Rais CWT aomba vyombo vya Serikali viache kuwaingilia

Rais wa CWT, Leah Ulaya akisikiliza jambo kutoka kwa mmoja wa wajumbe. Picha na Habel Chidawali
Muktasari:
- Baraza la CWT linafanyika huku kukiwa na mkanganyiko kuhusu hatima ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga ambaye kibali alichoomba kwa mwajiri wake kinakoma Septemba 30, 2023 wakati nafasi yake itakwenda hadi mwaka 2025.
Dodoma. Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Leah Ulaya amevitaka baadhi ya vyombo vya Serikali kuacha kuingilia mambo ya chama hicho na wakiache kisimame chenyewe.
Ulaya ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 25, 2023 wakati akifungua kikao cha dharura cha Baraza Kuu la CWT ambapo ametaka viongozi wa chama hicho ngazi ya mikoa kukataa kuingiliwa na mamlaka zingine.
Kauli ya kiongozi huyo imetolewa saa chache baada ya vuta nivute iliyotokana na polisi kuzuia mkutano huo kwa kile walichosema kuna maelekezo kutoka uongozi wa juu.
Polisi walifunga lango la kuingia katika ofisi za CWT makao makuu zoezi lililodumu kwa saa 1.20 kabla ya kupatikana kwa mwafaka na kuruhusiwa waendelee na kikao.
"Tunataka kusimama sisi wenyewe bila kuingiliwa na vyombo vingine, tusiingiliwe kwani tunafanya mambo yetu bila kuvunja sheria, tumechoka kufanya mikutano chini ya Polisi," amesema Ulaya.
Kiongozi huyo amewataka wajumbe ambao watakuwa na fikra tofauti kuhusu baraza hilo watoke nje ili waruhusu mkutano uendelee.
Amesema chama hicho kinapitia misukosuko na changamoto nyingi lakini kimesimama imara kwa sababu viongozi wake wako imara na wataendelea kuwa imara zaidi bila kuyumbishwa.
Ameomba ofisi ya msajili wa vyama isiyumbishwe kwa namna yoyote kwani kilichofanyika CWT ni udhalilishaji licha ya ukweli kuwa wako tayari kufanya kazi na Serikali.