Prime
Aliyekataa u-DC arejeshwa shuleni

Katibu Mkuu Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japhet Maganga
Muktasari:
- Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japhet Maganga akitakiwa kurejea katika kituo chake cha kazi kuanzia Oktoba mosi, Rais wa chama hicho, Leah Ulaya amesema iwapo atarejea atakuwa amepoteza sifa za kuendelea kuongoza katika nafasi hiyo ya utendaji.
Dodoma. Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japhet Maganga akitakiwa kurejea katika kituo chake cha kazi kuanzia Oktoba mosi, Rais wa chama hicho, Leah Ulaya amesema iwapo atarejea atakuwa amepoteza sifa za kuendelea kuongoza katika nafasi hiyo ya utendaji.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu agizo hilo la kumtaka arejee kazini, Maganga alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hajapata barua rasmi kutoka kwa mwajiri wake.
Januari 25 mwaka huu, Maganga, Rais wa CWT, Ulaya na Makamu wa Rais, Dinna Mathaman waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya, lakini ni Mathaman pekee ndiye alikubali uteuzi huo kwenda wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Ulaya ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita na Maganga Kyerwa mkoani Kagera, hawakujitokeza kwenda kuapa kutumikia nafasi hizo.
Alipoulizwa na waandishi wa habari, Januari 31, 2023 aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama alisema uteuzi wa Rais ni heshima kubwa ya hali ya juu inayoendana na madaraka makubwa ya kikatiba ambayo amepewa.
“Sisi kama menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora tunachokisubiri taarifa rasmi kwenye wizara zinazohusika, kwa sababu wale ni viongozi wa chama cha wafanyakazi ambao wanasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, lakini ni watumishi wanaofanya kazi kwenye Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),” alisema Mhagama.
Hata hivyo, alisema kama wangepatiwa taarifa hizo, ndani ya Serikali wangeona wafanye jambo gani mahususi kulingana na jambo hilo lililojitokeza.
Wakati hali ikiwa hivyo, juzi tangazo la ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam lilimtaka Maganga arejee katika kituo chake cha kazi baada ya maombi yake ya kuongezwa muda kuwa nje ya kazi kukataliwa.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, Maganga aliomba kibali cha kuazimwa na CWT kwa mara tatu na kukataliwa, baada ya kuwa amekubaliwa kwa vipindi viwili vya miaka mitatu kila kimoja.
Mara ya kwanza alipewa kibali Agosti 2017 ambacho kilimalizika muda wake Septemba 30, 2020, kisha aliomba nyongeza ya kibali Juni mosi 2020 na Ofisi ya Rais Utumishi iliridhia Agosti 10, mwaka 2020, ambacho kinaisha Septemba 30, mwaka huu.
Maganga ambaye cheo chake ni mwalimu mwandamizi, aliomba tena kibali cha kuazimwa kwa mara ya tatu, lakini katibu mkuu Utumishi hakuridhia maombi hayo, hivyo analazimika kurejea kazini.
“Hivyo basi Mwalimu Japhet Maganga anapaswa kurejea kwenye kituo chake cha kazi mara moja Oktoba mosi, 2023,” imeandikwa katika tangazo hilo.
Akizungumza Mwananchi jana, Maganga alisema hajapata barua rasmi kutoka kwa mwajiri wake bali amesoma taarifa hizo mtandaoni.
Alisema ofisi yake haijamtendea haki kwa kutoa taarifa zake ikiwemo namba yake ya mshahara (check number) katika mitandao ya kijamii ambako kunaweza kusababisha wahalifu kuzitumia kwenye kujipatia mkopo benki na kumsababishia matatizo.
“Itoshe kusema kuwa sina taarifa rasmi ya mwajiri wangu kunitaka kurejea kazini, nimeona jana katika mitandao ya kijamii tu,” alisema Maganga aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu kabla ya kuchaguliwa katibu mkuu.
Akizungumzia suala hilo, Ulaya alisema ikifika Septemba 30, mwaka huu, ambao ni ukomo wa kibali cha Maganga ndipo watajua kama mwajiri atamrejesha kwake (manispaa ya Temeke) au ataridhia aendelee kuitumikia CWT.
Alisema endapo ataondoka, utaratibu wa nani anachukua nafasi yake, utapangwa na vikao vya CWT baada ya kupata rasmi barua kutoka kwa mwajiri wake.
Alisema kila Septemba CWT hufanya kikao cha Baraza la Taifa ambalo kazi yake kubwa ni kufanya mapitio ya bajeti na mambo mengine ambayo huainishwa kikatiba.
Ulaya alisema kwa nafasi za kiutendaji kama aliyonayo Maganga na makatibu wa chama hicho wilaya na mikoa, zinapaswa kushikwa na walimu ambao ni waajiriwa wa umma.
Maganga alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu Desemba mwaka akichukua nafasi ya Deus Seif.