Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yabatilisha hukumu aliyemuua mkewe, mtoto

Muktasari:

  • Ilielezwa mahakamani kuwa Omary Matonya alimchinja mkewe na mtoto kwa madai kuwa mkewe amekuwa na mahusiano na kaka yake (Omary) hadi akamzalisha na kudai mtoto huyo amefanana na huyo kaka yake.

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa Omary Matonya baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Moshi Daudi na mtoto wao, Mohamed Omary.

Upande wa mashitaka uliieleza mahakama kuwa Omary alimchinja mkewe na mtoto huyo akidai kuwa mkewe alikuwa na mahusiano na kaka yake (Omary) na mtoto huyo (Mohamed) alikuwa akifanana na huyo kaka yake.

Pia, mahakama hiyo imeamuru kumbukumbu za kesi hiyo zipelekwe Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora ili iweze kufanya marejeo kisha uamuzi, kwa kuhamisha kesi kwa Hakimu Mkazi aliyeongezewa mamlaka kwa ajili ya kusikiliza upya kesi hiyo.

Hata hivyo, imeamuru mrufani huyo kusalia kizuizini akisubiri kesi yake kusikilizwa upya.

Omary alihukumiwa adhabu hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa hayo mawili ya mauaji, ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mbele ya hakimu aliyeongezewa mamlaka alisikiliza na kutoa hukumu hiyo.

Katika kesi ya msingi, mrufani huyo alidaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2018 katika eneo la Mwanzugi, Kijiji cha Kalema, Kata ya Tura, Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora ambapo aliwaua mkewe na mtoto wake.

Katika rufaa hiyo ya iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini ambao ni Rehema Mkuye, Dk Paul Kihwelo na Dk Ubena Agatho, walioketi Tabora.

Majaji hao wametoa hukumu hiyo Juni 30, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Agatho amesema uhamishaji wa kesi hiyo kutoka kwa Hakimu mmoja kwenda kwa mwingine ulikuwa na dosari kutokana na kutokuwekwa wazi sababu ya uhamisho wa jalada kama utaratibu wa kisheria unavyoelekeza.

Amesema wanatumia mamlaka waliyopewa chini ya kifungu cha 4(2) cha AJA na kubatilisha mwenendo na hukumu ya mahakama ya mwanzo, kufuta hukumu na amri zilizotolewa.


Msingi wa rufaa

Awali, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, mrufani alikana kutenda kosa hilo ambapo upande wa Jamhuri katika kuthibitisha kesi hiyo ulikuwa na mashahidi 11.

Shahidi wa kwanza ambaye ni mama wa marehemu, Paulina Uchena, amesema mrufani na mkewe (marehemu kwa sasa)  walikuwa wakigombana mara kwa mara  akidai mtoto (marehemu kwa sasa) alifanana na mdogo wa mrufani.

Aliiambia mahakama kuwa kabla ya mauaji hayo, Moshi (marehemu)  alikuwa amemkimbia mumewe (mrufani) pamoja na watoto wake watatu.

Shahidi wa pili ambaye ni mdogo wa mrufani, Lazima Matonya, alieleza kuwa mama yake alimweleza mrufani alimuua mkewe na mtoto na kuwa walitengana kwa sababu ya mtoto aliyejifungua ambaye mrufani alidai alifanana naye (Lazima).

Shahidi wa tatu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Juma Iddi aliieleza mahakama alishuhudia miili ya mama na mtoto waliokuwa wamechinjwa na kuwa awali alisuluhisha mgogoro wa wanandoa hao, na mrufani aliwahi kutishia kumuua mama yake kwa kisu.

Shahidi wa nne ambaye ni mama wa mrufani, Sada Hussein alieleza kuwa alikuta miili ya watu wawili wakiwa wamechinjwa kwenye nyumba ya mrufani.

Aliieleza mahakama kuwa siku za nyuma alikumbuka alipokuwa amembeba mtoto huyo wa pili wa mrufani (marehemu kwa sasa), mrufani alimuuliza kama anajua aliyembeba.

Shahidi wa tano ambaye ni kaka wa kwanza wa marehemu, Juma Daudi, aliieleza kuwa koromeo la mke wa mrufani (marehemu) lilikatwa kabisa huku shingo ya mtoto (marehemu) ikiwa karibu kukatwa lakini ni ngozi ya nyuma ya shingo pekee iliyobaki ikiunganisha kichwa na mwili.

Shahidi wa sita ambaye ni Mabuko Nkundi, aliyemkuta mrufani katika zahanati akiwa na mishale miwili tumboni mwake, alieleza kuwa marehemu na mrufani walikuwa na mgogoro wa muda mrefu.

Kufuatia mauaji hayo ya kikatili tukio hilo liliripotiwa polisi ambapo shahidi wa nane na wa tisa ambao ni G 2269 Rajab na Bagati Hande, waliunda timu ya uchunguzi ambapo pamoja na masuala mengine walirekodi maelezo ya onyo ya mrufani.

Kumbukumbu za mahakama hiyo zinaonyesha kuwa katika hali ya kushangaza shahidi wa saba, Mahona Samwel, alimshuhudia mrufani akijichoma mishale tumboni.

Shahidi wa 10, PC Fredrick alisema aliona kundi la watu wenye hasira wakikaribia kumuua mrufani ila aliokolewa na polisi.


Utetezi

Katika utetezi wake, mrufani  alikana kutenda makosa hayo na kudai kuwa maisha yake na marehemu (Moshi) yalikuwa na malalamiko mengi kwani aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mdogo wake (shahidi wa pili), ambaye aliishia kumpa ujauzito na kuwa siku ya tukio hakuwepo nyumbani.

Mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ya mauaji ilieleza kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha kesi hiyo bila kuacha  shaka yoyote, ikamkuta mrufani na hatia ya mauaji na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.


Rufaa


Katika rufaa hiyo mrufani aliwakilishwa na Wakili Kenani Aloyce huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili Joseph Makene na Aziza Mfinanga.

Mrufani huyo alikuwa na sababu tatu za rufaa ikiwemo Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza.

Wakili wa mrufani aliielekeza mahakama ukurasa wa 32 wa kumbukumbu ya rufaa hiyo ambayo inaeleza kuwa kulikuwa na amri ya uhamisho kutoka kwa Jaji Mfawidhi kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi, Gladys Barthy, aliyeongezewa mamlaka chini ya kifungu cha 256A (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kulingana na sehemu hiyo, Hakimu huyo ndiye aliyeongezewa mamlaka kwa wakati huo lakini kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi Juni 16, 2021, kesi hiyo ilipangwa tena kwa Hakimu Niku Mwakatobe aliyeongezewa mamlaka, kama inavyoonekana kwenye ukurasa wa 40 wa rekodi ya rufaa.

Hata hivyo, kabla ya kuendelea na shauri hilo kama inavyoonekana kwenye ukurasa wa 41 wa kumbukumbu ya rufaa, Jaji Mfawidhi, aliipanga upya kutoka kwa Niku kwenda kwa Hakimu Grabriel  Ngaeje kama kumbukumbu zinavyoonyesha kwenye ukurasa wa 42.

Wakili huyo alidai kuwa kulikuwa na makosa kwani Jaji mfawidhi badala ya kuhamisha kesi hiyo aliipanga tena kwa hakimu mwingine, huku akinukuu kesi ya Twaha Ridhiwani dhidi ya Jamhuri, iliyoelekeza kuwa mamlaka ya mahakama ni kuhamisha na siyo kupangiwa tena.

Aliieleza mahakama kuwa uhamisho huo ulipaswa kufanywa kwa hakimu aliyetajwa katika amri ya uhamisho na kuwa kutokana na hilo shauri, hukumu na amri iliyotolewa kinyume na kifungu cha 256A (1) cha CPA vifutwe kwa sababu hakimu huyo hana mamlaka.

Wakili huyo alipendekeza kwa kuwa Hakimu  hakuwa na mamlaka, hakuna rufaa yoyote mbele ya Mahakama hiyo hivyo kuwasihi majaji hao  kubatilisha mwenendo wa kesi, hukumu na amri na kutumia mamlaka chini ya kifungu cha 4(2) cha AJA ili kuamuru haki ya kusikilizwa upya kutokana na kukata rufaa.


Uamuzi majaji

Jaji Agatho alisema wanagusia kwa ufupi sheria ya uhamisho wa kesi kutoka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi na baada ya hapo, tutazingatia kama agizo la uhamisho lilikuwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema hatuna shaka kuhusu njia ya uhamisho au ugawaji upya kama  ilivyo sahihi katika Twaha Ridhiwani (supra) kifungu cha 256A cha CPA kinahusu uhamishaji wa kesi kutoka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi (Hakimu mwenye mamlaka ya ziada).

Jaji Agatho amesema kifungu hakitoi kukabidhiwa au kukabidhiwa upya kesi kama inavyofanywa katika kesi iliyopo ambapo kumbukumbu inaonesha kwa sababu zisizojulikana na kwa kutumia kifungu hicho cha 256A(1) cha CPA kesi hiyo ilikabidhiwa kwa Niku na Gladys.

Jaji amesema na baadaye  iliahirishwa tena toka kwa Niku kwenda kwa Grabriel.

Jaji huyo amesema kasoro nyingine ni ukosefu wa sababu za uhamisho wa jalada la kesi kama utaratibu wa kisheria, uhamishaji wa kesi kutoka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi lazima uhalalishwe kwa sababu au ushahidi wa aina fulani.

“Katika kesi hiyo, amri ya uhamisho uko kimya kuhusu sababu za kuhamisha tena jalada la kesi hiyo kutoka kwa Barthy, Niku hadi kwa Grabriel.

“Kwa sababu zilizotajwa hapo juu, tunaomba mamlaka tuliyopewa chini ya kifungu cha 4(2) cha AJA na kubatilisha mwenendo na hukumu ya mahakama ya mwanzo, kufuta hukumu, kufuta hukumu na amri zilizotolewa,” amehitimisha.

Jaji huyo aliagiza jalada lirejeshwe Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Tabora ili iweze kufanya marejeo na uamuzi sahihi wa kuhamishia shauri hilo kwa Hakimu Mkazi mwenye mamlaka ya ziada kwa ajili ya kusikiliza upya.