Maganga wa CWT asimamishwa ualimu, asema alishaacha kazi

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya
Muktasari:
- Barua ya Manispaa ya Temeke iliyoonekana mitandaoni imeeleza kuwa Maganga amesimamishwa kwa tuhuma za utoro kazini, kukaidi au kukataa maelekezo halali ya viongozi wake.
Dar/Dom. Wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya akitangaza kusimamishwa kazi kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japhet Maganga, mwenyewe amesema alishaacha kazi hiyo tangu mwaka 2017.
Maganga alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Tandika iliyopo Kata ya Tandika, Dar es Salaam.
Mwananchi limeiona barua iliyotolewa na kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha Manispaa ya Temeke, Francisca Melemo ya Desemba 5, 2023 ikieleza kuwa Maganga amesimamishwa kazoo kwa tuhuma za utoro kazini, kukaidi au kukataa maelekezo halali ya viongozi wake.
Hata hivyo, akizungumza leo Desemba 7, 2023 na Mwananchi, Maganga alieleza kushangazwa na barua hiyo, kwani yeye ni mwajiriwa wa mkataba wa kudumu wa CWT.
Maganga amesema kinachofanyika ni vita vya madaraka na waliondolewa kwenye uongozi na kwamba yeye alikoma kupokea mshahara na marupurupu yote kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Temeke tangu Desemba 2017, baada ya kuajiriwa kwenye nafasi ya uhasibu, Makao Makuu ya CWT.
“Unanisimamishaje kwa kazi ambayo sina haja nayo. Kama ni mtoro kazini, sheria inasema mtumishi akikosekana kazini kwa siku tano, amejifukuzisha kazi. Mimi sijaripoti tangu waliposema Oktoba mosi, wamalize kazi,” amesema.
Amesema yeye ni mtumishi mwenye ajira ya kudumu CWT na aligombea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu CWT Juni 5, 2020 na alishinda nafasi hiyo, huku Katibu Mkuu wake akiwa ni Deus Seif na alipopata matatizo ndiyo akachaguliwa kwenye nafasi hiyo.
“Mimi najua haki zangu. Ibara ya 30 ya Katiba ya CWT inaelekeza kwamba watumishi wa chama wa kuajiriwa wana haki ya kugombea, lakini si kupiga kura,” amesema.
Maganga amesema kwa ibara hiyo yeye akiwa mwajiriwa wa CWT alikuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi na alitoka Temeke na kujiunga na CWT kwa kuajiriwa kwenye nafasi ya mhasibu wa chama na si kiongozi wa kuchaguliwa.
Januari 25 mwaka 2023, Maganga na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya, lakini hawakwenda kuapa.
Leah aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, wakati Maganga akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Septemba 23, 2023 Maganga alitakiwa kurejea katika kituo chake cha kazi kupitia tangazo kwa umma lililotolewa na mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.
Katika tangazo hilo, inaonyesha Maganga aliomba kibali cha kuazimwa CWT kwa mara ya kwanza Agosti 2017 kilichomalizika Septemba 30, 2020.
Awali, Maganga aliomba nyongeza ya kibali cha kuazimwa Juni mosi mwaka 2020 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi alimpa nyongeza Agosti 10 mwaka 2020 kinachoishia Septemba 30, 2023.
Tangazo hilo lilisema Maganga aliomba tena kibali cha kuazimwa kwa mara ya tatu, lakini katibu mkuu utumishi hakuridhia maombi hayo.
“Hivyo, basi mwalimu Japheth Maganga anapaswa kurejea kwenye kituo chake cha kazi mara moja Oktoba mosi, 2023,” linaeleza tangazo hilo.
Hata hivyo, Deus Seif na aliyekuwa mweka hazina wa chama hicho, Abubakar Alawi walifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma wakiomba Mahakama ichukue hatua kwa uongozi wa CWT kwa kukiuka amri halali ya Mahakama ya kuzuia mkutano mkuu uliomchagua Maganga kufanyika.
Hali hiyo inakuja wakati Maganga akiwa katika shinikizo la kusitisha maadhimisho ya miaka 30, ili Sh7 bilioni zilizopangwa kutumika zitatue changamoto zilizopo.
Shinikizo hilo limetokana na barua ya mmoja wa wanachama, Victor Kazoba aliyedai kuwa maadhimisho hayo ni mwanya wa upigaji fedha za umma na matumizi mabaya.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Maganga alisema hawajapata barua hiyo ofisini na punde wakiipata watatoa majibu kwa njia ya maandishi.
Naye Rais wa CWT, Leah Ulaya anayedaiwa kutumiwa barua hiyo alisema hajaiona, ingawa amepata taarifa ya uwepo wake.