Simba kamili kwa dabi, Nouma na Che Malone fiti

Daktari wa klabu ya Simba Edwin Kagabo amesema kuwa wachezaji wote waliokuwa wanasumbuliwa na majeraha kikosini, wamepona na wapo fiti kwa ajili ya mchezo ujao.
Simba ipo kambini ikijiandaa na mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga ambao umepangwa kupigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Awali mechi hii ilipangwa kupigwa Machi 8, 2025, lakini ikasogezwa mbele muda mchache kabla ya mechi hiyo baada ya Simba kuandika barua na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa hawatacheza mchezo huo kutokana na kuzuiwa na wale wanaodaiwa kuwa walinzi wa Yanga kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mkapa siku moja kabla ya mchezo huo.
Hata hivyo ni mchezo ambao umejaa giza nene baada ya Yanga kutangaza kuwa haitashiriki kwenye mechi hiyo hadi itakapopata majibu kwanini mchezo wa Machi 8, 2025, uliahirishwa na kuzua sintofahamu kati yao na Bodi ya Ligi ambayo imeendelea kushikilia kuwa mchezo upo palepale.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kagabo amesema kuwa wachezaji wote kwa sasa wapo fiti na wanaendelea na mazoezi yao wakiwemo wale ambao walipata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), uliopigwa kwenye Uwanja wa Kwaraa Manyara na Simba kupoteza kwa mabao 3-1.
Wachezaji wa Simba waliokuwa na majeraha ni Moussa Camara, Valentino Nouma, Che Malone Fondoh pamoja na Mzamiru Yassin ambaye hakuonekana kikosini kwa muda mrefu.
"Wachezji wote ambao walikuwa wanasumbuliwa na majeraha wamerejea na wapo fiti kwa ajili ya mchezo wetu wa Dabi ya Kariakoo Jumapili dhidi ya Yanga.
"Mastaa wetu Moussa Camara, ambaye aliumia kifua, Nouma naye alikuwa na changamoto sawa na Che Malone pamoja na Mzamiru kwa sasa wote wapo fiti na wanafanya mazoezi na timu.
"Kwa ujumla ni kwamba wachezaji wote wapo fiti na tunaendelea na mazoezi yetu kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili, hakuna hata mmoja ambaye ana majeraha kwa sasa," alisema Kagabo.
Huu ni mchezo wa Ligi Kuu wa pili kwa timu hizo mbili kubwa hapa nchini baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 baada ya beki Kelvin Kijili kujifunga.
Mchezo huu unaweza kuwa ndiyo ulioshikilia ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kutokana na tofauti ya pointi kwa timu hizo mbili kwenye msimamo.
Yanga ndiyo inaongoza ligi kwa sasa ikiwa na pointi 73, huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 72 zikiwa zimebaki mechi tatu tu msimu umalizike.