Vuta nikuvute polisi wazuia kikao cha CWT

Polisi wakiwa wamesimama langoni kuzuiwa wajumbe wa Baraza la CWT wasiingie ndani ya jengo lao kuendelea na kikao chao leo Jumatatu Septemba 25, 2023.
Muktasari:
- Vute nikuvute Chama cha Walimu wakishinda kuanza kikao cha baraza baada ya kuzuiwa kwa zaidi ya saa moja.
- Baraza la CWT limekutana kwa kikao cha dharura, huku baadhi ya ajenda zikitajwa ni kujadili bajeti na kupitisha mishahara ya waajiriwa wapya.
Dodoma. Kikao cha Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimekwama kwa saa 1.23 huku kukiwa na mabishano makali na polisi.
Baraza hilo linakutana huku Mtendaji Mkuu wa CWT, Japheth Maganga akiwa amebakiza siku 5 za kibali alichoomba kutoka kwa mwajiri wake na kutakiwa kurudi kwa mwajiri wake ifikapo Oktoba mosi mwaka huu.
Mvutano huo umeanza leo Jumatatu Septemba 25, 2023 saa 3.00 asubuhi na kuhitimishwa saa 4.23 asubuhi baada ya Polisi kuruhusu baraza liendelee.
Sarakasi zilianza muda huo wakati wajumbe wa Baraza Kuu walipoanza kuingia eneo la kikao katika ofisi za CWT Mtaa wana Jamhuri na kukuta Polisi wenye silaha wakiwa wamefunga lango la kuingia na kutaka walioko ndani wabaki huko na wale wa nje wasiingie ndani.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Polisi Dodoma, Joram Samson aliongoza kikosi cha polisi 12 huku watano wakiwa na silaha za moto na wengine hawakuwa na sare ambao idadi yao haikufahamika.
"Tumepokea maagizo ya mdomo kutoka kwa viongozi wa juu kwamba hiki mnachotaka kukifanya kisifanyike, tunaomba mtawanyike," amewaambia Samson.
Kauli hiyo ilizua mvutano mkali na kuanza kurushiana maneno makali kati ya polisi waliozuia lango na walimu licha Mkuu wa Kituo cha Polisi kuendelea kutuliza hali akitaka Walimu wawe wapole wakati anaendelea kushughulikia jambo lao.
Saa 4.21 asubuhi kiongozi wa polisi ametoka kuzungumza na simu ya mkono pembeni kidogo kisha akawaita walimu na kuwatangazia kuendelea na kikao chao.
"Nimewaiteni hapa kuwaambia kuwa mmeruhusiwa kuendelea na kikao chenu lakini tunataka amani, hii simu nimetoka kuzungumza na Rais wenu (Leah Ulaya) ambaye ameniunganisha na msajiri wa vyama, tumeelewana na mmeruhisiwa," amesema Samson.
Busara ya Polisi huyo iliwaokoa pia baadhi ya Walimu kwani baada ya kuruhusiwa kuingia ndani, waliwakamata baadhi ya Walimu ambao ilielezwa walitoa matusi lakini akaamuru waachiwe waendelee na mkutano wao.
Awali Baraza hilo likipangwa kufanyika ukumbi wa Hotel ya St Gasper lakini ghafla usiku wa kuamkia leo walielezwa ukumbi hauna nafasi licha kwamba walishalipia.