Yanga yazidi kuweka ngumu ishu ya dabi

Muktasari:
- Katika mkutano huo, wazee hao waliitaka jamii ya Yanga, ikiwemo wanachama na mashabiki wa ndani na nje ya Dar es Salaam, kubaki nyumbani siku ya mechi kwani Yanga haitashiriki mchezo huo.
Dar es Salaam. Joto la mpambano wa watani wa jadi limezidi kupanda huku wazee wa Klabu ya Yanga wakisisitiza kwa mara nyingine tena kuwa hawatashiriki mechi ya dabi dhidi ya Simba, iliyopangwa kuchezwa Juni 15 mwaka huu.
Wazee hao wameeleza msimamo wao mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, wakitoa sababu mbalimbali na kuwataka mashabiki wao kuzingatia uamuzi huo.
Katika mkutano huo, wazee hao waliitaka jamii ya Yanga, ikiwemo wanachama na mashabiki wa ndani na nje ya Dar es Salaam, kubaki nyumbani siku ya mechi kwani kwa mujibu wao, klabu ya Yanga haitashiriki kabisa mchezo huo ambao awali ulipangwa kuchezwa Machi 8, 2025 lakini baadaye ukaahirishwa.
“Tunasema wazi mbele ya taifa na mbele ya mashabiki wetu popote walipo, Yanga hatuchezi mechi ya dabi ya tarehe 15. Hatupo kwenye mchezo huo,” amesema Shabani Omary Mgonja, Mratibu wa Matawi ya Klabu ya Yanga mkoa wa Dar es Salaam.
Wazee hao wameendelea kusisitiza kuwa msimamo huo si wa hisia bali ni wa kikanuni na kiitikadi, wakidai kuwa mazingira ya uendeshaji wa ligi hayaridhishi na hayatoi haki kwa klabu yao.
Aidha wameenda mbali zaidi kwa kuionya kampuni yenye haki za kurusha matangazo ya mpira wa miguu hapa nchini kuacha kutumia jina la Yanga, nembo au wanachama wake katika matangazo ya mchezo huo, kwa kuwa wamekwishaweka wazi msimamo wao wa kutoshiriki.
“Wapo wadau wetu ambao tuna haki nao ya kimatangazo na kimaudhui tunaomba waache mara moja kutumia jina la klabu yetu nembo yetu au wanachama wetu kwa ajili ya kuitangaza mechi ya tarehe 15 pia tunawaomba hata wadau wengine wowote wa habari waache kabisa kufanya hivyo.”
Wazee hao wametoa wito kwa mashabiki wa Yanga waliopo mikoani wasihangaike kukata tiketi wala kusafiri kuja Dar es Salaam, kwani wanaamini itakuwa ni kupoteza muda na fedha zao kwa tukio ambalo halitawahusu.
Kwa mujibu wao, Yanga imebakiza mechi tatu pekee msimu huu, mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la FA. Hivyo, kwao, suala la dabi tayari limefungwa na halipo tena kwenye ajenda ya klabu hiyo.
Mbali na msimamo huo, wazee hao wametoa wito wa kuvunjwa kwa bodi ya ligi, wakimtaja Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mtendaji Mkuu na Kamati ya Uendeshaji kuwa hawana uaminifu wa kutosha katika kushughulikia masuala ya ligi na haki za vilabu.
“Yanga haiwezi kupeleka timu kwa kamati ya ligi ileile ambayo ilihahirisha mechi ya Machi 8, tunataka yale yalioainishwa kwenye barua yetu kwa maana kwamba kamati ya bodi kuvunjwa yafanyiwe kazi, lakini bado mpaka sasa hakuna mabadiliko yoyote ambapo mtendaji mkuu wa bodi ya ligi yupo mpaka sasa, mwenyekiti wa bodi naye yupo.
“Yanga haiwezi kupeleka timu kucheza mchezo mwingine ikiwa hawa waliolalamikiwa kwenye barua yetu ya tarehe tisa bado wapo madarakai.”
Mchezo huo namba 184 wa raundi ya pili ya Ligi Kuu, ambao awali ulipangwa kuchezwa Machi 8, 2025, uliahirishwa baada ya Simba kudai kuzuiwa na wanaodaiwa kuwa walinzi wa Yanga kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa siku moja kabla ya mechi ikiwa kama timu mgeni. Tukio hilo lilizua mtafaruku mkubwa kuelekea mechi hiyo ambapo Bodi ya Ligi Kuu ilitangaza kuhairishwa kwa mchezo huo, huku Yanga wakitoa tamko kuwa hawatacheza tena mechi hiyo.
Yanga walipeleka malalamiko yao katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), wakitaka mechi hiyo isichezwe na wapatiwe pointi tatu, lakini shauri hilo halikufua dafu baada ya CAS kutupilia mbali ombi lao na kuwataka kumalizana na mamlaka za ndani kwanza.
Hivi karibuni, TPLB ilitangaza rasmi kwamba mechi hiyo ya dabi sasa itapigwa Juni 15, 2025. Hata hivyo, Yanga wameibuka tena na kuzidi kutilia mkazo msimamo wao wa kutoshiriki mchezo huo, huku Simba wenyewe wakiwa wameshatangaza kuwa wanaingia kambini kesho kujiandaa na mechi hiyo.