Mahakama yaitaka mechi ya Simba, Yanga

Dodoma. Baada ya timu ya Mahakama kunyakua makombe 15, sasa inajipanga kuomba mechi ya kirafiki dhidi ya timu za Ligi Kuu hasa Yanga na Simba.
Akizungumza jana wakati akipokea makombe hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema lengo la kuomba mechi hizo ni kujipima nguvu.
“Natamani kuiona timu ya michezo ya mahakama inacheza mechi kubwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja na timu zinazoshiriki ligi Kuu ya Bara,”alisema.
Akijibu hoja ya watumishi hao ya kuongezwa muda, Ole Gabriel alisema ombi la lao la kuongezewa muda wa mazoezi litafanyiwa kazi Kwa sababu michezo nayo ni sehemu ya kazi.
"Nitazingatia maombi yenu na kuyafanyia kazi kwa sababu ili la muda wa mazoezi lipo ndani ya uwezo wangu hivyo nitalifanyia kazi ili timu yetu iweze kusonga mbele,"amesema.
Hata hivyo ametoa rai kwa viongozi wa timu hiyo kuita wachezaji kutoka mikoa mbalimbali ambao ni watumishi wa mahakama ya Tanzania ili waweze kuungana na timu hiyo kuongeza nguvu kwenye kikosi cha timu hiyo.
Mwajabu Bwire ambaye ni mshindi wa mashindano ya Baiskeli amesema, michuano ya Mei Mosi ilikuwa na ushindani mkubwa lakini alijitahidi kuhakikisha anaipa ushindi timu ya michezo ya Mahakama.
Katibu wa timu ya michezo ya Mahakama, Robert Tende ameomba kuongezewa muda wa kufanya mazoezi ili waweze kutwaa ubingwa wa jumla katika michuano ijayo ya Mei Mosi na ile ya Shimiwi.
Amesema timu hiyo imeshika nafasi ya nne katika michuano ya Mei Mosi iliyofanyika Mei mkoani Singida na hiyo imetokana na ufinyu wa muda wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na michuano mbalimbali wanayoshiriki.
Tende amesema kikosi cha michezo mbalimbali cha timu hiyo,kama riadha, netiboli, soka,timu ya kuendesha baiskeli, darts pamoja na Karata wanahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi ili waweze Kuga ya vizuri katika michuano ijayo.
"Tunaomba tuongezewe muda wa kujiandaa na mashindano mbalimbali tunaweza kufanya vizuri zaidi ya mwaka huu katika michuano ya Mei Mosi na Shimiwi,"amesema.
Katika hafla hiyo, washindi wamekabidhiwa kuwakabidhi vyeti lengo likiwa ni kuonyesha mahakama inatambua mchango unaofanywa na timu ya michezo ya Mahakama ya Tanzania.