Mafinga kutumia Sh1 bilioni kuweka taa za barabarani 180

Mufindi. Jumla ya kiasi cha Sh 1 bilioni zinatarajiwa kutumika katika mradi wa uwekaji wa taa 180 za barabarani za Halmashauri ya Mji wa Mafinga umbali wa kilomita 5 kwa ajili ya kuwarahisishia wananchi kuweza kufanya biashara zao kwa urahisi.
Akizungumzia mkataba huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Regnant Kivinge amesema kuwa halmashauri hiyo imesaini mkataba na Wakala wa Umeme Vijiji (REA) wa Sh500 milioni kwa ajili ya uwekaji huo wa taa umbali wa kilomita 5.
Aidha Kivinge amesema katika utekelezaji wa Miradi huo mnufaika ambao ni halmashauri wamechangia kiasi cha Sh500 milioni kwa ajili ya gharama ya mradi huo ambayo thamani ya mradi huo ni kiasi hicho ni Sh1 bilioni.
Pia mwenyekiti huyo amesema kuwa mradi huo wa taa za barabarani utasaidia kukuza uchumi wa Mji wa Mafinga kutokana na wafanyabiashara wataweza kufanya biashara zao kwa uhuru na usalama bila kuwepo kwa changamoto yoyote sanjari na kuweka mji huo katika mwonekano nzuri.
Kwa upande wake Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema ni fahari kwa wananchi wa Mji Mafinga kupata mradi huu wa taa za barabarani ambazo zitawekwa umbali wa kilomita 5 jambo ambalo litawasidia kufanya biashara zao muda wote.
“ Wananchi wa Mafinga wamekuwa wakisubiri mradi huu kwa shauku kubwa kwa sababu wafanyabiashara wataweza kutafanya biashara zao masaa 24, ukizingatia tumepambana kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mji Mafinga mpaka mradi umekuja," amesema Chumi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Happiness Laizer alisema kuwa Mradi utatekelezwa kwa siku 120 baada ya kusainiwa mkataba huo maeneo ambayo yataguswa na mradi huo katika uwekaji wa taa za barabarani ambayo ni Kinyanambo A,B,C yenye umbali wa km1.9 huku Mafinga hospitali ikiwa na km 0.2
Maeneo mengine ambayo yatawekwa taa katika mradi huo kuwa CF plazer- tanki la maji pipeline km 0.4, NSSF- Bomani km 0.9, Luganga- Mgololo km 0.1, Mashujaa - Royal Park Hotel km 0.2, Chaibora- Dembe km 0.1, NMB-Mashujaa-Mashine ya Mpunga km 1.2.
Pia Mkurugenzi huyo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais wa Jamhuri wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa malengo yake kupitia REA ili kuhakikisha wananchi wote hasa maeneo ya vijijini wanapata nishati bora ikiwemo Mji wa Mafinga ambao unakuwa kiuchumi.
Awali akizungumza kabla ya saini mkataba huo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia, Mhadisi Advera Mwijage alisema kuwa wanaishukuru halmashauri hiyo kwa kufanikisha kusainiwa kwa mkataba huo huku akisema watahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.