Mahakama kuamua iwapo basi la Kilimanjaro Express lipigwe mnada

Muktasari:
- Ni kwa ajili ya fidia iliyotokana na basi hilo kugonga gari na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi Septemba 11, 2024, kuhusu iwapo basi la Kilimanjaro Express litaendelea kupigwa mnada au mwenendo wa shauri la madai lililompa ushindi Leonard Kisena, aliyestahili kulipwa fidia ya Sh300 milioni, utaanza upya.
Fidia hii inatokana na ajali iliyosababisha kifo cha binti yake, Immaculate Kisena (16).
Uamuzi huo umetangazwa leo, Septemba 6, 2024 na Jaji Wilfred Dyansobera, baada ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd na pingamizi zilizowasilishwa na Kisena, kupinga maombi ya shauri hilo kuanza upya kwa.
Jaji Dyansobera ameeleza kuwa maombi hayo yaliletwa chini ya hati ya dharura, hivyo pingamizi na maombi ya msingi yatashughulikiwa kwa pamoja.
Wakili wa Kilimanjaro Truck Ltd, Dickson Ngowi, aliomba Mahakama itupilie mbali uamuzi wa Desemba 21, 2022, uliompa ushindi Kisena, akidai kuwa kuna taratibu za kisheria zilizokiukwa.
Hata hivyo, Wakili wa Kisena, Dk Aloys Rugazia, akisaidiana na Valentine Charles, amedai kuwa makosa ya kimwenendo hayawezi kusahihishwa katika mahakama hiyohiyo iliyotoa hukumu, badala yake waleta maombi walipaswa kukata rufaa kwa mujibu wa Sheria ya Madai (CPC), Kifungu cha 70 (2).
Pia aliongeza kuwa maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda.
Rugazia alibainisha kuwa waleta maombi walipuuza fursa ya usuluhishi, ambapo walikosekana mara tatu, hivyo, jalada lilirejeshwa kwa Jaji Mgonya na kesi iliendelea bila waleta maombi kufika mahakamani. Kutokana na hilo amesema haoni sababu ya kuanza upya kwa shauri hilo.
Ameongeza kuwa mteja wake, licha ya kupata madhara makubwa kwa kupoteza mtoto, pia alikabiliwa pia na dharau za wadaiwa, ambao hawakuchukua hatua zozote za kibinadamu baada ya ajali hiyo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Dyansobera aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 11, 2024, kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Wakati huo huo, basi la Kilimanjaro aina ya Scania liko mikononi mwa dalali wa mahakama, Daniel Mbuga wa Legit Auction Mart, likitarajiwa kupigwa mnada Septemba 13, 2024 kulipa fidia hiyo.
Kesi hiyo ilianzia kwenye ajali iliyotokea Desemba 24, 2021, eneo la Kerege, Bagamoyo, ambapo basi la Kilimanjaro liliparamia gari la Kisena, aina ya Toyota Landcruiser, na kusababisha kifo cha binti yake mwenye umri wa miaka 16.
Kisena na familia yake walikuwa wakielekea Kilimanjaro kusherehekea Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Dereva wa basi hilo, Mjahid Mohamed, alifunguliwa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo kwa makosa manne: kuendesha gari lisilokuwa na bima, kusababisha kifo, majeraha, na uharibifu wa mali kutokana na uzembe.
Alikiri makosa hayo na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh110, 000 kwa makosa yote, au kifungo cha miezi sita jela.
Baada ya hukumu hiyo, Kisena alifungua kesi ya madai dhidi ya Kampuni ya Kilimanjaro Truck Company Limited, mkurugenzi wake Rowland Sawaya, na dereva Mjahid Mohamed, akidai fidia ya Sh400 milioni kwa madhara ya ajali hiyo, ikijumuisha gharama za matibabu, mazishi, na uharibifu wa gari lake.
Kesi hiyo, iliyosikilizwa na Jaji Leila Mgonya, ilimalizika kwa hukumu Desemba 21, 2022, ambapo mahakama iliagiza kampuni hiyo imlipe Kisena fidia ya Sh300 milioni, pamoja na riba ya asilimia saba kwa mwaka hadi malipo yakamilike.
Hata hivyo, utekelezaji wa hukumu haukufanyika, hivyo Kisena alirudi mahakamani kukazia hukumu hiyo.