Serikali yajitenga na ishu ya dabi, yawaachia TFF

Muktasari:
- Mchezo baina ya Yanga na Simba ambao unatarajia kuchezwa Jumapili, giza limeendele kutanda kutokana na msimamo ya Yanga kugomea.
Dar es Salaam. Sakata la mchezo kati ya Simba na Yanga limeingia bungeni ambapo Serikali imesema haiwezi kuingilia kwa kuwa mchezo wa mpira una kanuni zake kitaifa na kimataifa.
Kauli hiyo ilifuatia swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga leo Juni 11, 2025 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Sanga amesema kuimarisha timu ya Taifa ni pamoja na kuhakikisha kwamba sheria na taratibu za michezo zinafuatwa nchini.
“Ligi yetu inaelekea mwisho lakini kumekuwa na mvutano wa hizi timu mbili na viongozi wa TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania), ipi kauli ya serikali,”amesema.
Hata hivyo kabla ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutoa kibali kwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) kujibu Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya alianza kuzungumza nje ya kipaza sauti.
Kufuatia hatua hiyo, Dk Tulia alimhoji Bulaya kama anataka kumsaidia kujibu Naibu Waziri kujibu.
Hata hivyo, baadaye Spika alimpa nafasi Mwana FA kujibu swali hilo ambapo amesema kama ambavyo wabunge wanafahamu shughuli za mchezo wa mpira wa miguu zina mamlaka zake za kimataifa na za kitaifa.
“Na tumekuwa tukisisitiza mara kwa mara Serikali kutoingilia moja kwa moja uendeshaji wa shughuli hizo ili kuepuka kuja pengine hata kufungiwa na FIFA (Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani) katika nyakati hizi ambapo kitakwimu nchi yetu inafanya vizuri sana katika uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu,”amesema.
Amesema mamlaka za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za mpira wa miguu nchini ziko chini ya TFF lakini pia na bodi ya ligi kuu.
Amesema Serikali hata taarifa ambazo wanazitoa bungeni huwa wanapata taarifa kutoka katika mamlaka hizo kuhusu mchezo huo.
“Tunafuatilia kwa karibu jinsi ambavyo mgogoro huu unavyoendelea kutatuliwa, lakini huku tukijaribu kwa kiwango kikubwa kabisa kutoingilia moja kwa moja maamuzi ya TFF na bodi ya ligi,”amesema.
Amesema wanafanya hivyo kwa kwa kuhakikisha hawaingilii moja kwa moja ili kuepuka nchi kufungiwa kwa vile mchezo wa mpira wa miguu unajiendesha wenyewe.
Baada ya kumaliza kujibu, Dk Tulia alimpa nafasi Bulaya aseme alichotaka kukisema ambapo alisema taratibu na sheria ni pamoja na kupata ripoti kwa nini mchezo wa tarehe 8 hawakucheza.
Kauli hiyo ilifanya Dk Tulia kumweleza Bulaya kwa kuwa yeye alikuwa akikataza ushabiki lakini leo anautaka ushabiki.
“Haya mbunge wa Simba anayetaka kumjibu,”amesema ambapo alimruhusu Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko kumjibu Bulaya.
Akimjibu Matiko amesema kama alivyojibu naibu waziri lazima waheshimu kanuni ambazo zinaongoza mchezo wa mpira wa miguu ili waweze kukuza vipaji na wasiweke ushabiki.