Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ilivyokataa utetezi wa Polisi kumshikilia mfanyabiashara siku 48

Muktasari:

  • Sheria inaelekeza mtuhumiwa anapokamatwa kwa tuhuma za makosa yanayodhaminika kufikishwa mahakamani si zaidi ya saa 24, lakini katika matukio mengi watuhumiwa wamekuwa wakishikiliwa na polisi kwa miezi bila kufikishwa mahakamani.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Moshi, imeliagiza Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kumuachilia huru, kumpatia dhamana au kumfikisha mahakamani mara moja mfanyabiashara Mussa Majeba, ambaye amekuwa akishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi kwa zaidi ya siku 48 bila kufikishwa mahakamani.

Amri hiyo imetolewa na Jaji Safina Simfukwe Mei 8, 2025, kufuatia shauri la maombi ya amri ya kuachiliwa au kufikishwa mahakamani alilolifungua Majeba, baada ya kukataa hoja za utetezi wa wajibu maombi.

Jaji Simfukwe amefikia uamuzi chini ya  kifungu cha 390(1)(a) na (b) cha Sheria ya Mwenendo wa  Makosa ya Jinai (CPA) baada ya kujadili hoja za pande zote na kesi rejea, na kukubaliana na mwombaji kuwa alikuwa akishikiliwa kituoni hapo muda wote huo kinyume cha Sheria.

Amesema kuwa chini ya kifungu cha 32(1), (2) na (3) cha CPA, mtu awe amekamatwa kwa hati au bila hati ya ukamatwaji kama ni kosa linalodhaminika anapaswa kufikishwa mahakamani bila kucheleweshwa bila sababu.

“Iwe ndani ya saa 24 au ‘mara tu inapowezekana’ hakuna tofauti,” amesema Jaji Safina Simfukwe, akisisitiza kuwa muda wa kumfikisha mtu mahakamani baada ya kukamatwa hautakiwi kuvukwa bila sababu za msingi.

Alisema hayo wakati akitoa uamuzi wa shauri hilo, huku akirejea hukumu mbalimbali za Mahakama ya Rufani pamoja na Ibara ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolinda haki na uhuru wa mtu binafsi kuwa huru.

“Tangu mwanzo, napenda kuweka wazi kuwa, iwe mwombaji ameshikiliwa kwa zaidi ya siku 48 au hata siku 14; iwe masharti ya dhamana yalitolewa au la; iwe alishindwa kuyatimiza au hakuyatimiza wajibu maombi walilazimika kufuata masharti ya sheria,” alieleza Jaji Simfukwe kwa msisitizo.

Akiendelea kutoa ufafanuzi, alisema kuwa kwa makosa kama ya wizi au kuuza mali zinazotuhumiwa kuwa za wizi, muda wa siku 48 au 14 hauwezi kufasiriwa kuwa ni “mara tu inapowezekana” kama inavyotakiwa kisheria. “Sheria iko wazi mtu anapaswa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 au mapema iwezekanavyo, si vinginevyo,” alisisitiza.

Jaji Simfukwe aliongeza kuwa hata kama ingechukuliwa kuwa mwombaji alishindwa kutimiza masharti ya dhamana ya polisi, bado polisi walipaswa kumpeleka mahakamani hata kwa kutumia hati ya mashtaka ya muda ikiwa kulikuwa na nia ya kumfikisha katika mahakama ya mkoa tofauti na Kilimanjaro.

“Kwa kuzingatia msingi wa sheria na mamlaka ya Mahakama hii, ninaona kuwa maombi haya yana mashiko,” alihitimisha Jaji Simfukwe, akieleza kuwa Jeshi la Polisi lilikiuka haki za msingi za mwombaji kwa kumshikilia kwa muda mrefu kinyume na taratibu za kisheria.

“Hivyo basi, ninaamuru kuwa mwombaji aachiwe huru kutoka kwenye kizuizi cha wajibu maombi au afunguliwe mashtaka katika mahakama yenye mamlaka ndani ya masaa 48 au apewe dhamana kama sheria inavyoelekeza", ameamuru Jaji Simfukwe.

Majeba alikamatwa na polisi Machi 14, 2025 katika eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za wizi. Baada ya kukamatwa, alisafirishwa hadi mkoani Kilimanjaro ambako amekuwa akishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi bila kufikishwa mahakamani hadi alipofungua shauri hilo la maombi.

Wajibu maombi katika shauri hilo la maombi ya jinai mchanganyiko namba  10494 ya mwaka 2025 walikuwa ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) na Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kilimanjaro.

Wengine walikuwa ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Wilaya ya Moshi, Mkuu wa Upelelezi Kituo Kikuu cha Polisi Moshi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). 

Katika shauri hilo aliomba, mahakama iridhie kuamuru achiliwe huru mara moja, ama wajibu maombi wafike mahakamani kueleza  kwa nini wasimwachilie kutoka kizuizini kisicho halali kituoni hapo.

Pia, aliomba mahakama itoe amri kuwazuia wajibu maombi wasimshikilie kwa kipindi kirefu zaidi ya kile kinachoruhusiwa na sheria, iwalazimishe wamwachilie huru kwa mujibu wa sheria.

Katika  kiapo cha Wakili Kimaro, kilichounga mkono maombi hayo, Majeba ni mkazi wa Mkoa wa Mwanza na mfanyabiashara wa vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta mpakato na vifaa vya simu jijini Dar es Salaam.

Baada ya kukamatwa siku hiyo, Machi 14, 2025, huko Mikocheni Dar es Salaam, alipelekwa kituo cha Polisi Chang’ombe.

Huko  alielezwa kuwa amekamatwa kwa kosa la kuiba kompyuta mpakato moja, kompyuta aina ya ‘tablet’ moja na bastola moja mali ya Minja, mfanyakazi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanapa).

Aprili 22, 2025,  alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi  na tangu wakati huo, aliendelea kumshikiliwa kituoni hapo (Moshi) japo kosa  alilokiwa anatuhumiwa linadhaminika.

Katika kiapo chake Wakili wa Serikali,  Ramadhani Kajembe, kwa niaba ya wajibu maombi alipinga maombi hayo.

Alidai kuwa mwombaji  yuko chini ya ulinzi wa wajibu maombi akidai kuwa anafanya biashara haramu ya kuuza kompyuta mpakato zilizoibiwa.

Pia, Wakili Kajembe , alidai kuwa mwombaji alipewa masharti ya dhamana ambayo hajatimiza hadi sasa. 

Wakati maombi haya yaliposikilizwa kwa njia ya mdomo, wakili  Kimaro  alidai kuwa mwombaji alikamatwa bila hati ya kukamatwa, hivyo alitakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 au kupewa dhamana ya polisi.

Alidai kuwa iwapo walitaka kuendelea kumshikilia, walipaswa kuomba ruhusa ya mahakama, lakini  wameendelea kumshikilia kwa zaidi ya siku 48 kinyume na kifungu cha 32 cha CPA na Ibara ya 13(6) na 15 ya Katiba ya Nchi.

Kuhusu madai ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana Wakili Kimaro alipinga hoja hiyo akidai kuwa hata wakili wa Serikali kwa hakuyaeleza (kama kweli mwombaji alipewa).

Akijibu hoja hizo wakili Kajembe pamoja na mambo mengine alidai kuwa mwombaji ameshikiliwa kwa wiki mbili tu na kwamba  alikamatwa kwa hati ya kukamatwa, chini ya  kifungu cha 32(3) cha CPA. 

Hivyo alidai kuwa chini ya kifungu hicho, mtuhumiwa anatakiwa kufikishwa mahakamani mara tu inapowezekana na kwamba hivyo sharti la saa 24 halihusiki katika kesi hiuo.

Alifafanua kuwa “mapema iwezekanavyo" inategemea busara ya mahakama na akasisitiza kiwa mwombaji yuko chini ya ulinzi wa polisi kwa sababu hana mdhamini.