitaji la kutumia njia zingine za kisheria linakubaliana na uwepo wa taasisi kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kwamba, marekebisho hayo yalifanywa kwa nia njema na yanalindwa chini ya ibada ya 30(2) ya Katiba.

Mahakama ya Rufani imekubali rufaa hiyo na kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu na amri zilizotolewa. Hata hivyo, haikutoa amri kuhusu gharama za rufaa hiyo.

Ole Ngurumwa kupitia mawakili wake, alidai vifungu hivyo vilionekana kuwa vikwazo katika mashauri ya kikatiba yenye masilahi ya umma kwani vinamzuia Mtanzania binafsi kupeleka maombi mahakamani kulinda haki na uhuru ulioanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mrufani alidai Juni 19, 2021 Serikali ya Tanzania ilichapisha katika Gazeti la Serikali Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya mwaka 2020, iliyofanya mabadiliko makubwa katika Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu kwa kuongeza vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5).

Alieleza kifungu cha 4(2) kinahitaji kila mtu anayepeleka shauri Mahakama Kuu kuhusu ukiukwaji wa haki za kikatiba kuambatanisha kiapo kinachoeleza jinsi alivyoathirika binafsi, kifungu cha 4(3) kinabana zaidi mashauri ya masilahi ya umma kwa kutaka mlalamikaji kuonyesha masilahi binafsi kwa mujibu wa Ibara ya 30(3) ya Katiba.

Mrufani alieleza kifungu cha 4(4) kinahitaji pale mtu anapotafuta haki dhidi ya viongozi wa juu serikalini, wakiwamo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu, kesi ipelekwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu badala ya viongozi hao moja kwa moja.

Kuhusu kifungu cha 4(5) alisema kinataka mlalamikaji kutumia njia zote nyingine za kisheria zilizopo kabla ya kufungua kesi chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu.


Hukumu ya majaji

Jopo la majaji katika hukumu iliyopatikana katika mtandao wa Mahakama limebatilisha vifungu hivyo vinavyolalamikiwa likieleza kifungu cha 4(2) kinavunja dhana ya mashauri ya masilahi kwa umma kwa kuhitaji waathirika binafsi pekee, hali inayokinzana na Ibara ya 26(2) ya Katiba.

Kuhusu kifungu cha 4(3) imeelezwa ni batili kwa kuwa kinachanganya masharti ya Ibara ya 30(3) (maslahi binafsi) na haki za masilahi kwa umma zinazolindwa chini ya Ibara ya 26(2).

Majaji wamesema kifungu cha 4(4) ni batili kwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hana mamlaka ya kikatiba kuwakilisha mihimili mingine, hasa Mahakama au viongozi wa kisiasa walio huru kikatiba kama Jaji Mkuu.

Kifungu cha 4(5) kimeelezwa kuwa batili kwa kuwa hakuna sheria nyingine zinazotoa nafuu ya moja kwa moja kwa mashauri ya masilahi ya umma.


Kauli za mawakili

Akizungumzia hukumu hiyo, Profesa Shivji amelipongeza jopo la majaji waliosikiliza shauri hilo kwa kufanya uamuzi wa haki ambao utakuwa na manufaa kwa Watanzania wote. Ameeleza uamuzi huo ulikuwa faraja kubwa kwake.

"Jopo la majaji lililoongozwa na Jaji Levira, kwa kiasi fulani limetoa uamuzi wa kijasiri hasa kutokana na mazingira yetu. Uamuzi kama huu hatujauona katika kipindi cha miaka 10 hivi," amesema.

Profesa Shivji amesema Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamwezesha mtu au kikundi ambacho kimeathirika, kwenda mahakamani kudai haki zao na kuonesha namna ambavyo wameathirika na namna Katiba imevunjwa.

Amesema Ibara 26(2) ya Katiba inasema kila mtu ana haki ya kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria ili kulinda Katiba na mfumo wa sheria.

"Sheria ilikuwa inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi. Marekebisho hayo yalikuwa yanarekebisha Katiba kwa mlango wa nyuma," amesema.

Profesa Shivji amesema sheria hiyo ilikuwa inatoa kinga kwa viongozi wakuu kushtakiwa mahakamani, jambo alilosema halifai kwani Tanzania ni Jamhuri na si nchi ya kifalme.

Amesema: "Hakuna aliye juu ya sheria."

Wakili mwandamizi, Mpale Mpoki amesema kesi hiyo ni ya umma na ushindi huo si wa Ole Ngurumwa pekee kwa kuwa alikata rufaa hiyo, bali ni wa Watanzania wote ambao sasa wana uwezo wa kwenda mahakamani dhidi ya kiongozi yeyote wanapoona haki zao zinavunjwa.

"Ushauri wangu ni kwamba, pale Mahakama inapoona kuna kesi kubwa ya umma kama hii, iwaite marafiki wa Mahakama wasaidie kufikia uamuzi wa haki," amesema.

Wakili John Seka amesema hakuna aliye juu ya sheria anayefanya matendo yasiyo ya haki atahukumiwa kwa jina lake na siyo kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama sheria hiyo ilivyokuwa inaelekeza.

Amewataka wananchi wasisite kwenda mahakamani wanapoona viongozi wao wanavunja haki zao, kwani milango imefunguliwa kupitia sheria hiyo iliyokuwa inaweka zuio la kuwashitaki viongozi wa juu kama vile Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika au Jaji Mkuu.